Tafuta

Mtakatifu Yohane Paulo II Mwaka 1984 alitangaza kwamba Bikira Maria ni Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Waraka wake wa kitume "Tot tantaeque". Mtakatifu Yohane Paulo II Mwaka 1984 alitangaza kwamba Bikira Maria ni Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Waraka wake wa kitume "Tot tantaeque". 

Mt. Yohane Paulo II: B. Maria Ni Mlinzi na Mwombezi wa Tanzania

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kama Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awaombee watu wa Mungu Tanzania fadhila ya upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake wa 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Sherehe ya B. Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini Tanzania ifikapo tarehe 9 Desemba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tanzania inaposherehekea Miaka 60 ya Uhuru: 1961-2021 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Tanzania Imara, Kazi Iendelee” tujikumbeshe kwamba, ilikuwa ni tarehe 8 Novemba 1984, Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka unaojulikana kama “Tot tantaeque” yaani “Bikira Maria ameidhinishwa kuwa Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Ioannes Paulus . Li Litterae Apostolicae Tot Tantaeque Beata Virgo Immaculata Patrona Confirmatur Rei Publicae Tanzaniensis” Hili ni ombi lililotolewa kwa wakati huo na Askofu Anthony Petro Mayalla wa Jimbo Katoliki la Musoma, ambaye alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kuomba ili Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aweze kuwa ni Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia familia ya Mungu nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya uhuru, siku moja tu, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka huu wa Kitume, anasema hapa duniani kuna matatizo na magumu mengi yanayowakabili wafuasi wa Kristo Yesu. Kumbe, wanatafuta ulinzi si tu katika hekima ya binadamu, kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hata pia kutoka kwa Bikira Maria, anayewapenda na kulinda watoto wake. Kumbe, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia ombi la kuadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kama Mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili awakirimie watu wa Mungu nchini Tanzania fadhila ya upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake mkuu wa mwaka uliofanyika Juni 2016 liliamua kwamba, kuanzia sasa Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili itakuwa inaadhimishwa kitaifa nchini Tanzania ifikapo tarehe 9 Desemba.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika barua yake kwa ajili ya tukio hili alisema uamuzi huu ni utekelezaji wa zawadi iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 kwa kuiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Kumbe, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Tanzania, Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili kitaifa nchini Tanzania iliadhimishwa rasmi tarehe 9 Desemba 2016. Hii ni nafasi ya kuombea familia ya Mungu nchini Tanzania ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, nguzo msingi ambazo daima zimewatambulisha watanzania katika Jumuiya ya Kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Mtakatifu Yohane XXIII aliwaombea watanzania upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila na utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; pamoja na viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele, Amina. Tanzania Imara, Kazi Iendelee!

Tanzania
08 December 2021, 16:02