Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu nchini Scotland barua na kuwataka kuwaombea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia watu wa Mungu nchini Scotland barua na kuwataka kuwaombea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. 

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa COP26: Barua ya Papa Scotland

Papa katika barua yake kwa waamini nchini Scotland anasema, alitamani sana kushiriki mkutano wa COP26. Anawashukuru kwa kumuunga mkono katika nia hii njema katika kukabiliana na moja ya changamoto kubwa za kimaadili katika nyakati hizi yaani: Utunzaji bora wa Kazi ya Uumbaji, aliyokabidhiwa binadamu kama bustani, ili aitunze kama nyumba ya familia ya binadamu! COP26!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2021 ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani ambacho kimekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa watu na mali zao! Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa familia ya Mungu nchini Scotland anasema, alitamani sana kuwa pamoja nao na kushiriki mkutano wa COP26. Anawashukuru kwa kumuunga mkono katika nia hii njema katika kukabiliana na moja ya changamoto kubwa za kimaadili katika nyakati hizi yaani: Utunzaji bora wa Kazi ya Uumbaji, aliyokabidhiwa binadamu kama bustani, ili aitunze kama nyumba ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Scotland kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopewa dhamana na madaraka ya kuongoza Jumuiya ya Kimataifa, ili wawe na hekima itakayowasaidia kutoa maamuzi mazito ili kuweza kukabiliana na changamoto kwa ajili ya kizazi cha sasa na vile vijavyo! Muda unazidi kuyoyoma kwa kasi kubwa, hii ni fursa inayopaswa kutumiwa vyema, vinginevyo, watu watahukumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kushindwa kuwa watunzaji bora wa mazingira ambayo amewakabidhi kuyatunza. Hii ni barua iliyoandikwa na Baba Mtakatifu tarehe 9 Novemba 2021 na kuwasilishwa kwa watu wa Mungu nchini Scotland na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Balozi wa Vatican nchini Uingereza.

Itakumbukwa kwamba, hii ilikuwa ni Sikukuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, kielelezo cha ushirika wa imani na upendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Scotland kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Anawasalimia na kuwatakia wote heri na baraka kutoka katika “sakafu ya moyo wake” bila kuwasahau waathirika wa ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkumbuka na kuwakumbuka Maaskofu wote katika urika wao kwa ajili ya huduma ya Injili, ili kwa pamoja waendeleze mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa. Katika nyakati hizi zenye changamoto nyingi Wakristo nchini Scotland wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, ili nguvu ya Injili iweze kuleta mwanga angavu na matumaini katika mchakato wa ujenzi haki, udugu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya kiroho na kimwili. Mwishoni mwa barua yake, anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Scotland uwepo wake kwa njia ya sala.

Papa Scotland
11 November 2021, 14:48