Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 amekutana na kusali Masifu ya Jioni na: Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wahudumu wa shughuli za kichungaji nchini Canada. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 amekutana na kusali Masifu ya Jioni na: Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wahudumu wa shughuli za kichungaji nchini Canada. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Mihimili ya Uinjilishaji

Baba Mtakatifu amekazia: Malezi na majiundo ya Kipadre, kwa kuwakumbusha watu wa Mungu nchini Canada kwamba, Seminari ya kwanza nchini humo ilifunguliwa kunako mwaka 1663. Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu. Wachungaji wa Kanisa wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na msamaha; kwa kuguswa na madonda ya kila mwamini., ili kuyaponya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” ni sehemu ya utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Sura ya Pili ya Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani Mapadre wanapaswa kuunganika na Kristo Yesu ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili.

Seminari ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao! Kanisa linaangalia pia wito wa Kipadre unaoweza kuibuka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji na jinsi ya kuwasaidia vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Sura ya Tatu inagusia misingi ya malezi ya Kipadre. Hapa wahusika wakuu ni majandokasisi na kiini cha malezi haya ni utambulisho wa Padre mintarafu mafundisho ya kitaalimungu kwa kutambua kwamba, Padre ni Sadaka hai na takatifu inayompendeza Mungu na Sakramenti hii inapata chimbuko lake katika Ubatizo, lakini wanapakwa mafuta matakatifu, ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na Kusamehe dhambi za waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Padre anajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kanisa. Kumbe, safari ya majiundo ya Kikasisi imwezeshe Jandokasisi kufanana na Kristo Yesu kwa kuwa mtakatifu pasi na mawaa; mtu mwenye huruma na mapendo kwa ajili ya wokovu wa watu. Malezi ya maisha ya kiroho ni muhimu sana ili kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa.

Mihimili ya Uinjilishaji iwe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Mihimili ya Uinjilishaji iwe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Ni katika mkutadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 amekutana na kusali Masifu ya Jioni na: Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wahudumu wa shughuli za kichungaji nchini Canada, kwenye Kanisa kuu la Notre-Dame, Jimbo kuu la Quèbec “Notre-Dame de Québec.” Katika mahubiri yake amekazia kuhusu umuhimu wa majiundo na malezi ya Kipadre, furaha ya Kikristo, mitazamo hasi katika ulimwengu mamboleo; baadhi ya changamoto za kichungaji ni pamoja na: kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amekazia sana kuhusu umuhimu wa malezi na majiundo ya Kipadre, kwa kuwakumbusha watu wa Mungu nchini Canada kwamba, Seminari ya kwanza nchini humo ilifunguliwa kunako mwaka 1663. Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu kila mara wanapokutanika watu wa Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Wachungaji wa Kanisa wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na msamaha; kwa kuguswa na madonda ya kila mwamini, tayari kuyaganga na kuyaponya. Wachungaji waoneshe huruma na upendo wa dhati, kama ushuhuda wa ukaribu wao kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya furaha na imani kwa wachungaji wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ambaye kwanza kabisa amewaonesha huruma na upendo wake wa daima na anaendelea kuwasindikiza katika hija ya maisha na utume wao hapa duniani. Watambue kwamba, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wale wote wanaokutana na Kristo Yesu; wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, furaha inazaliwa na kuchipuka upya, chemchemi ya uinjilishaji mpya. Rej Evangelii gaudium, 1. Baba Mtakatifu anaitaka mihimili ya Uinjilishaji kuwa na mang’amuzi mapana yatakayowasaidia kuondokana na mtazamo hasi kuhusu dunia kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawabariki na kuwaongoza katika hija ya maisha na utume wao.

