Tafuta

Papa Francisko: Ujumbe wa utume wa umisionari wa familia ulimwenguni Papa Francisko: Ujumbe wa utume wa umisionari wa familia ulimwenguni 

Papa: Ujumbe wa Utume wa Umisionari wa Familia Duniani

Ujumbe wa utume wa umisionari wa familia ni mwaliko kwa wanandoa na familia kusikiliza sauti ya Mungu anayewaita, ili wawe wamisionari duniani. Hii ni dhamana inayowataka watu wa Mungu kushikamana na kuambatana. Wanandoa vijana, watazame na kuiga mfano bora wa wale waliowatangulia na wale waliotangulia, wajitahidi kuwa ni wandani wa safari kwa wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na kuhitimishwa rasmi wakati maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Juni, 2022. Ni maadhimisho ambayo yamenogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.”. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” umekuwa ni wakati muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia.” Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 25 Juni 2022 amehitimisha rasmi Maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Juni 2022 amewagawia waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa uwanjani hapo ujumbe wa utume wa umisionari wa familia. Baba Mtakatifu anawaalika wanandoa na familia kusikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu anayewaita, ili wawe wamisionari duniani.

Wanandoa wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia ulimwenguni kote
Wanandoa wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia ulimwenguni kote

Hii ni dhamana inayowataka watu wa Mungu kushikamana na kuambatana katika ushirika. Wanandoa vijana, watazame na kuiga mfano bora wa wale waliowatangulia na wale waliotangulia, wajitahidi kuwa ni wandani wa safari kwa wengine. Kwa wanandoa waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na changamoto na matatizo mbalimbali yanayowasibu katika maisha, Baba Mtakatifu anawaalika kuvunjilia mbali huzuni kwa kujiaminisha katika upendo wa Mungu uliomiminwa rohoni mwao, daima wajitahidi kumwomba Roho Mtakatifu ili aendelee kuupyaisha upendo huo. Wanandoa wanahimizwa kutangaza na kushuhudia furaha ya uzuri wa maisha ya ndoa na familia. Wawatangazie watoto na vijana neema ya ndoa ya Kikristo. Wawagawie matumaini, wale waliokata tamaa na watende kana kwamba, yote yanawategemea wao, kwa kutambua kwamba, wamepewa dhamana hii na Mwenyezi Mungu.

Ni wakati wa kushuhudia mshikamano na huduma ya upendo
Ni wakati wa kushuhudia mshikamano na huduma ya upendo

Wanandoa watambue kwamba, wanayo dhamana ya “kushona” muundo wa jamii na wa Kanisa la Kisinodi, unaojenga mahusiano, kwa kuzidisha upendo na kuthamini maisha. Wawe ni ishara ya Kristo aliye hai na kamwe wasiogope kupokea maombi kutoka kwa Kristo Yesu na kwamba wajitahidi kuwa wakarimu mbele yake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanandoa kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao, wamsikilize katika hali ya ukimya wa sala. Wawasindikize wadhaifu, wawe ni faraja kwa walio pweke, wakimbizi na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Wanandoa wawe ni mbegu ya ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Kimsingi, wajitahidi kuwa ni familia yenye moyo mkuu! Washuhudie ile sura ya ukarimu wa Kanisa na wadumu katika sala daima. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa anawasaidie wanandoa pale wanapotindikiwa divai; awasindikize nyakati za kimya kikuu na majaribu ya maisha; awasaidie kutembea kwa mshikamano na Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu Mfufuka.

Utume wa umisionari wa familia
26 June 2022, 15:38