Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Haki Msingi za Binadamu

Baba Mtakatifu amegusia mifumo mbalimbali ya ukoloni na madhara yake. Amewahimiza Wacanada kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii. Changamoto zinazomwandama mwanadamu ni pamoja na: Ukosefu wa amani, athari za mabadiliko ya tabianchi na Ugonjwa wa UVIKO-19; Mchango wa watu asilia wa Canada katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, tayari kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya wa matumaini, kama ndugu wamoja! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini Canada. Hotuba ya Baba Mtakatifu ilijikita zaidi katika nembo zinazopatikana kwenye bendera ya Canada. Baba Mtakatifu amekazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; athari za ukoloni na umuhimu wa uinjilishaji unaosimikwa katika utamadunisho, unaozingatia na kuheshimu haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amegusia mifumo mbalimbali ya ukoloni, lakini hasa ukoloni wa kiitikadi na madhara yake katika maisha ya watu. Amewahimiza watu wa Mungu nchini Canada kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake. Changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni pamoja na: Ukosefu wa amani, athari za mabadiliko ya tabianchi na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Mchango wa watu asilia wa Canada katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau athari za ongezeko la idadi ya maskini na wahitaji zaidi.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe na wote
Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe na wote

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni ufunuo wa upendo wa Mungu kwa viumbe vyake vyote, changamoto na mwaliko kwa binadamu kumsikiliza Mwenyezi Mungu kwa umakini zaidi; na binadamu kujenga utamaduni wa kusikilizana wao kwa wao pamoja na kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha Dunia Mama. Mabadiliko ni jambo zuri, lakini wakati mwingine huwa ni chanzo cha wasiwasi pale yanaposababisha madhara ulimwenguni na hivyo kuathiri ubora wa maisha ya watu wengi. Rej Laudato si, 18. Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na tabia ya uchoyo, ubinafsi na maamuzi mbele. Watu wajenge mahusiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ukoloni mkongwe na mfumo wa elimu ya makazi kwa watu asilia wa Canada ni mambo yaliyopelekea kusigina: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Mihimili wa Uinjilishaji, kwa wakati huo ikamezwa na malimwengu, kiasi cha “kutia mchanga” tunu msingi za Kiinjili na mchakato mzima wa utamadunisho. Mambo yote haya yakatengeneza madonda makubwa ya mahusiano na mafungamano miongoni mwa wananchi wa Canada.

Baba Mtakatifu kwa niaba ya Kanisa ameomba tena msamaha kwa mapungufu ya kibinadamu yaliyodhalilisha: tamaduni, mila na desturi njema za watu asilia wa Canada. Ni wakati wa kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, ili kulinda na kudumisha haki msingi za watu asilia wa Canada. Yote haya hayana budi kukita mizizi yake katika mchakato mzima wa: toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho, sanjari na kutambua haki msingi za watu asilia wa Canada. Mama Kanisa anapenda kujizatiti zaidi na zaidi katika utekelezaji wa haki msingi za watu asilia wa Canada kama zinavyofafanuliwa na Tamko La Haki Msingi za Watu Asilia wa Canada kama lilivyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu: utamaduni, lugha na mchakato wa elimu bora zaidi. Kanisa litaendelea kuboresha mahusiano na mafungamano yake na watu asilia ya wa Canada, ili kutembea pamoja katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, katika ukweli na haki; kwa kuponya na kuendelea kujizatiti katika upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika matumaini. Mifumo mbalimbali ya ukoloni hadi wakati huu ambapo ukoloni wa kiitikadi unaendelea kushamiri, Mama Kanisa anasema kwamba, huu ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa ni safari ndefu na kwamba, madhara ya ukoloni hayawezi kufutika mara moja kama “ndoto ya mchana.” Huu ni mwaliko wa kutibu “Saratani ya Utamaduni” kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Utuanzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili
Utuanzaji bora wa mazingira ni wajibu wa kimaadili