Papa Francisko amekazia malezi na majiundo ya Kipadre
Papa Francisko amekazia malezi na majiundo ya Kipadre

Ukanimungu ni hatari kwani watu wanapaswa kuongozwa na Amri za Mungu zinazotekelezwa kwa uhuru na utashi kamili. Kamwe wasijiruhusu kuwa ni walaji wa kupindukia, watu wenye uchu wa mali na madaraka. Dini ina umuhimu wa pekee sana katika maisha ya watu, kumbe kuna haja ya kuwa na mwelekeo chanya kuhusu ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, anaorodhesha baadhi ya changamoto katika shughuli za kichungaji, zinazopaswa kuwa ni sehemu ya sala na huduma ya kichungaji. Mihimili ya uinjilishaji haina budi kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, inawatangazia watu wa Mataifa ile furaha ya Injili, ili Kristo Yesu aweze kufahamika na watu, jambo ambalo kimsingi linahitaji kipaji cha ubunifu, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kukutana na kujadiliana na watu wa Mungu. Wainjilishaji wafahamu fika kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu vinavyopaswa kuzaa matunda katika ulimwengu mamboleo. Habari Njema ya Wokovu inatangwa, lakini zaidi inashuhudiwa kwa njia ya matendo adili na matakatifu. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni vitendo ambavyo vinahitaji kushughulikiwa kisheria ili haki iweze kutendeka, kwa sababu hivi ni vitendo vinavyodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Mama Kanisa ameomba msamaha kwa watu wote waliotendewa kinyume cha maadili na utu wema. Ubaguzi ni dhambi ambayo haipaswi kuendekezwa ndani ya Kanisa kama ulivyo pia ukoloni wa kiitikadi. Mihimili ya uinjilishaji itambue kwamba, inaitwa na kutumwa kuwahudumia watu wa Mungu, ili kujenga Kanisa lenye mwelekeo tofauti kabisa linalosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, upendo na huruma, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho na uinjilishaji mpya unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Huu ni uinjilishaji unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaopata chimbuko lake katika tunu msingi na kweli za Kiinjili, kwa kujenga na kuimarisha ushirika wa Kanisa; kwa kutoa fursa ya watu wa Mungu kukutana katika: Sala, Neno la Mungu na katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; kwa kujenga na kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi na zaidi sana, kuboresha mahusiano na mafungamano mema, mambo msingi kwa ajili ya ujenzi wa ushirika na huduma kwa watu wa Mungu. Kanisa liwe ni chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mungu katika ngazi mbalimbali za maisha, tamaduni, mila na desturi njema za watu, kwa kutambua kwamba, kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari ya Masifu ya Jioni na: Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wahudumu wa shughuli za kichungaji nchini Canada kwa kukazia umuhimu wa kumwilisha imani, matumaini na mapendo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama alivyokazia Mtakatifu François de Laval, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Quèbec katika maisha na utume wake.

Papa Francisko ameomba msamaha kwa dhambi zilizotendwa na watoto wa Kanisa
Papa Francisko ameomba msamaha kwa dhambi zilizotendwa na watoto wa Kanisa

Kwa upande wake, Askofu Raymond Poisson, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada "The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB)” lililoanzishwa kunako mwaka 1943 na kutambuliwa rasmi na Vatican mwaka 1948, amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na ushuhuda wake katika mchakato mzima wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Hii ni changamoto ya kutembea pamoja, ili kuishi kwa pamoja kama ndugu katika ardhi ya wote. Hija hii, imetia hamasa kwa Mihimili ya uinjilishaji kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika mchakato wa uinjilishaji na upatanisho wa Kitaifa, kwa kuwa na maono na mwelekeo mpya wa maisha ya watu wa Mungu nchini Canada. Huu ni wakati wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama alivyofanya Bikira Maria kwa binamu yake Elizabeth, kutokana na fadhila ya unyenyekevu, Mwenyezi Mungu amewatendea makuu na jina lake ni takatifu. Mara baada ya masifu haya ya jioni, akiwa njiani kurejea Uaskofuni, alipata bahati ya kusimama na kutembelea Kituo cha Mapokezi na Tasaufi cha Udugu wa Mtakatifu Alphonse “Fraternité St. Alphonse” kinachowahudumia watu 50 ambao wengi wao ni wazee, wagonjwa wa UKIMWI na waathirika wa dawa za kulevya. Baba Mtakatifu amekaa kwa muda kusikiliza historia ya maisha yao, na hatimaye, wote wakasali kwa pamoja. Hiki ni kituo kinachosimamiwa na kuongozwa na Padre Andrè Morency.

Wainjilishaji
29 July 2022, 15:34