Tafuta

Mlipuko wa volkano kwenye mlima Semeru Indonesia umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hili ni janga la kitaifa. Mlipuko wa volkano kwenye mlima Semeru Indonesia umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hili ni janga la kitaifa. 

Mlipuko wa Volkano Mlima wa Semeru Indonesia Wasababisha Maafa Makubwa.

Mlipuko wa Volkano Mlima Semeru umesababisha vifo vya watu zaidi ya 34 na wengine 16 hawajulikani mahali walipo baada ya makazi ya watu kufunikwa na tope la lava. Mlipuko huo umesababisha maafa makubwa kiasi kwamba, kuna baadhi ya vijiji vimefunikwa na tope. Watu wengine 56 wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mlipuko huo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mlipuko wa Volkano uliotokea kwenye Mlima wa Semeru, Wilaya ya Lumajang, Mkoa wa Java nchini Indonesia, Jumapili, tarehe 5 Desemba 2021 umesababisha vifo vya watu zaidi ya 34 na wengine 16 hawajulikani mahali walipo baada ya makazi ya watu kufunikwa na tope la lava. Mlipuko huo umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi kwamba, kuna baadhi ya vijiji vimefunikwa na tope. Watu wengine 56 wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na mlipuko huo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, amezipokea habari hizi kwa huzuni kubwa na kwamba, anapenda kuungana na watu wa Mungu nchini Indonesia waliofikwa na kuguswa na janga hili zito.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Indonesia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, kwa kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia; majeruhi waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku. Anawaombea wafanyakazi wanaoendesha zoezi la kuokoa watu, watambue kwamba, anawaombea na kuwapatia baraka zake za kitume ili waweze kuitekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu.  Kwa upande wake, Rais Joko Widodo wa Indonesia, Jumanne tarehe 7 Desemba 2021 ametembelea eneo la tukio na kukutana na waathirika. Majengo zaidi ya 2, 000 yataondolewa katika eneo la hatari ya mlipuko wa volkano na wakazi wa eneo hili watahamishiwa kwenye makazi ya muda katika kipindi cha miezi sita ijayo. Kila familia iliyoathirika itajengewa nyumba mpya na kupewa ruzuku ya kujikimu na hali ngumu ya maisha.

Volkano Indonesia

 

08 December 2021, 15:04