Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, tarehe 16 Januari 2022 linaadhimisha Dominika ya Amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, tarehe 16 Januari 2022 linaadhimisha Dominika ya Amani. 

Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani: Dominika ya Amani 16 Januari 2022

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, Dominika tarehe 16 Januari 2022 linaadhimisha Dominika ya Amani kwa kujikita katika ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya kuombea amani duniani. “Pax Christi” kimekuwa mstari wa mbele ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa amani nchini Uingereza na Walles. Watu watambue kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Elimu, Kazi Na Majadiliano Kati ya Vizazi: Nyenzo za Ujenzi wa Amani ya Kudumu.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakazia umuhimu wa wajumbe wa amani, majadiliano kati ya vizazi kama nyenzo ya ujenzi wa amani; mafunzo na elimu kama vikolezo vya amani; utengenezaji wa fursa za ajira unasaidia kujenga amani. Nabii Isaya akizungumzia kuhusu amani anasema: “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Nabii Isaya anakazia umuhimu wa mjumbe wa amani, kama kielelezo cha faraja na ahadi ya kupyaisha historia na mwanzo mwema wa maisha ya baadaye. Rej. Isa 52:7.

Familia nzima ya binadamu imeungana na kushikamana licha ya migawanyiko, kinzani, mipasuko pamoja na vita inayoendelea kurindima sehemu mbalimbali za dunia. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bado limetamalaki. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, hali ambayo imepelekea ongezeko la watu wanaokabiliwa na baa la njaa na ukame wa kutisha. Kuna sera na mikakati ya kiuchumi inayokita mizizi yake katika ubinafsi na uchoyo. Kumbe, kuna haja ya kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini, ili kujenga na kudumisha misingi ya amani na haki. Kimsingi jamii inawahitaji wajenzi na wasanii wa amani kutoka katika sakafu ya nyoyo zao watakaosaidia mchakato wa ujenzi wa amani kuanzia katika nyoyo za watu; kwa kuimarisha mahusiano kifamilia na kijamii; kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Haya ni mahusiano yanayopaswa kuboresha mafungamano na mahusiano kati ya jamii na Umoja wa Mataifa. Majadiliano kati ya vizazi kama nyenzo ya ujenzi wa amani yasaidie kuondokana na vita pamoja na mipasuko ya kijamii inayopelekea watu wengi kuzikimbia nchi zao. Majadiliano haya yanapaswa kusimikwa katika ukweli, uwazi, kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kudumisha utamaduni wa watu kukutana. Maambukizi makubwa ya ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, yamewasaidia watu wa Mungu kujenga na kudumisha huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Majadiliano ni mchakato unaohitaji sanaa ya kusikiliza, kushirikishana mawazo na hatimaye kufikia muafaka kwa kutembea kwa pamoja katika umoja.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, Dominika tarehe 16 Januari 2022 linaadhimisha Dominika ya Amani kwa kujikita katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea amani duniani. Chama cha Harakati za Amani Kimataifa, “Pax Christi” kimekuwa mstari wa mbele ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa amani nchini Uingereza na Walles. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema watambue kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika haki kama anavyobainisha Mtakatifu Paulo VI. Ujumbe wa amani kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa unasimikwa katika mchakato wa upatanisho, haki, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuwajengea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Maadhimisho haya yanachota pia ujumbe wake katika Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane 2: 1-12 kuhusu Harusi ya Kana ya Galilaya, Ishara ya ufunuo wa huruma na upendo; utukufu, ukuu na Umungu wa Kristo Yesu.

Kwa kawaida, harusi ni tukio linalowakutanisha vijana wa kizazi kipya na wazee ili kukoleza majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na ujenzi wa amani ya kudumu. Majadiliano yanasaidia kukuza na kudumisha kumbukumbu dhamana inayotekelezwa na wazee wakati ambapo historia inaendelezwa na vijana wa kizazi kipya. Watu wanapaswa kuthamini na kudumisha umoja na utofauti unaoonekana katika maisha. Huu ni wakati wa kuadhimisha na kuendeleza kazi kubwa ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano yanayowahusisha watu wa marika yote, kwa kuibua pia miradi inayoweza kutekelezwa kwa pamoja katika umoja. Mambo msingi ya kuzingatiwa ni majadiliano, ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kuamua na kutenda kwa umoja; ili kuweza kutembea kwa pamoja, sehemu muhimu wa mchakato wa ujenzi wa amani. Hii ndiyo njia muafaka ya mchakato wa ujenzi wa fadhila ya matumaini, ndoto na siasa mpya ili kuganga na kuponya madonda makubwa yanayojionesha kwenye kazi ya uumbaji kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Dominika ya Amani
15 January 2022, 15:57