Tafuta

1635934718849.JPG

Papa Fransisko:Kanisa linajikita kwa moyo wote katika huduma ya wanandoa!

Tunachapisha utangulizi wa Papa Francisko katika Hati ya “Taratibu za Ukatekumeni kwa ajili ya Maisha ya Ndoa”,kama sehemu ya Mwongozo wa Kichungaji kwa Makanisa mahalia:Ni katika Hati iliyotayarishwa na Baraza la Kipapa la Walei Familia na Maisha mwishoni mwa Mwaka uliowekwa wakfu kwa familia”.

 “Tangazo la Kikristo kuhusu familia ni habari njema kweli” (Amoris laetitia, 1). Uthibitisho huu wa mwisho wa uhusiano wa Sinodi ya Maaskofu juu ya familia ulistahili kufungua Wosia wa Kitume Amoris laetitia. Kwa sababu Kanisa katika kila zama, linaitwa kutangaza upya, hasa kwa vijana, uzuri na wingi wa neema zilizomo katika Sakramenti ya ndoa na maisha ya familia yanayobubujika kutoka humo. Miaka mitano baada ya kuchapishwa, Mwaka “Famiglia Amoris Laetitia" ulikusudia kuirejesha familia katika kitovu ili kuwaalika watu kutafakari mada za Wosia wa Kitume na kuhuisha Kanisa zima katika dhamana ya furaha ya uinjilishaji kwa ajili ya familia na familia. Moja ya matunda ya mwaka huu wa pekee ni “Taratibu za mafundisho ya  Kikatekumeni kwa ajili ya maisha ya ndoa”, ambayo sasa ninayo furaha kuwakabidhi wachungaji, wenzi wa ndoa na wale wote wanaofanya kazi ya uchungaji ya familia.

Hiki ni chombo cha kichungaji kilichotayarishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kufuatia kielelezo ambacho nimekuwa nikieleza mara kwa mara, yaani “uhitaji wa” ukatekumeni mpya “katika maandalizi ya ndoa”; kwa hakika, ni ya haraka kutekeleza kwa uthabiti yale ambayo tayari yamependekezwa katika Familiaris consortio (n. 66), yaani, kwamba, kuhusu Ubatizo wa watu wazima wakatekumeni ni sehemu ya mchakato wa sakramenti, hivyo pia maandalizi ya ndoa yanakuwa sehemu muhimu ya utaratibu mzima wa sakramenti ya ndoa, kama dawa inayozuia kuzidisha michakato ya  ndoa batili au zisizolingana "(Hotuba kwa Rota Romana, 21 Januari 2017). Wasiwasi mkubwa ulijitokeza hapa bila shaka juu ya ukweli kwamba, katika maandalizi ya juu juu sana, wanandoa wanakabiliwa na hatari halisi ya kusherehekea ndoa batili au moja yenye misingi dhaifu kama "kuanguka" kwa muda mfupi na kushindwa kupinga hata migogoro ya kwanza isiyoweza kuepukika.

Kushindwa huku huleta mateso makubwa na kuacha majeraha makubwa kwa watu. Wanabaki wakiwa wamekata tamaa, wakiwa na uchungu na, katika hali zenye uchungu zaidi, hata wanaishia kutoamini tena wito wa upendo, ulioandikwa na Mungu mwenyewe katika moyo wa mwanadamu. Kwa hiyo, kwanza kabisa kuna wajibu wa kuwasindikiza wale wanaodhihirisha nia yao ya kuungana katika ndoa kwa hisia ya uwajibikaji, ili waepukwe na majeraha ya kutengana na kamwe wasipoteze imani katika upendo. Lakini pia kuna hisia ya haki ambayo inapaswa kutuhuisha. Kanisa ni mama, na mama hafanyi upendeleo miongoni mwa watoto wake. Yeye hawatendei bila usawa, anajitolea kwa huduma sawa, tahadhari sawa, wakati huo huo kwa kila mtu. Kutoa muda ni ishara ya upendo: ikiwa hatutoi muda  kwa mtu ni ishara kwamba hatumpendi. Hili linanijia akilini mara nyingi ninapofikiri kwamba Kanisa linatumia muda mwingi, miaka fulani, likiwatayarisha watahiniwa kwa ajili ya ukuhani au maisha ya kitawa lakini linatumia muda mfupi, majuma machache tu, kwa wale wanaojiandaa kwa ndoa. Kama mapadre na watu waliowekwa wakfu, wenzi wa ndoa pia ni watoto wa Kanisa mama, na tofauti kubwa namna hii katika kutendewa si sawa. Wanandoa walio katika ndoa ndio wengi zaidi wa waamini, na mara nyingi ni nguzo katika parokia, vikundi vya kujitolea, vyama na harakati.

