Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waandishi wa habari kupokea ujumbe wa madonda makuu ya binadamu katika hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki kuanzia tarehe 2-6 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waandishi wa habari kupokea ujumbe wa madonda makuu ya binadamu katika hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki kuanzia tarehe 2-6 Desemba 2021. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Madonda Makuu

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume ya 35 Kimataifa kwa kutembelea Cyprus na Ugiriki, amewatumia salam za matashi mema wakuu wa nchi wa Italia na Ugiriki. Kwa namna ya pekee anawaalika waandishi wa habari ambao wako kwenye msafara wake kupokea ujumbe wa madonda makuu ya binadamu katika hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki. Kumekucha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Ni yule Mtume aliyekuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume anapenda kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kufarijiana katika imani, kama sehemu ya nyenzo muhimu katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano, ujenzi wa madaraja ya watu kukutana sanjari na ukarimu; amali za jamii nchini Cyprus. Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni tarehe 1 Desemba 2021 alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma, kabla ya kuanza hija yake nchini Cyprus na Ugiriki.

Alhamisi asubuhi, tarehe 2 Desemba 2021 amekutana na kusali na wakimbizi pamoja na wahamiaji kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Malaika, “Santa Maria Degli Angeli” karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Fiumicino, ili kusali na kusalimiana na wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa Parokiani hapo.   Akiwa njiani kuelekea Cyprus, Baba Mtakatifu amemtumia salam na matashi mema, Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimwelezea kuhusu safari ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki, ili kuzima kiu kutoka katika chemchemi ya imani. Baba Mtakatifu anapenda kukutana na ndugu zake katika imani na watu wa Mungu katika nchi hizi. Baba Mtakatifu anawatakia watu wa Mungu nchini Italia utulivu na ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu alipoingia kwenye anga la Ugiriki amemtumia salam na matashi mema Rais Katerina Sakellaropoulou wa Ugiriki, akiwaombea watu wa Mungu nchini Ugiriki sanjari na kuona shauku ya kukutana na wananchi wa Ugiriki kuanzia tarehe 4 hadi 6 Desemba 2021. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume.

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe mwanana wakati wa kuanza hija yake 35 Kimataifa nchini Cyprus na Ugiriki amesema kwamba, haya ni maeneo ambayo katika historia yamewakutanisha watu kutoka katika tamaduni mbalimbali kiasi cha kutajirishana. Ni wajibu na dhamana ya watu wote kuhakikisha kwamba,  Ukanda wa Mediterrania unakuwa na amani, ukarimu kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Rais Sergio Mattarella amemtakia Baba Mtakatifu Francisko safari njema. Kuna waandishi wa habari 77 ambao wako kwenye msafara wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus na Ugiriki. Akizungumza nao, Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, hii ni hija maalum inayopania kugusa madonda ya binadamu. Ni matumaini yake kwamba, wale wote walioko kwenye msafara wake, wataweza kuupokea ujumbe huu, watakaokutana nao. Amewashukuru kwa kuwepo na huduma yao!

Salam na Matashi Mema

 

02 December 2021, 15:02