Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Iqaluit, Jimbo Katoliki la Churchill, Canada, amekutana na kuzungumza na wazee na vijana; amezungumza pia kwa faragha na baadhi ya wanafunzi wa zamani. Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Iqaluit, Jimbo Katoliki la Churchill, Canada, amekutana na kuzungumza na wazee na vijana; amezungumza pia kwa faragha na baadhi ya wanafunzi wa zamani. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Hotuba Kwa Wazee Na Vijana wa Canada: Uponyaji

Papa Francisko asema: Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu zao na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uzee ni kipindi cha neema na baraka; wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii, mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni pamoja na: imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo hii kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano mapya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, ili kushirikishana amana na utajiri wa maisha, ili hatimaye waweze kuota ndoto ya pamoja, kwa kuvuka kinzani na mipasuko kati ya kizazi na kizazi, tayari kujiandaa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Bila ya mwelekeo huu mpya wa maisha, matamanio hayo halali yatakufa kwa baa la njaa kutokana na kuongezeka kwa upweke hasi; uchoyo na ubinafsi, nguvu za ubaguzi na utengano. Ubinafsi ni hatari katika maisha ya kijamii. Neno la Mungu linatoa mwaliko kwa waamini kushirikishana jinsi walivyo na kile walicho nacho; yaani vijana na wazee wanaweza kushikamana. Kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii. Vijana ni manabii wa siku za usoni, lakini wazee ni chimbuko la historia na kamwe hawawezi kuchoka kuendelea kuota ndoto na kurithisha uzoefu na mang’amuzi yao kwa vijana wa kizazi kipya, bila kuwa ni kizingiti kwa maisha yao ya sasa na yale ya mbeleni.

Umoja na mshikamano kati ya wazee na vijana ni muhimu sana.
Umoja na mshikamano kati ya wazee na vijana ni muhimu sana.

Lengo kuu la hija ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Canada, kuanzia Dominika tarehe 24 hadi Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 ni kusaidia kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, kwa kugusa madonda ya ukosefu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo ambayo walitendewa watu asilia wa Canada katika maisha na historia yao. Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Iqaluit, Jimbo Katoliki la Churchill, Canada, amekutana na kuzungumza kwanza kwa faragha na baadhi ya wanafunzi waliosoma kwenye shule za makazi ya watu asilia wa Canada. Katika hotuba yake, amewaomba tena msamaha kwa makosa na udhaifu ulioneshwa na wamisionari wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu zao na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya.

Ni wakati wa uponyaji na upatanisho wa kitaifa.
Ni wakati wa uponyaji na upatanisho wa kitaifa.

Baba Mtakatifu anasema, hija hii ya kitume imekuwa ni fursa kwake kuja kuomba msamaha kwa dhambi zilizotendwa na wamisionari katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho wa Injili. Amesikiliza kwa makini shuhuda mbalimbali zilizotolewa na wazee waliosoma kwenye shule za makazi ya watu asilia nchini Canada, kwa hakika ni mambo ya kusikitisha, kwani yalitengua mahusiano na mafungamano kati ya wazazi na watoto wao. Sasa ni wakati wa kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, ili kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Vijana wa kizazi kipya wajifunze kutoka kwa wazee wao jinsi ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kuwahudumia jirani zao pamoja na kutunza historia ya watu wao katika ujumla wake. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza wazee wao na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kama “Mzee” anapenda kuwashauri mambo makuu matatu. Vijana wahakikishe kwamba, wanatembea kifua mbele, kwa kuzingatia kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu. Wajenge moyo wa huduma kwa Mungu na jirani, kwa kuendelea kujikita katika ukweli na haki; wapandikize mbegu ya amani na hivyo kujenga mahusiano na mafungamano thabiti ya kijamii.

Wananchi wa Canada wasikate wala kukatishwa tamaa na wapinga maendeleo
Wananchi wa Canada wasikate wala kukatishwa tamaa na wapinga maendeleo

Kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa na wapinga maendeleo yao, bali wao waendelee kutembea kifua mbele, kwa kuuendea mwanga wa maisha. Wajitahidi kuishi vyema kwa kutembea katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo thabiti. Watambue kwamba, Kristo Yesu ni mwanga wa ulimwengu na wao wajitahidi kuwa mwanga angavu kwa ushuhuda wa maisha na vipaumbele vyao, kwa kuondoa giza la dhambi katika sakafu ya nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuwa ni watu huru na wenye furaha ya kweli. Vijana katika maisha na utume wao, wajitahidi kushirikiana na kuunda timu na wala wasipende kufanya shughuli za kipweke pweke, bali washirikiane na wengine kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Yote haya wayatekeleze kadiri ya tamaduni, lugha, huku wakiendelea kuwasikiliza na kuwathamini wazee wao. Kwa kuthamini amana na utajiri unaobubujika kutoka katika tamaduni, mila na desturi njema sanjari na uhuru wa mtu binafsi, vijana wanaweza kukumbatia Injili ya Kristo Yesu, ambayo wamerithishwa kutoka kwa wahenga na hivyo kwa sasa wanaweza kukutana na Uso wa upendo na huruma wa Kristo Yesu.

Vijana na wazee

 

30 July 2022, 10:03