Tafuta

Kwaresima Ni Wakati Wa Kuamka Kutoka Usingizi wa Maisha Kiroho

Baba Mtakatifu Francisko amejikita zaidi katika mashuhuda wa Fumbo la Pasaka waliokuwa wameelemewa na usingizi mzito. Changamoto katika Maisha ya sala, Kwaresima kama kipindi muhimu cha kuamka kutoka katika usingizi wa maisha ya kiroho, tayari kuwasha taa na mwanga wa uwepo angavu wa Mungu katika maisha. Waamini wajenge utamaduni wa kusali daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko kwa waamini kuitafakari kashfa ya Fumbo la Msalaba, Utukufu wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na hatimaye ni kwa waamini kujikita katika maisha ya sala, ili kutoelemewa na usingizi, tayari kutamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kama ilivyoandikwa. Mwinjili Luka 9: 28-36 anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, na mavazi yake yakawa meupe pe! Katika mwanga wa utukufu wake, wakaonekana Musa, kielelezo cha Torati na Eliya anayewakilisha Manabiii, waliokuwa wajadiliana kuhusu Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake, uliokuwa machoni pake huko Yerusalemu. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 13 Machi 2022, amejikita zaidi katika mashuhuda wa Fumbo la Pasaka waliokuwa wameelemewa na usingizi mzito. Changamoto katika Maisha ya sala, Kwaresima kama kipindi muhimu cha kuamka kutoka katika usingizi wa maisha ya kiroho, tayari kuwasha taa na mwanga wa uwepo angavu wa Mungu katika maisha.

Kwaresima ni kipindi cha kuamka katika maisha ya kiroho.
Kwaresima ni kipindi cha kuamka katika maisha ya kiroho.

Mwinjili Luka katika simulizi hili, anakazia kwa kusema kwamba, Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wameelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wa Kristo Yesu na wale wawili waliosimama pamoja naye. Si jambo la bahati mbaya kwamba, hawa Mitume watatu, ndio wale wale “watakaouchapa” usingizi Bustanini Gethsemane alipokuwa akisali kwa huzuni. Rej. Mk 14: 37-41. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kitendo cha Mitume kuelemewa na usingizi wakati wa matukio muhimu kama haya, ni jambo la kushangaza sana. Lakini ikumbukwe kwamba, Sala ya Kristo Yesu ilikuwa ni ndefu, kiasi kwamba, ilichukua pia muda mrefu, katika tafakari ya kina iliyoambatana na kimya kikuu. Bila shaka hata wao pia walikuwa wanasali, lakini pole pole wakaelemewa na usingizi. Jambo kama hili linatokea hata kwa waamini katika ulimwengu mamboleo. Baada ya pilika pilika za siku, mwamini anapoamua kukaa kitambo na Kristo Yesu katika sala, mara anajikuta akitumbukia katika usingizi mzito. Inatokea pia hata ndani ya familia watu kushinda kuzungumza kutokana na kuelemewa na uchovu pamoja na usingizi mzito. Wengi wangependa kuwa macho na makini, ili kuonesha ushiriki wao mkamilifu, lakini wanajikuta wakielemewa na usingizi mzito.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kwaresima ni kipindi muafaka ambacho Mwenyezi Mungu anapenda kukitumia ili kuwaamsha waja wake kutoka katika usingizi wa maisha ya kiroho. Hii ni neema ambayo waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia na wala si kwa jeuri yao wenyewe. Wale Mitume watatu, mashuhuda wa mateso na kifo cha Kristo Yesu, walitamani kukesha huku wakiwa makini, lakini wanajikita “wakiuchapa usingizi.” Kwa nguvu zao wenyewe hawakuweza “kufua dafu” na matokeo yake wakajikuta wakisinzia na kuamka pale tu, Kristo Yesu alipokuwa anageuka sura. Kwa hakika hata waamini wanahitaji kupata mwanga angavu wa uwepo wa Mungu, ili awasaidie kuona mambo kwa jicho la tofauti. Hii ina maana kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayewaamsha na kuwapatia kiu na hamu ya kutaka kusali; kwa kujiangalia kutoka katika undani wa maisha ya mtu binafsi, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani. Waamini wanaweza kuvuka kikwazo cha mchoko wa mwili kwa nguvu ya Roho wa Mungu.

Waamini wajenge utamaduni wa kusali daima.
Waamini wajenge utamaduni wa kusali daima.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kabla ya kuzima taa na kulala, wahakikishe kwamba, wanawasha mwanga angavu wa uwepo wa Mungu. Hii inawezekana kwa kusoma sehemu ya Injili, kwa sababu Neno la Mungu ni mwanga angavu katika mapito ya maisha ya mwanadamu. Ni wakati wa kuangalia Msalaba wa Kristo, ili kushangazwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wajenge utamaduni wa kusali kabla ya kulala. Ni Mungu peke yake mwenye nguvu ya kuweza kuleta mageuzi makubwa katika safari ya maisha ya kila siku. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaacha waamini wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kuweka nyoyo zao wazi na hadharani, tayari kukipokea na kukitumia vyema, Kipindi hiki cha neema ya Kwaresima.

Papa Usingizi wa Kiroho

 

13 March 2022, 15:05

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >