Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Pasaka: Urbi Et Orbi 2022

Ujumbe wake wa Pasaka: “Urbi et Orbi” kwa mwaka 2022 Papa amegusia amani kwa watu ambao wanaendelea na Kwaresima kutokana na vita na UVIKO-19. Kristo Yesu ndiye mwenye haki ya kutangaza na kushuhudia amani duniani, mwaliko wa kutoa nafasi kwa amani, haki na upatanisho na kuendelea kupambana na majanga asilia kwani amani ni dhamana na wajibu wa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, tarehe 17 Aprili 1949, alitoa Ujumbe wa Pasaka kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake maarufu kama “Urbi et Orbi” kwa njia ya Televisheni ya Ufaransa, akiwatakia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema heri na baraka za Sherehe ya Pasaka. Katika ujumbe huo, alikazia umuhimu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na waamini katika ujumla wao, kukutana katika uwanja wa mawasiliano na kwa wakati huo, Televisheni. Katika muktadha huu, njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii imekuwa ni msaada mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ni imani iliyotangazwa na kushuhudiwa kwanza kabisa na wanawake jasiri wa imani, Mitume wa Yesu na hatimaye waamini wa Kanisa la Mwanzo. Hii ni imani ambayo imethibitishwa kwa njia ya Agano Jipya, wakaitangaza na kuihubiri kwa ari na moyo mkuu kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka pamoja na Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu amefufuka kutoka wafu. Kwa kifo chake alishinda mauti. Wafu amewapa uzima. Rej KKK 638. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu.

Papa Francisko ameongoza Ibada ya Misa ya Pasaka na kutoa salam na baraka za Pasaka
Papa Francisko ameongoza Ibada ya Misa ya Pasaka na kutoa salam na baraka za Pasaka

Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika ya Pasaka tarehe 17 Aprili 2022, ameadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye ametoa ujumbe wa Pasaka: “Urbi et Orbi” kwa ajili ya mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake, tukio ambalo limefuatiliwa na maelfu ya waamini na watu wenye mapenzi mema kwa ushiriki mkamilifu, kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake wa Pasaka: “Urbi et Orbi” kwa mwaka 2022 amegusia amani kwa watu ambao wanaendelea na Kwaresima kutokana na vita na UVIKO-19. Kwa madonda yake Matakatifu Kristo Yesu ndiye mwenye haki ya kutangaza na kushuhudia amani duniani. Anawaalika watu wa Mungu ili kutoa nafasi kwa amani, haki na upatanisho pamoja na kuendelea kupambana na majanga asilia na kwamba, amani ni dhamana na wajibu wa watu wote.

Baba Mtakatifu anasema Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, Amefufuka na anapenda kuwakirimia waja wake zawadi ya amani, wale wote wanaolia na kuomboleza; walioshikwa na hofu na hali ya kukata tamaa, hata leo hii, anasema tena “Amani kwenu.” Hii ni zawadi ambayo Kristo Yesu aliwakirimia Wanafunzi wake waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Leo bado wana hofu na mashaka kutokana na vita inayoendelea kupamba moto kati ya Ukraine na Urussi, hali inayowapatia waamini ugumu wa kuamini ikiwa kama kweli Kristo Yesu amefufuka kwa wafu! Huu ni ukweli unaotangazwa na kushuhudiwa kwamba, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka kweli kweli, wakati huu, ambapo Kwaresima inaonekana kuendelea kushamiri kutokana na vita pamoja na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Bado kuna watu wanaoendelea kumwaga damu ya ndugu zao waliowageuza na kuwa maadui kama ilivyokuwa kwenye Maandiko Matakatifu. Walimwengu wanamhitaji Kristo Yesu Mfufuka, ili aweze kuwakirimia ushindi unaosimikwa katika upendo na kuendelea kutumaini katika mchakato wa upatanisho! Kwa hakika watu wa Mungu wanataka kusikia tena “Amani kwenu.”

Amani ni zawadi ya Mungu inayowawajibisha watu wote kadiri ya dhamana na wajibu wao.
Amani ni zawadi ya Mungu inayowawajibisha watu wote kadiri ya dhamana na wajibu wao.

