Tafuta

Jukwaa la IV la Amani Paris Ufaransa kwa Mwaka 2021: Papa Francisko: Kujenga na kudumisha amani, utawala bora, mapambano dhidi ya UVIKO-19 na Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jukwaa la IV la Amani Paris Ufaransa kwa Mwaka 2021: Papa Francisko: Kujenga na kudumisha amani, utawala bora, mapambano dhidi ya UVIKO-19 na Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. 

Jukwaa la IV la Amani Paris, 2021: Ujumbe wa Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Jukwaa la IV la Amani Paris, Ufaransa kwa Mwaka 2021 anawataka wajumbe wajizatiti katika kukuza na kudumisha amani, utawala bora pamoja na kujielekeza katika mchakato wa maisha bora kwa wote pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jukwaa la IV la Amani Paris, Ufaransa kwa Mwaka 2021 “Forum de Paris sur la Paix” au “The 4th Paris Peace Forum” ambalo Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU ni mdau wake mkubwa, pamoja na mambo mengine linapania kutoa kipaumbele cha pekee kwa utawala bora katika ajenda zake za Kimataifa. Hili ni Jukwaa ambalo wadau mbalimbali wa maendeleo wanajadiliana katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kupata suluhu katika mambo msingi matatu: suluhu ya changamoto za Kimataifa; majadiliano pamoja na uvumbuzi. Kati ya mada ambazo zinachambuliwa na wajumbe wa Jukwaa la IV la Amani la Paris kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 13 Novemba 2021 ni pamoja na: Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika misingi ya utawala bora pamoja na Maboresho ya Ulimwengu wa Kidigitali. Wajumbe wamejikita katika mapambano dhidi ya habari za kughushi na hatari zinazoisonga tasnia ya mawasiliano ya jamii. Wamekazia umuhimu wa kulinda na kutunza maeneo ya kiraia hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Umefika wakati wa kuboresha usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume; mchakato wa kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa kati ya Nchi za Kusini na Kaskazini sanjari na mabadiliko ya Ubepari mintarafu athari za kiuchumi!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Jukwaa hili anawataka wajizatiti katika kukuza na kudumisha amani, utawala bora pamoja na kujielekeza katika mchakato wa maisha bora kwa wote pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu amezungumzia juu ya uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na utamaduni wa utupaji pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Mchakato wa kurejea tena katika maisha ya kawaida si rahisi sana kutokana na mfumo wa uchumi uliokuwa unawakumbatia matajiri wachache wakati mamilioni ya watu wakiteseka kupata mahitaji yao msingi, ili wapate kuishi maisha yenye hadhi na yanayozingatia utu wa binadamu. Kuna maafa makubwa ambayo yamesababishwa na vita, kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii. Kwa sasa kumeibuka kwa kasi kubwa tabia ya baadhi ya Mataifa kudhani kwamba, yanajitosheleza, utaifa uliokithiri, tabia ya kujilinda, ubinafsi na kujitenga na katika mwelekeo huu, maskini wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, hali ambayo haitoi matumaini kwa siku za usoni hata kidogo!

Katika ulimwengu wa utandawazi, watu wanapaswa kutambua kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe, kumbe, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana kwa kufanya kazi kwa pamoja, ili kudumisha amani na kuendelea kujikita zaidi katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa wito kwa Mataifa ambayo bado hayajaridhia Mkataba huu, kushiriki na kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba, dunia inakuwa ni mahali pa salama pasi na silaha za nyuklia, ili kuchangia katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaohitajika sana kwa wakati huu. Amani ya kweli inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru sanjari na kuaminiana. Soko huria la silaha ni changamoto kubwa katika kukuza na kudumisha misingi ya amani na kuendeleza matumaini kwa watu wa Mungu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaweza kusaidia kuamsha matumaini ya kweli miongoni mwa watu wa Mungu, ili kupambana na ukosefu wa haki, vita na kinzani kwa sababu haya si malengo ya binadamu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inawajengea watu wa Mungu matumaini yanayowajibisha. Hii ni changamoto ya kukubali kwamba, janga hili linaweza kuwa fursa makini ya toba, wongofu wa ndani, mabadiliko sanjari na mageuzi makubwa katika mitindo ya maisha sanjari na mifumo ya uchumi na kijamii. Matumaini yanayowajibisha yanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kutafuta suluhu makini na yanawapatia ujasiri wa kuendelea na safari ya kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hifadhi na huduma kwa maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Huu ni muda muafaka wa kufanya maboresho katika ulimwengu, kwa kufanya maamuzi mazito pamoja na kujielekeza katika maendeleo, ustawi na amani.

Sera na mifumo ya uchumi iwe ni ile inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ilinde na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote na siasa zijielekeze zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa kuganga na kutibu donda hili kwa familia ya Mungu. Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe wake kwa kusema, “BWANA asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo.” Yer 6:16.

Jukwaa la Amani Paris
12 November 2021, 15:17