Tafuta

Papa Francisko ametuma salama na matashi mema kwa Wakristo wa Makanisa ya Kiorthodox Mashariki wanapoadhimisha Noeli ya Bwana kwa mwaka 2022. Papa Francisko ametuma salama na matashi mema kwa Wakristo wa Makanisa ya Kiorthodox Mashariki wanapoadhimisha Noeli ya Bwana kwa mwaka 2022. 

Salam za Papa Francisko Kwa Noeli ya Makanisa ya Mashariki: Amani na Maendeleo

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania, tarehe 6 Januari 2022 amewakumbuka na kuwaombea Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox wanaoadhimisha Noeli ya Bwana, tarehe 7 Januari 2022. Amewatakia amani dumifu, ustawi na maendeleo ya kweli. Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, aangaze familia na jumuiya zao zote kwa mwanga wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makanisa ya Kiorthodox kutoka Mashariki tarehe 7 Januari 2022 yanaadhimisha Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Kiini cha imani ya Kikristo ni kwamba, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yn. 1:14. Huu ndio Ukweli wa Noeli na wala hakuna ukweli mwingine zaidi ya huu. Sherehe za Noeli ni mwaliko wa kutafakari changamoto zinazoibuliwa kwenye historia kutokana na majeraha ya dhambi. Mwanadamu anatafuta ukweli wa mambo, huruma ya Mungu na wokovu. Kwa upande mwingine, Mwenyezi Mungu kutokana, huruma, upendo, ukarimu na wema wake mkuu amekuja kukutana na wanadamu, ili kuwatangazia Ukweli unao okoa maisha na hivyo kuwashirikisha katika urafiki na maisha yake ya Kimungu. Zawadi hii ya Kimungu, inapokelewa katika hali ya unyenyekevu unaofumbatwa katika maisha ya Mwenyezi Mungu, wakati wa Sherehe za Noeli. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania, tarehe 6 Januari 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbuka na kuwaombea Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox wanaoadhimisha Noeli ya Bwana kwa Mwaka 2022. Amewatakia amani, ustawi na maendeleo ya kweli. Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, aangaze familia na jumuiya zao zote.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika ujumbe wake kwa Sherehe za Noeli kwa mwaka 2021-2022 anasema Neno wa Mungu alitwaa mwili, ili kuwatembelea na kukaa kati pamoja na waja wake. Waamini wanamtukuza, wanamsifu na kumwadhimisha kwa nyimbo na tenzi za rohoni. Hii ni kwa sababu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu ameutukuza na kuuza ubinadamu. Ni mwanga kwa mwanga, Mungu kweli na mtu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, wenye umungu mmoja na Baba ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka kutoka mbinguni, kwa ajili ya wokovu wa binadamu wote. Fumbo la Umwilisho linapita ufahamu wa binadamu, kwa sababu huu ni ukweli unaofunuliwa na Mungu mwenyewe, kwa kumwonesha mwanadamu ambaye ni mkalifu pasi na mawaa katika maisha yake yaani Kristo Yesu. Kwa kumheshimu na kumwabudu Mwenyezi Mungu, mwanadamu pia anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwenye haki na nyajibu zinazopaswa kutekelezwa barabara. Kanisa ambalo ni fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, linamwakilisha na kumhudumia Kristo Yesu katika Umungu na Ubinadamu mintarafu Liturujia ya Kanisa na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.

Ni katika mantiki hii kwamba, Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai na utakatifu wa maisha sanjari na kuendeleza mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa ni chombo cha baraka na neema zinazobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuna haja kwa Mama Kanisa kujikita zaidi katika majadiliano yenye tija na mvuto na wala si malumbano. Kanisa linahitaji toba na wongofu wa shughuli za kichungaji; ushiriki pamoja na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Ni mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika tasaufi na maisha ya Liturujia ya Kanisa, kwa ajili ya utukufu na sifa kwa Mwenyezi Mungu na utakatifu wa binadamu. Mama Kanisa anapaswa kuendelea kuwa mwaminifu katika Mapokeo yake, ili kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu changamoto zinazoibuliwa kwa nyakati hizi.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwa kusema, katika kipindi cha mwaka 2020-2021 watu wengi wameteseka, kufariki dunia na hata kujikatia tamaa kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuwawezesha watafiti na wanasayansi, kusaidia kupatikana kwa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hii ni changamoto kuhakikisha kwamba, chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 inawafikia watu wengi zaidi, sehemu mbalimbali za dunia, kwa kutambua kwamba, sayansi ni zawadi ya Mungu kwa binadamu na inapaswa kupokelewa kwa moyo wa shukrani na mapendo. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wameibuka kuwa ni washauri wa kiroho kwa kupinga matumizi ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Takwimu za kisayansi zinaonesha kwamba, chanjo imesaidia sana kupunguza maambukizi, na hatimaye vifo vywa wagonjwa wa UVIKO-19. Kupinga chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kuendelea kusambaza maambukizi ya UVIKO-19 ni kwenda kinyume kabisa cha Injili ya huruma na mapendo kwa Mungu na jirani na matokeo yake ni kuhatarisha maisha ya watu wengine, kama inavyojionesha kwa sasa. Watu wengi waliitikia na kuhamasika kuchanjwa dhidi ya UVIKO-19; wachache wakapinga, leo hii maambukizi ya UVIKO-19 yameongezeka maradufu. Ni matumaini ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwamba, maisha ya binadamu yataongozwa zaidi na hekima na busara ya Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, Mwaka 2022 uwe ni mwaka furaha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, licha ya changamoto na magumu yanayoweza kujitokeza. Mwaka 2022 uwe ni mwaka wa ukombozi kwa watu wote wa Mungu, kwa kumwachia nafasi Kristo Yesu kuongoza historia na hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani anawapenda na kuwalinda watu wote. Mwenyezi Mungu Mwokozi hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Rej. 1 Tim 2:4. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anawatakia watu wote wa Mungu maadhimisho mema ya Sherehe za Noeli, Mwenyezi Mungu apewe utukufu; mshikamano wa udugu na upendo, uendelee kuoneshwa kwa Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu.

Makanisa Mashariki

 

07 January 2022, 16:42