Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, “Motu Proprio”: “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia Akili Zao” ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, “Motu Proprio”: “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia Akili Zao” ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu  

Dominika ya III ya Neno la Mungu: Kuombea Umoja wa Wakristo 2022

Dominika ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene. Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Shuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, “Motu Proprio”: “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia Akili Zao” alianzisha Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa. Na kwa mwaka 2022, hii ni Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa tarehe 23 Januari 2022. Hii ni Dominika kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani huu ni wakati wa kuombea Umoja wa Wakristo. Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Kristo Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” Lk. 24:45. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Dei verbum” yaani “Neno la Mungu”, wanafafanua: maumbile na maana ya ufunuo; urithishaji wa ufunuo wa Mungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, Agano la Kale na Agano Jipya.

Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Makatekista kufundwa kikamilifu, ili wawasaidie waamini kukua katika imani kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu na Kristo Yesu mwenyewe. Neno la Mungu lina utajiri mkubwa na amana ya kufundishia. Neno la Mungu ni muhtasari wa Fumbo la Pasaka, chemchemi ya imani hai na ya ukweli wa maisha wa Fumbo na Mwenyezi Mungu. Neno lilifafanua historia ya wokovu, linabainisha maisha ya kiroho na kanuni ya Fumbo la Pasaka. Neno la Mungu ni chemchemi ya upendo unaomwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kumbe, Dominika ya Neno la Mungu ni mchakato wa kutambua utajiri usio na kikomo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na waja wake.

Hii pia ni Dominika kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo kwa kukoleza: uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Wakristo wasaidiane kusoma na kufafanua Maandiko Matakatifu. Makatekista kwa ajili ya huduma waliyo nayo, wawasaidie wengine kukuwa katika imani na hivyo kuendelea kupyaisha maisha na imani yao katika Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo wajenge na kuimarisha uhusiano wao na Maandiko Matakatifu, ili kuondoa ubaridi, vinginevyo macho yatabaki yamefungwa kutokana aina mbambali za upofu. Waamini wawe waaminifu katika kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu. Ufunuo wa Mungu unatimilika na kukamilika kwa njia ya Kristo Yesu; hata hivyo, Roho Mtakatifu anaendeleza kazi yake. Maana, tungepunguza hadhi ya kazi ya Roho Mtakatifu tukifikiri kwamba inahusu tu hali ya uvuvio wa kimungu wa Maandiko Matakatifu na waandishi wake mbalimbali tu. Ni muhimu kuwa na imani katika utendaji wa Roho Mtakatifu ambaye anaendelea kutimiza aina yake pekee ya uvuvio pale ambapo Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” yanafafanua kihalisi.

Baba Mtakatifu anaelezea kwamba “maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha za kibinadamu yameingia katika maneno ya wanadamu, kama vile Neno wa Baba wa milele alivyojifanya mtu, akichukua udhaifu wa maumbile ya kibinadamu” (na. 13). Ni sawa na kusema kwamba umwilisho wa Neno wa Mungu ni kielelezo na maana ya uhusiano baina Neno la Mungu na maneno ya wanadamu, yakiwa pamoja na maumbile yake ya kihistoria na kitamaduni. Ni katika tukio hili ambamo huundwa Mapokeo, ambayo pia ni Neno la Mungu. Rej. Dei verbum 9. Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Roho yuleyule ambaye kwake yaliandikwa, yanadumu daima kuwa mapya. Agano la Kale si kamwe kuukuu, likiwa ni sehemu ya Agano Jipya, kwa sababu yote yanageuzwa na yule Roho mmoja anayeyavuvia. Ujumla wa matini takatifu una tabia ya kinabii: nayo haihusu mambo yajayo, bali ya leo ya kila anayejilisha Neno hili. Yesu mwenyewe anasisitiza kwa wazi ukweli huu mwanzoni mwa kuhubiri kwake: “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk 4:21).

Neno la Mungu ni mwaliko wa daima wa kwenda kwenye upendo wa Mungu Baba uliojaa huruma na kuwadai watoto wake kuishi katika mapendo. Maisha ya Yesu ni kielelezo bora na kikamilifu cha upendo huu wa Mungu, asiyebakiza chochote kwa ajili yake, bali anajitolea kwa wote bila ubaguzi. Huu ni wito wa kushikamana na kufungamana na Kristo Yesu. Katika safari ya kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu, waamini wanaye Bikira Maria, aliyelisikiliza Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya linawaalika kwa namna ya pekee kabisa waamini kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Dominika ya III ya Neno la Mungu yananogeshwa na Neno la Mungu kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi, familia, jumuiya ndogondogo na hata kwenye mitandao ya kijamii, inayowakutanisha vijana wengi hata kama hawajawahi kuonana mubashara.

Neno la Mungu

 

 

 

 

21 January 2022, 16:00