Wao ni walezi wa maisha halisi, sio tu kwa sababu wanazaa watoto, wanawasomesha na kusindikizana  nao katika ukuaji wao, lakini pia kwa sababu wanatunza wazee katika familia, wanajitolea kwa huduma ya watu wenye ulemavu na mara nyingi, hali nyingi za umaskini wanazokutana nazo. Miito ya ukuhani na maisha ya kuwekwa wakfu huzaliwa kutoka kwa familia; na ni familia zinazofanya jamii na kurekebisha machozi kwa subira na kujitoa sadaka kila siku. Kwa hiyo ni wajibu na  haki kwa Mama Kanisa kutenga muda na nguvu kwa ajili ya maandalizi ya wale ambao Bwana anawaita kwa ajili ya utume mkubwa sawa na ule wa familia. Kwa maana hiyo, ili kutoa uthabiti wa hitaji hili la dharura, “Nilipendekeza kutekeleza ukatekumene wa kweli kwa wenzi wa ndoa wa baadaye, ambao unajumuisha hatua zote za safari ya sakramenti, wakati wa kujiandaa kwa ndoa, sherehe yake na miaka inayofuata”, (hotuba kwa washiriki katika kozi ya mchakato wa ndoa, 25 Februari 2017).

Hivi ndivyo Waraka ninaowasilisha hapa unapendekeza kufanya na ninashukuru. Umegawanywa katika vingele vitatu: maandalizi ya ndoa (ya mbali, ya karibu na ya haraka); sherehe ya harusi; Kusindikiza na miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa. Kama mtakavioona, ni suala la mchakato ambao ni sehemu muhimu ya njia ya  pamoja na wanandoa kwenye safari ya maisha yao, hata baada ya harusi, hasa wakati wataweza kupitia shida na nyakati za kukata tamaa. Kwa  maana hiyo tutajaribu kuwa waaminifu kwa Kanisa, ambalo ni mama, mwalimu na  msindikizaji daima wa safari kando yetu. Ni matamanio yangu ya dhati kwamba Hati hii ya kwanza ifuatwe haraka iwezekanavyo na nyingine, ambamo mbinu madhubuti za kichungaji na safari zinazoweza kusindikiza zimeoneshwa mahsusi kwa wale wanandoa ambao wamepitia kuvunjika kwa ndoa yao na ambao wanaishi katika muungano mpya au wanaolewa tena kistaarabu. Kanisa, kwa hakika, linataka kuwa karibu na wanandoa hawa na pia kutembea nao kupitia upendo (taz. Amoris laetitia, 306), ili wasijisikie wameachwa na kupata katika jumuiya mahali pa kufikiwa na kidugu pa kukaribishwa, kusaidia katika utambuzi na ushiriki. Hati hii ya kwanza ambayo sasa inatolewa ni zawadi na

Zawadi, kwa sababu inatoa nyenzo nyingi na za kusisimua kwa wote, matokeo ya tafakari na uzoefu wa kichungaji ambao tayari umetekelezwa katika majimbo/maparokia mbalimbali za ulimwenguni.  Na pia ni kazi, kwa sababu sio suala la  kanuni za kiini macho zinazofanya kazi moja kwa moja (automatiki). Ni vazi ambalo lazima litengenezwe kwa kipimo cha watu watakaolivaa. Kwa hakika, ni suala la mielekeo inayoomba kupokelewa, kurekebishwa na kuwekwa katika vitendo katika hali halisi za kijamii, kiutamaduni na kikanisa ambapo kila Kanisa hujikuta likiishi. Kwa hiyo ninatoa wito kwa unyenyekevu, bidii na ubunifu wa wachungaji wa Kanisa na washiriki wao, kufanya kazi hii muhimu na ya lazima ya malezi, kutangaza na kusindikiza na familia, ambayo Roho Mtakatifu anatutaka tuifanye, kwa ufanisi zaidi kwa sasa.

“Sikurudi kamwe nyuma kwa jambo ambalo lingeweza kuwafaa kuwahubiria na kuwafundisha” (Matendo 20:20). Ninawaalika wale wote wanaofanya kazi ya uchungaji wa familia kuyafanya maneno haya ya Mtume Paulo kuwa yao wenyewe na wasivunjike moyo mbele ya kazi ambayo inaweza kuonekana kuwa ngumu, yenye kudai au hata kupita uwezo wao. Kazana! Wacha tujikite kuanza kuchukua hatua za kwanza! Hebu tuanze taratibu za upyaishaji wa kichungaji! Hebu tuweke akili na mioyo yetu katika huduma ya familia zijazo, na ninawahakikishia kwamba Bwana atatutegemeza, atatupa hekima na nguvu, atatufanya sote tuwe na shauku na zaidi ya yote atatufanya tupate utamu na faraja, (Evangelii gaudium, 9), wakati tunapotangaza Injili ya familia kwa vizazi vipya.

UTANGULIZI WA PAPA KATIKA HATI KUHUSU UKATEKUMENI WA NDOA
15 June 2022, 16:46