Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Novemba 2021 ameshiriki katika ufunguzi wa mkutano wa 75 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Novemba 2021 ameshiriki katika ufunguzi wa mkutano wa 75 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. 

Papa Francisko na Ujumbe wa Heri za Maaskofu Katika Utume Wao.

Mkutano wa 75 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia unanogeshwa na kauli mbiu “Safari ya Kisinodi kwa Makanisa Nchini Italia.” Baba Mtakatifu amependa kutumia fursa hii, kuteta kwa faragha na Maaskofu kwa kuwapatia Heri za Maaskofu zinazowataka kujibidiisha kuishi fadhila ya ufukara wa Kiinjili kama sehemu ya ushuhuda wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji nchini Italia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuanzia tarehe 22-25 Novemba 2021 linaadhimisha Mkutano mkuu wa 75, ambao umefunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 22 Novemba 2021. Mkutano wa 75 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia unanogeshwa na kauli mbiu “Safari ya Kisinodi kwa Makanisa Nchini Italia.” Baba Mtakatifu amependa kutumia fursa hii, kuteta kwa faragha na Maaskofu Katoliki wa Italia kwa kuwapatia Heri za Maaskofu zinazowataka kujibidiisha kuishi fadhila ya ufukara wa Kiinjili kama sehemu ya ushuhuda wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa watu wa Mungu nchini Italia. Heri Askofu ambaye anatumia ufukara kama ushirikishaji wa mtindo wake wa maisha, kwa sababu kwa njia ya ushuhuda huu anajenga Ufalme wa Mungu. Heri Askofu yule ambaye haoni haya kulowanisha uso wake kwa machozi mbele ya watu kwa sababu kwa njia ya machozi haya, aweze kuakisi mateso na machungu ya watu wa Mungu; mateso na mahangiko ya wakleri, ili kwa njia yake, wale wote wanaoteseka waweze kupata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Heri Askofu yule ambaye anauona utume wake kuwa ni huduma na wala si kielelezo cha utawala na hivyo kuifanya fadhila ya unyenyekevu kuwa nguvu yake katika huduma, kwa kutoa haki ya uraia kwa wote wanaobisha hodi katika moyo wake, ili wanyenyekevu wa moyo wapate kuishi katika nchi ya ahadi! Heri Askofu yule ambaye hajifungii kwenye jumba la utawala, na kamwe hakumbatii ukiritimba unaozingatia idadi na kusahau sura za watu; historia zao na daima akishirikiana nao katika kutekeleza ndoto ya Haki ya Mungu, kwa sababu kwa kukutana na Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya wa sala ya kila siku, inageuka kuwa ni lishe ya maisha na utume wake! Heri Askofu ambaye anaguswa na umaskini wa watu wa Mungu, anayethubutu kuwahudumia watu katika utu wao, ili kuwawezesha kuwa watu wa thamani kama dhahabu mbele ya Mungu. Heri Askofu ambaye hakwaziki kwa udhaifu wa jirani yake kwa sababu anatambua udhaifu wake binafsi, kwa vile Uso wa Kristo Yesu Mfufuka, utakuwa ni mhuri wa huruma yake!

Heri Askofu ambaye si mnafiki ndani ya moyo wake, anayeota ndoto ya uzuri na wema hata kama kuna uwepo wa ubaya na dhambi, kwa sababu atakuwa na uwezo kufurahia Uso wa Mungu katika mahangaiko ya watu wa Mungu. Heri Askofu yule ambaye ni mtu wa amani, anayewasindikiza watu katika hija ya upatanisho; anayepandikiza katika sakafu ya nyoyo za wakleri wake mbegu ya ushirika; anayesindikiza jamii iliyomeguka na kugawanyika katika mawazo ya upatanisho; anashikana mikono na watu wote wenye mapenzi mema kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; Mwenyezi Mungu atamtambua kuwa ni mtoto wake mpendwa. Heri Askofu kwa ajili ya Injili haogopi kupambana na mawimbi mazito, wala kujiachilia kumezwa na hali ya kutofahamika na vikwazo mbalimbali kwani anatambua kwamba Ufalme wa Mungu unaendelea kujengeka katikati ya kinzani za kiulimwengu.

Kwa upande wake, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, alimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko huku akikazia umuhimu wa urika wa Maaskofu na dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Mkutano huu ni kielelezo cha Kanisa linaloishi na kutenda katika nguvu ya Roho Mtakatifu, Neno la Mungu linalowawezesha kuzama hadi kilindini katika mafumbo ya Kanisa, ili hatimaye, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 75 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia yalizinduliwa kunako mwezi Mei 2021 kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye mara kwa mara amekuwa akishiriki pamoja nao kama ilivyokuwa tarehe 27 Februari 2021, Mkutano wa Kiekumene uliofanyika Jimbo kuu la Bari, Mwezi Februari 2020 na alipokutana na vijana wa kizazi kipya mara baada ya Sherehe ya Pasaka. Huu ni wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Huu ni muda muafaka kwa Kanisa kujenga na kuimarisha dhana ya Sinodi kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza na hivyo kuliwezesha Kanisa kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu.

Maaskofu Italia 2021
23 November 2021, 15:23