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu nchini Canada kusimama kidete kulinda, kutangaza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaosimikwa katika Sera za utoaji mimba, kifo laini pamoja na kutetea haki za wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji. Watambue umuhimu wa familia, ili hatimaye kutangaza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Leo hii, familia nyingi zinakabiliana na changamoto, matatizo na fursa ambazo zikitumika barabara zinaweza kuwa ni chachu ya ustawi na maendeleo ya familia. Lakini: vipigo vya majumbani, changamoto za fursa ya ajira, uchoyo na ubinafsi; kazi za kuvunja watu moyo; ukosefu wa fursa za ajira, upweke hasi; vijana wengi kuelemewa na hatimaye, kumezwa na malimwengu; kutelekezwa kwa wazee na wagonjwa, kuwa ni kati ya changamoto pevu. Huu ni wakati wa kujifunza kanuni maadili na utu wema kutoka kwa watu asilia wa Canada kwa kuheshimu: tunu msingi za maisha ya kifamilia; kwa kulinda na kudumisha misingi ya familia bora; kwa kukosoana na kurekebishana kiutu; kwa kufarijiana na hatimaye, kuanzisha mchakato wa upatanisho pale ambapo misigano ya kijamii imejitokeza. Kamwe, haki na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zisibezwe kwa kisingizio cha uchumi unaojikita katika uzalishaji na mafao binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, kwa kuondokana na misimamo mikali, maamuzi mbele, chuki na uhasama kati ya watu wa Mungu. Amani ya kweli inasimikwa katika upendo kwa jirani. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Hili ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshikirisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha duniani; utengenezaji, usambazaji na ulimbikizaji wa silaha duniani ni hatari kwa amani duniani. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya amani duniani, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika medani mbalimbali za Kimataifa. Changamoto hizi ni pamoja na ukosefu wa amani sehemu mbalimbali za dunia; athari za mabadiliko ya tabianchi; madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na zaidi sana wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji Kimataifa. Hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kwa njia ya majadiliano sanjari na kuwahusisha wadau. Jimbo la Quebec nchini Canada linaendelea kujinadi kwa sera na mikakati makini ya Kiikolojia.

Umoja na mshikamano wa Kimataifa ni muhimu kukabiliana na changamoto
Umoja na mshikamano wa Kimataifa ni muhimu kukabiliana na changamoto

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwingiliano wa watu, tamaduni, mila na desturi ni fursa ya kushirikishana kile kilicho bora zaidi. Katika mchakato huu, hata maskini na tamaduni, matamanio na uwezo wao wa kufikiri na kutenda, wanapaswa kushirikishwa na kamwe wasidharauliwe. Haya ni mafungamano ya watu wa Kimataifa ambayo ni fursa ya kuendeleza tofauti za nafsi; na kwamba, hawa ni jumla ya watu ndani ya jamii inayotafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, kila mmoja anapaswa kunufaika na mafungamano haya. Mchakato wa utamadunisho ni endelevu na fungamani kwani ni kielelezo cha ukarimu na upendo kama inavyojionesha kwa Canada kuwapokea na kuwakaribisha wakimbizi na wahamiaji kutoka Ukraine na Afghanstan. Ni mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu na wajibu wake kwa umma. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa hotuba yake viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini Canada amegusia kuhusu ongezeko la maskini wanaohitaji msaada wa hali na mali katika jamii. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali za dunia zinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Inasikitisha kuona kwamba, watu asilia wa Canada wengi wao wanaendelea kupekenywa na umaskini, ujinga na mardhi. Hili ni kundi la watu ambao wana makazi duni sana nchini Canada. Kumbe, watu asilia wa Canada wanayo haki ya kupata huduma msingi, ili kuboresha maisha yao, kwa kushirikishwa katika hatua mbalimbali za maamuzi kiuchumi na kijamii, kwa kutambua kwamba, ushirikishwaji wa watu wa Mungu ni sehemu muhimu sana ya ujenzi wa mafungamano ya kijamii.

Papa Viongozi
28 July 2022, 16:36