Tafuta

Baba Mtakatifu amegusia lengo la hija yake ya Kitume katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho. Baba Mtakatifu amegusia lengo la hija yake ya Kitume katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho.  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Watu Asilia wa Canada

Baba Mtakatifu amegusia: Mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho. Amana na utajiri aliochota kwa kukutana na watu wa Mungu pamoja na umuhimu wa kuendeleza dhamana na wajibu wa wanawake katika jamii, kwa kufuata mifano bora ya wanawake watakatifu. Canada ni nchi kubwa na hivyo safari ya uponyaji na upatanisho unahitaji subira na uvumilivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko  Kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe Jumamosi, tarehe 30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada kama sehemu muhimu sana ya Kanisa katika uinjilishaji na utamadunisho wa tunu msingi za Kiinjili. Mama Kanisa anawajibika kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete katika wongofu wa kitamaduni unaothamini tamaduni, mila na desturi njema za watu mahalia. Huu ni uinjilishaji unaosimika mizizi yake katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kutakasa na kukuza tamaduni, mila na desturi njema, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Askofu wa Jimbo kuu la Quèbec.

Papa Francisko tarehe 29 Julai 2022 amekutana na watu asilia wa Canada
Papa Francisko tarehe 29 Julai 2022 amekutana na watu asilia wa Canada

Amekutana na “kuchonga” kwa faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Canada hasa wakati huu wanapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola unaofikia kilele chake tarehe 31 Julai 2022. Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola imekuwa ni fursa ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kuweza kuyapatanisha yote na Kristo Yesu, anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Umekuwa ni muda wa kuuendea ulimwengu, kusaidia roho za watu na kuyaangalia mambo yote mapya katika jicho la Kristo Yesu. Wayesuit wanapaswa kujinyenyekesha na kuwaachia wengine nafasi ili waweze kuwasaidia. Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Wote wanaweza kuokolewa kama jumuiya au kuangamia na wala hakuna njia ya mkato. Ni Yesu peke yake ambaye amewaonesha njia, hivyo ni wajibu wao kusaidiana kutafuta na hatimaye, kuambata njia inayokwenda kwa Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada wanaoishi mjini Quèbec na hivyo kuhitimisha shughuli zake Jimbo kuu la Quèbec na kuelekea Iqaluit, maana yake ni sehemu yenye samaki wengi.

Papa Francisko amesikiliza shuhuda na matamanio yao halali.
Papa Francisko amesikiliza shuhuda na matamanio yao halali.

Baba Mtakatifu amegusia lengo la hija yake ya Kitume katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho. Amana na utajiri aliochota kwa kukutana na watu wa Mungu nchini Canada pamoja na umuhimu wa kuendeleza dhamana na wajibu wa wanawake katika jamii, kwa kufuata mifano bora ya wanawake watakatifu. Baba Mtakatifu anasema Canada ni nchi kubwa na hivyo safari ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa ni jambo ambalo linahitaji subira. Amekwenda kati yao kama hujaji ili kukutana, kuzungumza, kusikia na kujionea mwenyewe tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazofumbatwa katika maisha ya watu asilia wa Canada. Hii ni hija ya toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho kwa kutambua na kukiri makosa yaliyotendwa na mihimili ya uinjilishaji kwa kushirikiana na wakoloni kwa nyakati zile za kihistoria. Anatambua changamoto za kiafya anazokabiliana nazo, lakini, ameamua kwenda nchini Canada, ili kutafuta ukweli na hatimaye, kukoleza mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, tayari kupandikiza mbegu ya matumaini kwa ajili ya kizazi za cha sasa na vile vijavyo, ili hatimaye, kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, anabeba ndani ya sakafu ya moyo wake amana na utajiri unaobubujika kutoka katika maisha yao na kwa hakika kwa sasa ni sehemu ya maisha yake. Dhamana na utume wa wanawake nchini Canada, usaidie kuwahamasisha watu wa Mungu kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kukoleza mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya, ili kutangaza na kushuhudia uzuri unaosimikwa katika maridhiano kati ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawahimiza watu asilia wa Canada kulinda, kudumisha na kuendeleza mambo matakatifu katika maisha yao. Wakuze Ibada kwa Mtakatifu Anna, Mzazi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu, aliyelinda Mtoto Yesu. Mtakatifu Kateri Tekakwitha, aliyejisadaka katika sala na kazi, aliyeshinda majaribu na kusimama imara katika imani, matumaini na mapendo, awe ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu nchini Canada katika kutekeleza ndoto ya Mungu katika maisha yao. Wanawake hawa waendelee kuwa ni ishara ya unabii katika maamuzi na utekelezaji wa maisha yao; wawe ni waombezi katika mchakato mzima wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa.

Watu Asilia Canada
29 July 2022, 17:17