Tafuta

Wanasheria Wakatoliki Italia, "Unione Giuristi Cattolici Italiani " Simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Wanasheria Wakatoliki Italia, "Unione Giuristi Cattolici Italiani " Simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. 

Wanasheria Simameni Kidete Kulinda Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu

Papa Francisko anawataka wanasheria kusimama kidete kulinda: Utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, wakimbizi na wahamiaji, wagonjwa na watoto ambao bado hawajazaliwa; wagonjwa walioko kufani na maskini ni kati ya makundi ambayo yanasukumizwa katika utamaduni wa kutupa. Kwa wale ambao hawachangii katika ukuaji wa uchumi si mali kitu! Sheria na Haki ni Muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya Kitume nchini Cyprus na Ugiriki, tarehe 5 Desemba 2021 alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji kwenye Kisiwa cha Lesvos nchini Ugiriki. Alisema kuna haja ya kukuza na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na uhuru ili kuvuka mipaka ya hofu na migawanyiko isiyokuwa na mvuto wala mashiko. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto inayopaswa kushughuliwa na wote kama yalivyo pia maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwamba, licha ya Jumuiya ya Kimataifa kuchelewa kutekeleza sera na mikakati ya mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini kwa sasa dalili za matumaini zinaanza kujitokeza. Lakini kwa wakimbizi na wahamiaji, changamoto hii imewekwa kando, ingawa maisha ya watu yanawekwa rehani, amani na utulivu viko mashakani. Ni kwa njia ya upatanisho wa kweli na maskini, maendeleo kwa siku za usoni yanaweza kupatikana. Pale maskini wanaposukumizwa pembezoni mwa jamii, amani iko mashakani!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, utashi imara wa kustahi utu wa watu wengine na mataifa mengine, pamoja na uzingativu thabiti wa udugu wa kibinadamu ni vya lazima kabisa katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Rej. GS, 78. Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na Umoja wa Wanasheria Wakatoliki wa Italia “L’Unione Giuristi Cattolici Italiani”, Ijumaa tarehe 10 Desemba 2021 alikazia tena umuhimu wa wanasheria kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anasema, kwa bahati mbaya sana, hata leo hii, tabia ya unyanyasaji, unyonyaji, uzembe na kutotimiza wajibu kunapelekea wale wote wasiokuwa na ulinzi madhubuti kutumbukizwa katika utamaduni wa kutupa na hatimaye, kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanasheria Wakatoliki wanahamasishwa kusimama kidete ili kubadili mwelekeo huu potofu, kwa kuzingatia weledi, taaluma na nafasi zao, huku wakiongozwa na dhamiri nyofu pamoja na uwajibikaji makini. Hata maskini wanayo haki ya kulindwa na kutetewa na huu ni msukumo unaopata chimbuko lake katika msingi wa imani.

Katika Kipindi hiki cha Majilio, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanakumbushwa maneno ya Nabii Isaya akisema “Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.” Isa 42: 3-4. Hapa Nabii Isaya anakazia Sheria na Haki. Kristo Yesu katika maisha na utume wake hapa duniani, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Akawaganga na kuwaponya; akawasamehe dhambi zao; akawalisha na kuwanywesha, lakini zaidi akwatangazia na kuwashuhudia Habari Njema ya Wokovu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Ni katika hali na mazingira kama haya, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wanasheria Wakatoliki kusimama kidete kulinda na kutetea haki za maskini na wanyonge katika mfumo wa uchumi na kijamii unaojidai kuwashirikisha wote, lakini ukweli wa mambo ni kwamba kuna watu ambao wanatengwa na jamii na wala hawana tena sauti. Haki msingi za wafanyakazi, wakimbizi na wahamiaji, wagonjwa na watoto ambao bado hawajazaliwa; wagonjwa walioko kufani na maskini ni kati ya makundi ambayo yanasukumizwa katika utamaduni wa kutupa. Kwa wale ambao hawachangii katika mchakato wa ukuaji wa uchumi si mali kitu. Kwa kuwakosesha haki msingi za binadamu ni sawa na kutweza utu na heshima yao kama binadamu, kwa kushindwa kupata matibabu ya: kimwili, kisaikolojia, ujira wa haki na unaotosheleza mahitaji msingi ya binadamu ni sawa na “kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu.”

Leo hii nchini Italia kuna wafanyakazi wanaonyanyaswa na kudhulumiwa wakati wa kuvuna mazao, kwani wanafanya kazi kubwa lakini kwa ujira “kiduchu” na wakati mwingine, wanafukuzwa bila hata ya kupewa hifadhi ya kijamii. Kumbe, ni wajibu wao kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha sheria zinazolinda haki na hasa haki za maskini, utu na heshima yao. Wanasheria Wakatoliki katika taaluma yao, wanapaswa kusaidia kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuendeleza pia udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haki msingi za maskini si haki dhaifu hata kidogo. Haki hizi zilindwe kwa hekima na busara; kwa kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu na haki.

Wanasheria
11 December 2021, 15:02