Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Maji: Uponyaji na Utakaso
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, tayari kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya wa matumaini, kama ndugu wamoja! Baba Mtakatifu Francisko alitamani kuona kwamba, sherehe ya upatanisho wa Kitaifa inaadhimishwa huko Edmont kwenye Madhabau ya Kitaifa ya “Ziwa la Mtakatifu Anna” “Lac Ste. Anne” ili kutoa fursa kwa wagonjwa na wale wote waliojeruhiwa kupata nafasi ya kujitakasa, tayari kuanza kutembea katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaosimikwa katika utamadunisho na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kama kielelezo cha imani tendaji! Haya ni matembezi ya mshikamano wa pamoja katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, tayari kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kwa makini. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi.
Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa kutembea katika njia ya upatanisho na uponyaji, ili kutakasa kumbukumbu, na hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na Injili ya matumaini. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 26 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Neno la Mungu kwenye Madhabau ya Kitaifa ya “Ziwa la Mtakatifu Anna” “Lac Ste. Anne” yaliyoko mjini Quèbec, Canada. Hapa ni mahali ambapo waamini na watu wenye mapenzi mema, wameonja huruma na upendo wa Mungu kwa kuponywa magonjwa na kuondolewa dhambi zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. “Ziwa la Mtakatifu Anna” “Lac Ste. Anne” ni mahali ambapo waamini wamepyaisha imani na ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewaalika waamini kurejea tena kwenye chemchemi ya imani, mahali muafaka pa kutangaza, kushuhudia na kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa sababu maji ni chanzo cha uhai, maji yanatakasa na kuponya.
Ni katika madhabahu haya, mchakato wa utamadunisho unaweza kupata nguvu na maana yake halisi, kwani ni mahali pa kuwakutanisha watu katika: Neno, Sala na Huduma ya uponyaji tayari kuendelea kushikamana na kutembea na Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Ziwa la Mtakatifu Anna” “Lac Ste. Anne” ni kielelezo cha uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuilinda, kuitunza na kuiendeleza na kwa njia hii, mwanadamu anaweza kurejea tena kwa Mungu chanzo na asili ya uhai na imani kwa Kristo Yesu. Kama ilivyokuwa wakati wa Yesu, kwenye Ziwa la Galilaya ambako alikutana na watu wa kila aina na hapo akwatangazia Habari Njema ya Wokovu, huku akiwataka wawe ni vyombo vya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Na kwa njia hii, Ziwa la Galilaya likawa ni eneo maarufu sana la kutangaza, kushuhudia na kujenga udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika ushirika mkamilifu, kwa kutambua na kuheshimu tofauti msingi zinazojitokeza. Maji ni chanzo cha uhai na mahali ambapo watu watakatifu wa Mungu wanagangwa na kuponywa magonjwa yao.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, maji ni chanzo cha uhai na imani ambayo inarithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine. Maji ni chemchemi ya uponyaji wa magonjwa mbalimbali yanayomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, ili hatimaye, kumkirimia amani na utulivu wa ndani. Maji haya yasaidie kuganga na kuponya madonda yaliyosababishwa na athari za mifumo mbalimbali ya ukoloni na ubaguzi wa rangi, ili kwamba, kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria, asaidie kweli kukoleza mchakato wa upatanisho na utamadunisho kwa kuthamini na kuenzi tamaduni, mila na desturi njema kutoka kwa watu asilia wa Canada. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu wa imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni chombo cha kuganga na kutakasa, ili kuwawezesha watu kusimama katika ukweli, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Kanisa ni mahali pa kuwakutanisha watu wote wa Mungu katika Neno, Sakramenti na huduma, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kama kielelezo cha imani tendaji.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Ziwa la Mtakatifu Anna” “Lac Ste. Anne” liwawezeshe waamini kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba na kifo laini. Liwe ni chemchemi ya matumaini kwa vijana waliokata na kujikatia tamaa ya maisha; vijana ambao wanauza uhuru wao kwenye simu za viganjani; vijana ambao hawana dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, wamekuwa kama “Daladala zilizokatika usukani.” Ziwa hili liwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wanaotaka kuona mabadiliko katika maisha, ili wapate upendo na kuonja faraja kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili aweze kugusa undani wa maisha yao, na hatimaye, kuganga na kuyatakasa. Na wakisha kutakasika, wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kwa kuwashirikisha wengine amana na utajiri unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao.