Tafuta

Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda za vijana wa kizazi kipya kutoka Ugiriki na kuwataka kuwa ni jasiri wa matumaini katika ulimwengu mamboleo pasi na kukata tamaa. Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda za vijana wa kizazi kipya kutoka Ugiriki na kuwataka kuwa ni jasiri wa matumaini katika ulimwengu mamboleo pasi na kukata tamaa. 

Hija ya Kitume Ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Vijana Jengeni Ujasiri wa Matumaini

Vijana wajenge utamaduni wa kusamehe, kusahau na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Vijana watambue ufunuo wa Sura ya Mungu kwa njia ya jirani zao na kwamba, maisha yanapaswa kuwa ni sehemu ya huduma kwa Mungu na jirani, wajitahidi daima kumwilisha udugu wa kibinadamu katika maisha yao. Mambo yote haya yawasaidie vijana kuwa ujasiri wa matumaini. UJANA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija ya 35 ya kitume kimataifa nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu amehitimisha hija yake ya kitume nchini Ugiriki kwa kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki. Mkutano huu umefanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Dionisi “St. Dionysius School” katika shule inayoendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Watawa wa Mtakatifu Ursula huko Maroussi mjini Athene nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusikiliza shuhuda za vijana kutoka nchini Ugiriki na hatimaye, akawapatia wosia wake wa kitume. Baba Mtakatifu amewafafanuliwa vijana kuhusu tatizo la mashaka ya imani, kutoeleweka na vijana wenzao na changamoto za maisha, watambue kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu na kwamba, hiki ndicho kiini cha imani. Vijana wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau na kamwe wasichoke kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Vijana watambue ufunuo wa Sura ya Mungu kwa njia ya jirani zao na kwamba, maisha yanapaswa kuwa ni sehemu ya huduma kwa Mungu na jirani, wajitahidi daima kumwilisha udugu wa kibinadamu katika maisha yao. Mambo yote haya yawasaidie vijana kuwa ujasiri wa matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anasema mashaka katika imani ni virutubisho vinavyoiwezesha imani kukua na kukomaa, kwa kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuandamana nao hatua kwa hatua, awatie moyo pale wanakumbana na mashaka; awashike mkono na kuwanyanyua pale wanapoteleza na kuanguka. Kila siku wajitahidi kuboresha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Vijana katika shida na mahangaiko yao ya ndani na wakati mwingine kutoeleweka, kiasi cha kukosa imani, amani na utulivu wa ndani, wajifunze kuona mshangao wa Mungu katika maisha yao mintarafu fumbo la maisha na kazi ya uumbaji.

Falsafa ya maisha iwasaidie kuboresha imani katika Kristo Yesu, tayari kuanzisha majadiliano na Yesu kwa njia ya sala. Vijana watambue kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Kumbe, ni jukumu lao kumpenda Mungu na jirani kwa sababu Mwenyezi Mungu anawapenda daima na wala hajutii kuwapenda watoto wake licha ya dhambi na mapungufu yao ya maisha. Mwenyezi Mungu amemuumba manadamu kwa jinsi ya ajabu na ya kutisha na matendo ya Mungu ni ya ajabu sana. Rej.  Zab 139:14. Vijana wajifunze kuangalia mshangao wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa kusamehe na kusahau kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, msamaha na mapendo daima anasamehe na kusahau. Vijana wajenge utamaduni wa kukimbilia na kuambata msamaha wa Mungu katika maisha yao na kamwe wasikatishwe tamaa na matangazo ya biashara. Jambo la msingi vijana wajitambue jinsi walivyo yaani: karama, na mapungufu yao ya kibinadamu na kujikubali wakati huu wanaposafiri kwenda nyumbani kwa Baba.

Leo hii, vijana wengi wamekuwa ni wahanga wa matangazo ya biashara yanayotaka kuwateka na kuwatumbukiza katika ulaji wa kupindukia. Vijana watambue kwamba, inapendeza kuwa Wakristo na waendelee kushangazwa na furaha na uzuri wa Injili. Kama Wakristo wajitahidi kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu anawapenda kipeo na kwamba, kila mmoja wao ni wapekee kabisa mbele ya upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwa njia ya mshangao wa Mungu katika maisha yao, kwenye kazi ya uumbaji, katika mchakato wa ujenzi wa urafiki na ushirikiano; kwa kujikita katika huruma na msamaha wa Mungu, wanaweza kugundua sura ya ufunuo wa Uso wa Mungu katika sura za jirani zao. Vijana wajitahidi kutambua uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao, kwa kuwathamini na kuwajali jirani zao, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kitabu cha Matendo ya Mitume ni ushuhuda wa maisha ya Wakristo wa Kanisa la kwanza. Kila mtu ni kitabu cha ufunuo wa Mungu, changamoto ya kujenga na kudumisha ujirani mwema.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua maisha kuwa ni sehemu ya mchakato wa huduma kwa Mungu na jirani. Kwa kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine, maisha yanaendelea kupyaishwa daima. Vijana wajenge utamaduni wa kukutana na jirani zao katika uhalisia wa maisha kwani mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii yana utajiri na mapungufu yake makubwa. Vijana wajenge utamaduni wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na mafungamano ya kijamii. Wajiamini wanapokutana na wenzao ili kwa pamoja waweze kushirikishana ile furaha ya Injili na huduma makini kwa jirani. Vijana wajenge na kuimarisha mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa kuthaminiana na kuwaona vijana wengine kuwa ni sehemu ya maisha yao, licha ya tofauti wa mahali wanapotoka, historia, imani na dini zao. Huu ni wakati kwa vijana kuota na kumwilisha ndoto ya udugu wa kibinadamu na kamwe wasikubali kuzeeka na kuanza kula “pensheni” kwa kubweteka kuangalia luninga. Nchi ya Ugiriki ni maarufu sana kwa michezo ya kale kama vile michezo ya Olimpiki na mbio ndefu za nyikani maarufu kama “Marathon.”

Baba Mtakatifu anawaka vijana waendelee kufanya mazoezi ya ujenzi wa  udugu wa kibinadamu. Vijana wengi wamelazimika kuzikimbia nchi na familia zao kutokana na: vita, nyanyaso, dhuluma na ukosefu wa haki msingi za binadamu; umaskini pamoja na majanga mbalimbali ya maisha. Katika shida na mahangaiko ya maisha, vijana wasipoteze imani, matumaini na mapendo. Lazima wote wapambane na hali zao, kwani wokovu wa Mwenyezi Mungu, iko siku utawafikia. Vijana wasikate wala kukatishwa tamaa, bali waendelee kuota ndoto kubwa kwa kuwa na ujasiri wa matumaini. Wafanye maamuzi mazito ya maisha kwa ujasiri, hasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amehitimisha majadiliano yake na vijana wa kizazi kipya kutoka nchini Ugiriki kwa kuwataka kusonga mbele kwa ari na mamko mpya. Wawe tayari kuthubu kuwaendea jirani zao, ili kujenga ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Wawe na ujasiri wa kugundua maana ya maisha!

Papa Vijana
06 December 2021, 16:41