Papa: Mauaji ya Sr. Luisa Dell'Orto: Ushuhuda wa Huduma ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 25 Juni 2022 ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na mauaji ya kinyama dhidi ya Sr. Luisa Dell’Orto wa Shirika la Dada Wadogo wa Injili wa Charles de Foucauld, aliyeuwawa Jumamosi tarehe 24 Juni 2022 huko mjini Port-au-Prince alikokuwa anatekeleza utume wake kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Mauaji haya yametokea katika purukushani la jaribio la majambazi kupora mali za watu mjini humo.
Baba Mtakatifu amemwombea Marehemu Sr. Luisa Dell’Orto wa Shirika la Dada Wadogo wa Injili wa Charles de Foucauld, ili Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuipokea roho yake huko mbinguni na hatimaye, kumstahilisha maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaombea watu wa Mungu nchini Haiti, wanaokabiliana na changamoto za hali ngumu ya maisha, waweze kupata amani na utulivu; ili hatimaye, waweze kupambana na umaskini pamoja na vitendo vya uvunjifu wa amani. Sr. Luisa Dell’Orto wa Shirika la Dada Wadogo wa Injili wa Charles de Foucauld, ametimiza wajibu wake barabara, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kama ushuhuda wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limetuma salam za rambirambi kwa Shirika la Dada Wadogo wa Injili wa Charles de Foucauld, ndugu jamaa pamoja na wamisionari wote wanaotekeleza dhamana na utume wao sehemu mbalimbali za dunia ambako kuna vita, mipasuko na misigano ya kijamii. Kifo cha Sr. Luisa Dell’Orto kiwe ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani nchini Haiti. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linasema kwamba, litaendelea kushirikiana na kushikamana bega kwa bega na watu wa Mungu nchini Haiti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifo cha Sr. Luisa Dell’Orto wa Shirika la Dada Wadogo wa Injili wa Charles de Foucauld anasema, Kardinali Matteo Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI ni mbegu ya haki, amani na upatanisho itakayozaa matunda kwa wakati wake.