Tafuta

Askofu mkuu Dieudonné Datonou Balozi wa Vatican nchini Burundi aliyetangazwa mubashara na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Septemba 2021, tukio la kihistoria! Askofu mkuu Dieudonné Datonou Balozi wa Vatican nchini Burundi aliyetangazwa mubashara na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Septemba 2021, tukio la kihistoria! 

Askofu Mkuu Dieudonné Datonou Aliyetangazwa mubashara na Papa Wakati wa Hija ya Kitume!

Askofu mkuu mteule Dieudonné Datonou mwenye umri wa miaka 57 alikuwa ni mratibu wa hija za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Huu ni uteuzi uliotangazwa moja kwa moja na Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Hungaria tarehe 12 Septemba 2021. Ameratibu hija za Papa nchini Iraq, Hungaria na Slovakia, muhimu sana kwa utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amemteua Monsinyo Dieudonné Datonou kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Burundi na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Dieudonné Datonou mwenye umri wa miaka 57 alikuwa ni mratibu wa hija za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Huu ni uteuzi uliotangazwa moja kwa moja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Hungaria tarehe 12 Septemba 2021. Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yalinogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kongamano hili pamoja na mambo mengine lilipania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni ili kupyaisha na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Hungaria.

Askofu mkuu mteule Dieudonné Datonou ndiye aliye ratibu pia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia iliyonogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu.” Aliratibu pia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq. Baba Mtakatifu Francisko alisema, hija yake ya kitume ya 33 kimataifa nchini Iraq ni kati ya hija ambazo zilikuwa hatari sana katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alitumia muda mrefu kusali na kutafakari. Akapima madhara na faida yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Iraq. Akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba ulinzi na usalama kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, akapiga moyo konde na kuamua kwamba, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 angefanya hija ya kitume nchini Iraq kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu amekuwemo nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Alipata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.

Hivi ndivyo Askofu mkuu mteule Dieudonné Datonou alivyohitimisha utume wake mjini Vatican, safari aliyoinza tarehe Mosi Julai 1995. Tayari alikwisha kufanya utume wake nchini Angola, Equador, Cameroon, Iran, India, El Salvador na baadaye kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Askofu mkuu mteule Dieudonné Datonou alizaliwa tarehe 3 Machi 1962 huko Dèkanmè, nchini Benin. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Desemba 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Cotonou, nchini Benin. Tarehe 7 Oktoba 2021 akateuliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Burundi sanjari na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Historia inaonesha kwamba, tukio kama hili liliwahi kufanywa na Mtakatifu Paulo VI tarehe 5 Januari 1964 alimpoteua Monsinyo Jaques Martin kuwa Askofu baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume iliyoacha historia ya pekee katika maisha na utume wake Nchi Takatifu. Huo ukawa ni mwanzo wa hija za kitume zilizoanza kutekelezwa na Mapapa baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Burundi
03 November 2021, 16:59