Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Mchakato wa Ukomavu Na Ushuhuda wa Imani

Papa Francisko anawataka waamini kuwa imara na thabiti kutangaza na kushuhudia imani yao, hasa nyakati za majaribu na pale maisha yanapoonekana kuwa kama ubatili. Wasikubali kuyumbishwa, kuteleza na hatimaye kubwagwa chini “kama gunia la nazi” bali wasimame kidete kupambana na maouvu kwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, Bwana wa uzima. Ushuhuda wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mwaka ifikapo tarehe 29 mwezi Juni, Kanisa huadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba wa Imani.  Mtume Petro aliikiri Imani kwa Kristo Yesu akisema “Wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai” (Mathayo 16:16). Hii ni kiri ya imani iliyotamkwa na Mtakatifu Petro, si kwa sababu ya ufahamu wake wa kibinadamu bali kwa sababu alikuwa amefunuliwa siri hii kubwa na Mwenyezi Mungu aliye mbinguni. Simoni Petro mvuvi wa Bethsaida akaanza hija ya kumwilisha kiri hii ya imani, iliyomchukua kitambo kirefu hadi kuweza kuikamilisha katika maisha yake, kama ilivyokua hata kwa Paulo, Mtume. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba ya Imani kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 29 Juni 2022. Na Mtume Paulo aliwatangazia na kuwashuhudia watu wa Mataifa imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Petro na Paulo ni mfano wa umoja na utofauti katika Kanisa katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na Mashuhuda wa Imani
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na Mashuhuda wa Imani

Hii ndiyo changamoto na mwaliko kwa wale wanaomwamini Kristo Yesu kuwa ni Masiha na Mwana wa Mungu aliye hai. Ili kuishi na kutenda mintarafu Injili ya Kristo Yesu, kunahitaji uvumilivu na unyenyekevu mkuu. Mtakatifu Petro Mtume, alipata mang’amuzi ya safari hii ya imani mara moja hata bila kuchelewa. Ni wakati ambapo Kristo Yesu alipowatangazia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, Petro Mtume, akamwambia kwamba haya ni mambo ambayo ni kinyume kabisa cha Masiha wanayemtarajia. “Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mt 16:23. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa imara na thabiti kutangaza na kushuhudia imani yao, hasa nyakati za majaribu na pale maisha yanapoonekana kuwa kama ubatili. Wasikubali kuyumbishwa, kuteleza na hatimaye kubwagwa chini “kama gunia la nazi” bali wasimame kidete kupambana na maouvu kwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, Bwana wa uzima. Kamwe waamini wasitafute njia za mkato katika imani, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, imani inapaswa kukua na hatimaye, kukomaa, ili kuweza kutolewa ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mtakatifu Petro alishuhudia ukomavu wa imani, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa kwa kutundikwa miguu juu na kichwa chini, kifo cha kusikitisha sana.

Ushuhuda wa imani kadiri ya wito, dhamana na utume wa kila mwamini ndani ya Kanisa
Ushuhuda wa imani kadiri ya wito, dhamana na utume wa kila mwamini ndani ya Kanisa

Imani ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa ilipitia changamoto nyingi hadi kufikia ukomavu wake. Paulo wa Tarso aliyelidhulumu Kanisa, alikutana mubashara na Yesu Kristo Mfufuka akiwa njiani kwenda Dameski, akajiachilia mikononi mwa Mungu, na neema na hatimaye akawa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Hapa kila mwamini anaweza kujipatia mfano wake katika maisha. Alipambana kufa na kupona na maisha na utume wake alitambua “mwiba uliokuwa mwilini mwake.” 2 Kor 12: 17. Hija ya maisha ya imani ni pevu, ngumu na inayomwajibisha mwamini. Mtakatifu Paulo Mtume, amekuwa Mkristo kwa taratibu, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujifunza kutoka kwake, hata wakati mwingine, kwa kupitia majaribu. Ushuhuda wa watakatifu Petro na Paulo, Mitume iwe ni nafasi kwa waamini kutafakari na kujiuliza kuhusu ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wawe tayari kuendelea kujifunza kwa kina kuhusu kiri ya imani. Mwishoni mwa Tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kamwe Wakristo wasiwe ni watu wa kukata wala kujikatia tamaa na kulalama. Changamoto za imani ziwe ni fursa ya kukua na kukomaa. Mtakatifu Paulo Mtume, anasema “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kuhifadhi hata nifike kwenye Ufalme wake wa mbinguni.” 2 Tim 4:18. Bikira Maria Malkia wa Mitume, awasaidie waamini kujifunza kutoka kwa Mitume wa Yesu, ili kuenenda na hatimaye, kukomaa katika njia ya imani.

Angelus
29 June 2022, 15:22

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >