Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya 35 ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki amesikiliza shuhuda za huduma zinazotolewa na Kanisa nchini Cyprus. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya 35 ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki amesikiliza shuhuda za huduma zinazotolewa na Kanisa nchini Cyprus. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Shuhuda za Imani

Kanisa liko mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; linajitahidi kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za imani, maadili na utu wema, ili waweze kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa. Kanisa linawahudumia wagonjwa na maskini, kielelezo cha faraja, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Bechara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili kuzungumza na Wakleri, watawa, makatekista pamoja na wanachama wa vyama vya kitume nchini Cyprus amekazia umuhimu wa ushuhuda wa imani. Mkutano huu umefanyikia kwenye Kanisa kuu la Bikira wa Neema huko Nicossia amewatambulisha viongozi wakuu wa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao ambao walikusanyika ili kusikiliza ujumbe wa Baba Mtakatifu wakati huu wa hija yake ya kitume nchini Cyprus. Hawa ni waamini waliofika Kisiwani Cyprus kunako mwaka 1192 na tayari mwaka 1121, Kanisa likaanza kupata viongozi mahalia. Tangu wakati huo, Kanisa limejikita zaidi katika mchakato wa huduma ya elimu, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni waamini wanaoishi kwa amani na utulivu!

Kwa upande wake, Sr. Perpetua Nyein Nyein Loo, amesema, Cyprus kwa sasa inahudumiwa na Mashirika manne ya kitawa, yanayojihusisha na shughuli za kichungaji, elimu na ustawi wa jamii. Kanisa liko mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuwasaidia walemavu ili waweze kutekeleza ndoto katika maisha yao. Kanisa linaendelea kujitahidi kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za imani, maadili na utu wema, ili waweze kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa. Kanisa linaendelea pia kuwahudumia wagonjwa na maskini, kielelezo cha faraja, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kimsingi watawa na makatekista wamekuwa mstari wa mbele katika katekesi na maandalizi ya waamini kwa ajili ya kupokea na kuadhimisha Sakramenti za Kanisa sanjari na majiundo endelevu.

Naye Sr. Antonia Piripitsi, amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kuhusu huduma inayotolewa na Kanisa katika sekta ya elimu kwa watu wote bila ubaguzi na kwamba, shule na taasisi za Kanisa zimesaidia kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Lengo ni kujenga leo na kesho yenye matumaini zaidi, wote wakitambuana kuwa ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Mpasuko wa Cyprus wa Mwaka 1974 ulipelekea baadhi ya watawa kukimbia na kurejea nchini mwao baada ya machafuko ya kisiasa. Licha ya changamoto hii, lakini bado watawa wanaendelea kutoa huduma kwa watu wa Mungu nchini Cyprus. Hapa watawa wanayo fursa ya kutangaza na kushuhudia wito na maisha yao ya kitawa. Shirika la Watawa Wamisionari wa Mtakatifu Francisko linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu waanze utume wao Ukanda wa Mashariki ya Kati na kilele chake ni mwaka 2022. Watawa wanaahidi kuendelea kutekeleza utume wao kwa ari na moyo mkuu, daima wakijitahidi kupyaisha maisha kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili.

Cyprus Ushuhuda

 

02 December 2021, 15:46