Hii ni zawadi inayoweza kutolewa na Kristo Mfufuka peke yake kwa kutangaza na kushuhudia amani duniani, kwa sababu ya Madonda yake matakatifu yaliyosababishwa na dhambi za binadamu, ugumu wa mioyo, chuki na kisasi. Madonda Matakatifu ni alama ya upendo na huruma ya Kristo isiyokuwa na kifani. Ni kielelezo cha mapambano na ushindi kwa niaba ya binadamu mdhambi, ushindi ambao umetundikwa juu ya silaha ya upendo, ili mwanadamu aweze kupata na hatimaye, kuishi katika amani ya Kristo Mfufuka. Madonda yake Matakatifu yawasaidie waamini wenye mioyo migumu kutangaza na kushuhudia amani duniani, ili kweli amani ya Kristo Mfufuka iweze kupenya na kukita mizizi yake katika maisha ya watu wa Mungu, majumbani mwao na katika nchi zote. Baba Mtakatifu Francisko anaombea amani nchini Ukraine, ambako kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita kati yake na Urussi. Kamwe watu wa Mataifa wasijenge mazoea ya vita, bali wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani duniani. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu duniani na wanasayansi wasitishe mchakato wa kutengeneza silaha. Vita inaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Makazi ya watu yameharibiwa na sasa nchi imebaki kuwa ni magofu. Watoto yatima wanaendelea kuongezeka na hivyo kuongeza idadi ya Watoto wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; Watoto ambao wanafariki dunia kwa kukosa tiba muafaka; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa kijinsia, mauaji na wale wanaotolewa mimba na hivyo kunyimwa haki ya kuzaliwa.

Vita ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao
Vita ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao

Hata katika maafa makubwa ya vita, bado kuna Jumuiya za Watu wa Ulaya ambazo zimejizatiti kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, matukio ambayo yanageuka na kuwa ni kielelezo cha baraka dhidi ya uchoyo na ubinafsi na hivyo ukarimu kutamalaki katika nyoyo za watu. Licha ya vita kati ya Urussi na Ukraine, bado mtutu wa bunduki unaendelea kurindima huko Mashariki ya Kati ambako mji wa Yerusalemu unapaswa kuwa ni kielelezo cha amani kati ya Wakristo, Wayahudi na Waislam. Hapa ni mahali ambapo wananchi wake wanapaswa kuishi kwa amani, udugu wa kibinadamu na hatimaye, kuishi katika uhuru wa kidini, kwa kuheshimu na kuthamini dini za watu wengine. Bado amani na upatanisho vinahitajika nchini Lebanon, Syria na Iraq, lakini zaidi ni kwa waamini wa dini ya Kikristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Amani na upatanisho vinahitajika nchini Libia, Yemen, Mynamar na Afghanstan; nchi ambazo kuna mateso na mahangaiko makubwa ya wananchi. Baba Mtakatifu Francisko ameombea amani Barani Afrika, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako vitendo vya kigaidi vimeshika hatamu, kiasi cha kuvuruga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Upatanisho unahitajika nchini Ethiopia; majadiliano katika ukweli, haki na upatanisho yapate nafasi nchini DRC; sala na mshikamano wa kidugu uwaendee wananchi wa Afrika ya Kusini ambao hivi karibuni wamekumbwa na mafuriko makubwa ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Mafuriko makubwa Afrika ya Kusini yamesababisha maafa kwa watu na mali zao.
Mafuriko makubwa Afrika ya Kusini yamesababisha maafa kwa watu na mali zao.

Kristo Yesu mfufuka aandamane na kuwasaidia watu wa Amerika ya Kusini, ambao katika baadhi ya matukio wameona hali zao za kijamii zikizidi kudidimia na kuwa mbaya zaidi katika nyakati hizi ngumu za maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, hali ambayo imechochewa na matukio ya uhalifu, vurugu, rushwa na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kristo Mfufuka aendelee kusaidia mchakato wa upatanisho wa watu asilia nchini Canada pamoja na Kanisa Katoliki. Roho ya Kristo Mfufuka igange na kutibu madonda yaliyopita na hatimaye, awawezeshe watu wa Mungu kutafuta na kuambata ukweli na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, madhara ya vita ni makubwa sana, kwani vita inaendelea kusababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuporomoka na kuyumba kwa mfumo wa uchumi pamoja na ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula duniani. Katika maafa makubwa ya vita na upotevu wa maisha kutokana na sababu mbalimbali, Kristo Yesu Mshindi wa dhambi na mauti; woga na hofu anawaalika na kuwahimiza watu wa Mungu kutojikatia tamaa na kunyong’onyea kutokana na ubaya na vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Iwe ni nafasi kwa amani ya Kristo Mfufuka kushinda na kutamalaki kwani hili ni jambo linalowezekana kabisa. Amani kwanza kabisa ni wajibu na dhamana ya watu wote.

Urbi et Orbi 2022

 

17 April 2022, 14:42

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >