Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana ameelezea kwa ufupi yale yaliyojiri katika hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana ameelezea kwa ufupi yale yaliyojiri katika hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki. 

Hija ya Kitume Ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Yaliyojiri Kwa Ufupi!

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Alhamisi tarehe 2 Desemba hadi tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija yake ya 35 ya Kimataifa nchini Cyprus na Ugiriki na amewashukuru watu wote wa Mungu katika nchi hizi mbili kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomwenesha alipokuwa kati yao.. Wakimbizi na Wahamiaji, Majadiliano ya Kiekumene na Udugu wa Kibinadamu ni mambo msingi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jumatano tarehe 8 Desemba 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amegusia kuhusu hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Alhamisi tarehe 2 Desemba hadi tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija yake ya 35 ya Kimataifa nchini Cyprus na Ugiriki na amewashukuru watu wote wa Mungu katika nchi hizi mbili kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomwenesha alipokuwa kati yao. Hija ya Kitume ya 35 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Cyprus kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 4 Desemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani.” Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, lulu ya thamani ya Cyprus imechafuliwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao umekuwa ni kikwazo kwa watalii kutembelea Kisiwani hapo. Ni nchi ambayo imeathirika kutokana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, lakini taratibu, Cyprus inaanza tena kuimarika kiuchumi. Jambo la msingi ni kusimama kidete ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma; mambo yanayokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu na matokeo yake ni kukua na kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.

Cyprus imejeruhiwa sana na ukosefu wa uhuru wa kuabudu kwani tangu kumeguka kwa Cyprus kuna watu ambao hawajapata mahali pa kuabudia. Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na ukuta unaoigawa Cyprus katika vipande viwili. Amegusia maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima. Katika hotuba yake alikumbushia hija yake ya kitume aliyoifanya Kisiwani Lesvos; Umuhimu wa kuendelea kurutubisha ushirika kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwapaka mafuta ya ushirika, ili kunogesha ushirika wa kidugu unaovuta neema ya Mungu. Wakristo wawe wanyenyekevu ili Roho Mtakatifu aweze kuwapaka mafuta ya hekima inayomwilishwa katika huduma. Hata katika tofauti zao msingi, Wakristo wanapaswa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mama Kanisa, anayewasindikiza, kuwalinda na kuwashika mkono ili kusonga mbele kama ndugu wamoja. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Cyprus itaendelea kuwa ni maabara ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kuthamianiana. Akiwa Kisiwani Lesvos ameona kwa macho yake “makavu” mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji. Mateso na mahangaiko yao yaondoe tabia ya kutojali mahangaiko ya wengine na hivyo kuwaangalia machoni ili kuamsha tena dhamiri nyofu.

Kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 alitembelea nchini Ugiriki, hija ambayo ilinogeshwa kwa kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Katika hotuba yake aligusia kuhusu demokrasia shirikishi, Mchango wa Ukanda wa Mediterrania, Athari za UVIKO-19 pamoja na Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Ametembelea Ugiriki kama hujaji katika nchi ambayo imesheheni utajiri wa tasaufi, utamaduni na maendeleo; chemchemi ya furaha inayorutubisha hekima na hivyo kushirikisha uzuri. Watu wote wa Mungu wanahimizwa kuwashirikisha wengine furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na kwamba, Wagiriki wanayo nafasi ya pekee katika mchakato wa kunogesha furaha ya kweli nchini humo na Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, akiwa nchini Ugiriki amebahatika kukutana na watu wa Mungu nchini humo katika maadhimisho ya Dominika yaani Siku ya Bwana. Amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki. Na hatimaye, alikutana na kuagana na Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima, kumbukumbu ambayo ameihifadhi katika sakafu ya moyo wake. Baba Mtakatifu anapenda kuyahifadhi matunda ya hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuombea mbegu hizi za mikutano na matumaini ili ziweze kuzaa uvumilivu na hatimaye kuchanua matunda ya kuaminiana.

Hija ya Kitume
09 December 2021, 15:11