Tafuta

Tangazeni na Kushuhudia Injili ya Msamaria Mwema: Huduma Makini

Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama Mitume Wasafiri, waliona na kuhurumia. Mwinjili Luka anakazia kuhusu Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alimwona, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai. Huu ndio wito na mwaliko anaoutoa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Baba Mtakatifu anakaza kusema, huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. 

Waamini anaitwa na kutumwa kuwa mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu
Waamini anaitwa na kutumwa kuwa mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu

Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho zinazofumbatwa katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili kwani kimsingi wao wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya kwanza vya huruma ya Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa inaweka mbele ya macho ya waamini Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema. “Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 10 Julai 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amechambua kuhusu huruma na upendo ulioshuhudiwa na Msamaria mwema aliyekuwa anasafiri. Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama Mitume Wasafiri, waliona na kuhurumia. Wito kwa kila mwamini kuwa na huruma kwa maskini na wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mwinjili Luka anakazia kuhusu Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alimwona, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai. Huu ndio wito na mwaliko anaoutoa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Rej. Yn 14:6.

Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.
Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.

Wanafunzi wa njia anasema Baba Mtakatifu Francisko wanapaswa kufikiri na kutenda huku wakifuata nyayo za Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kama ilivyokuwa kwa Msamaria, waamini wajifunze kuona ukweli ulivyo na hivyo kuwa na huruma, kinyume kabisa cha na mwelekeo kwa Kuhani na Mlawi, ambao kimsingi walipaswa kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wahitaji. Hakuna sababu ya kuwanyooshea watu wengine kidole, bali kwa sasa kila mwamini anaalikwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuachana kabisa na ubinafsi pamoja na uchoyo wake, tayari kufuata nyayo za Kristo Yesu. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili aweze kuwakirimia uwezo wa kuona na kuwa na huruma kwa maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali, ili kuwatangazia tena Injili ya matumaini, ili hatimaye, waweze kuinuka na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awaongoze katika ukomavu wa njia hii. Awaoneshe Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni “wanafunzi wa njia.”

Injili ya Msamaria Mwema

 

10 July 2022, 15:26

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >