Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki kwa kunogesha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakatoliki na Waorthodox. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki kwa kunogesha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakatoliki na Waorthodox. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Matashi Mema

Baba Mtakatifu amehitimisha hija yake ya kitume Cyprus na Ugiriki. Lengo: Kuzima kiu ya maisha ya kiroho kutoka katika chemchemi ya imani ya kitume na udugu wa kibinadamu kati ya Wakristo wa Makanisa mbalimbali. Ilikuwa ni nafasi ya kukaribia na kugusa madonda ya majeraha ya ubinadamu miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na matumaini zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Alhamisi tarehe 2 Desemba hadi tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija yake ya 35 ya Kimataifa nchini Cyprus na Ugiriki. Alikwenda kuwatembelea watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambazo zina utajiri mkubwa wa historia, tasaufi na utamaduni. Ni hija iliyolenga kuzima kiu ya maisha ya kiroho kutoka katika chemchemi ya imani ya kitume na udugu wa kibinadamu kati ya Wakristo wa Makanisa mbalimbali. Ilikuwa ni nafasi ya kukaribia na kugusa madonda ya majeraha ya ubinadamu miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na matumaini zaidi.

Baba Mtakatifu Jumatatu, tarehe 6 Desemba 2021 akiwa njiani kurejea mjini Vatican alimtumia Rais Katerina Sakellaropoulou wa Ugiriki ujumbe wa shukrani kwake binafsi na watu wa Mungu nchini Ugiriki katika ujumla wao, kwa mapokezi na ukarimu mkubwa waliomwonjesha wakati wa hija yake nchini mwao. Amewahakikishia sala na kuwapatia baraka zake za kitume. Alipoingia kwenye anga la Italia, Baba Mtakatifu amemtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia ujumbe wa heri na baraka baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki, ambako amejielekeza zaidi katika majadiliano ya kiekumene, uimarishaji wa demokrasia na ujenzi wa mafungamano ya kijamii kati ya watu wa Mataifa. Amewatakia heri na baraka watu wote wa Mungu nchini Italia.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Fumicino, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko mjini Roma kwa ajili ya kumshukuru Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus Populi Romani”. Katika sala yake ya shukrani, amemwelezea Bikira Maria yale yaliyojiri katika hija yake, nyuso alizokutana nazo pamoja na historia za watu aliokutana nao na kuwakabidhi wote hawa katika ulinzi na tunza yake ya Kimama! Baba Mtakatifu Francisko akaendelea na safari yake ya kurejea tena mjini Vatican.

Matashi Mema
07 December 2021, 16:04