Tafuta

Chama cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro "Pro Petri Sede" Kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya utume wake nchini Ubelgiji. Chama cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro "Pro Petri Sede" Kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya utume wake nchini Ubelgiji. 

Jubilei ya Miaka 150 ya Chama Cha Kitume Cha Mtakatifu Petro: Huduma!

Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede", tarehe 27 Novemba 2021 kinaadhimisha kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake Jimbo kuu la Brussels nchini Ubelgiji. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Dominique Mamberti, kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Ni katika muktadha huu, Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede", tarehe 27 Novemba 2021 kinaadhimisha kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake Jimbo kuu la Brussels nchini Ubelgiji. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya yatakayofanyika kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Koekelberg, Jimbo kuu la Brussels.

Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kumeibuka ukosefu mkubwa wa haki jamii zinazotokana na rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma, changamoto kubwa kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanajikita katika kupambana na magonjwa haya ya kijamii, kwa kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha haki, tabia ya kuaminiana, uaminifu, ukweli na uwazi. Hii ni dawa mchunguti katika mapambano dhidi ya tabia ya uchoyo na mwelekeo wa ubinafsi, kiasi cha kufunika ukweli. Jubilei ya Miaka 150 Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede" ni kielelezo cha huduma ya Injili ya upendo ambayo imetangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhidi ya uchoyo na ubinafsi. Baba Mtakatifu anawapongeza na anapenda kutumia fursa hii kuwatia shime ya kusonga mbele kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu!

Katika maadhimisho haya, Kardinali Dominique Mamberti ataambatana na Askofu mkuu mstaafu Augustin Kasujja aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Ubelgiji. Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi cha miaka 40 ya huduma yake kama Kasisi, Kardinali Dominique Mamberti kwa hakika amekuwa ni shuhuda wa imani na mapendo. Ataongoza Ibada ya Misa na kutoa mwaliko kwa waamini kupyaisha tena na tena ari na mwamko wa kitume unaobubujika kutoka katika imani, upendo na ibada kwa ajili ya sifa na ukuu wa Mungu, ambaye huruma yake yadumu milele. Baba Mtakatifu anahitimisha barua ya uteuzi wa Kardinali Dominique Mamberti kama mwakilishi wake kwenye Jubilei ya Miaka 150 Chama Cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede” kwa kumweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mwenyeheri Papa Pio wa IX.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 24 Februari 2020, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na wanachama wa chama hiki na alitumia fursa hiyo kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa kwake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomsibu mwanadamu na mazingira yake. Kuna kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita, kwa kukosa makazi bora, umaskini pamoja na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kusimama kidete ili kusitisha kabisa tabia ya unyonyaji wanayofanyiwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Umefika wakati wa kuondokana na vita, kinzani na nyanyaso mbalimbali zinazopelekea makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi na makazi yao. Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kwa kujizatiti katika wongofu wa kiikojia. Maisha ya wanachama wa Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika moyo wa ukarimu kwa kwa kuwajali wengine.

Huu ni mwaliko wa kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo, tabia ya kutowajali na kuguswa na mahangaiko ya jirani; hali inayohatarisha amani kati ya watu wa Mataifa pamoja na mazingira. Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kujizatiti kikamilifu na kujikita zaidi katika imani ili waweze kuwa kweli ni miale ya moto wa matumaini kwa watu wa nyakati hizi. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro Mtume, wanachama hawa wanapaswa kuwa na ujasiri na uthubutu wa kuwashirikisha wengine upendo wa Kristo Yesu uliofunuliwa kwao.

Jubilei ya Miaka 150
25 November 2021, 15:58