Tafuta

Papa Francisko: Tamko: Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis”. Papa Francisko: Tamko: Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis”.  

TAMKO: Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor Unitas"

Baba Mtakatifu Francisko katika tamko lake la tarehe 21 Januari 2022 amemtangaza Mtakatifu Ireneo kuwa Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis”. Mtakatifu Ireneo ni maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, awe ni chachu kwa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika mchakato wa umoja kamili miongoni mwa Wakristo. Ni daraja la tasaufi na majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 20 Januari 2022 amekutana na kuzungumza na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu. Baba Mtakatifu amesikiliza kwa makini mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Baraza hili wakiomba Mtakatifu Ireneo atangazwe na Mama Kanisa kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika tamko lake la tarehe 21 Januari 2022 amemtangaza Mtakatifu Ireneo kuwa Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis”. Mtakatifu Ireneo ni maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, awe ni chachu kwa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika mchakato wa umoja kamili miongoni mwa Wakristo.

Ireneo kwa lugha ya Kigiriki ni Εἰρηναῖος, Eirēnáios, «Mtu wa Amani»; kwa Lugha ya Kilatini ni Irenaeus; aliyezaliwa huko Smirne, nchini Uturuki kunako mwaka 130 BK. Katika maisha yake alibahatika kuteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lyon nchini Ufaransa. Alikuwa ni mwanafunzi hodari wa Mtakatifu Polycarp aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo. Mwaka 177, baada ya kuhamia nchini Ufaransa, Ireneo alipewa Daraja Takatifu ya Upadre huko Lyons, na baada ya kutumwa kidogo Roma kama mjumbe kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro aliponea chupuchupu kuuawa katika madhulumu dhidi ya Wafiadini wa Lyon, na baadaye aliteuliwa kuwa askofu wa Jimbo hilo. Alifariki dunia huko Lyon kunako mwaka 202.

Ni Askofu aliyejibidiisha kunogesha umoja wa Wakristo dhidi ya uzushi wa “Wagnos”. Alikazia Mapokeo na Imani ya Kitume. Katika maandishi yake alijitahidi sana kutetea imani ya Kanisa Katoliki inayokita mizizi yake katika Mapokeo ya Mitume wa Yesu dhidi ya uzushi wa mafundisho ya “Wagnos” yaliyotegemea zaidi ujuzi ambao yeyote alidai kuwa nao akianzisha kikundi chake. Ni kiongozi wa kwanza pia kushuhudia Injili Nne kuwa Neno la Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis” alikuwa ni daraja la maisha ya kiroho na majadiliano ya kitaalimungu kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Jina lake kama linavyoonesha, alikuwa ni mtu wa amani aliyetoka kwa Bwana, ili kuwapatanisha na hatimaye, Wakristo wote waweze kuwa wamoja.

Mwalimu wa Kanisa

 

21 January 2022, 15:03