Tafuta

Tarehe 12 Oktoba 1931 Sanamu ya Kristo Mfalme ilisimikwa kwenye kilele cha Mlima wa Corvado. Ujumbe wa Papa: Ujenzi wa udugu wa kibinada,u, upatanisho na mafao ya wengi. Tarehe 12 Oktoba 1931 Sanamu ya Kristo Mfalme ilisimikwa kwenye kilele cha Mlima wa Corvado. Ujumbe wa Papa: Ujenzi wa udugu wa kibinada,u, upatanisho na mafao ya wengi. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Jiji la Rio De Janeiro: Upatanisho!

Papa Francisko anakazia: Umuhimu wa majadiliano katika ukweli, ili kuondokana na uchoyo, ubinafsi, mzunguko wa vurugu na mipasuko ya kijamii. Jamii ijenge utamaduni wa majadiliano kati ya kizazi kimoja hadi kingine; majadiliano kati ya watu. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 90 tangu kuzinduliwa kwa Sanamu ya Kristo Mfalme nchini Brazil ni fursa ya kupyaisha ukarimu na upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sanamu ya Kristo Mfalme ilizinduliwa tarehe 12 Oktoba 1931 na Rais Getúlio Vargas wa Brazil. Imegota miaka 90 tangu kuzinduliwa kwa sanamu hii ambayo imewekwa kwenye kilele cha Mlima Corvado. Mwanga wake ulitengenezwa na Guglielmo Marcon. Hii ilikuwa ni alama ya mwanga wa Kristo Yesu kwa walimwengu; kielelezo cha neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 90 tangu kuzinduliwa kwa Sanamu ya Kristo Mfalme huko Brazil amemtumia ujumbe wa matashi mema Kardinali Orani João Tempesta O.Cist. Askofu mkuu wa Jimbo kuu la “San Sebastian do Rio de Janeiro”.

Ujumbe huu ambao umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anakazia mwaliko wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upatanisho na msamaha wa kweli kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Brazil. Maadhimisho haya yawe ni kikolezo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, hususan na wale wote wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Kila mtu anao uwezo wa kushiriki katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kuangalia kiwango chake cha elimu wala hali yake ya kiuchumi, jambo la msingi ni kukunjua mikono kuonesha upendo na ukarimu wa udugu wa kibinadamu, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na uchoyo, ubinafsi, mzunguko wa vurugu na mipasuko ya kijamii. Jamii ijenge utamaduni wa majadiliano kati ya kizazi kimoja hadi kingine; majadiliano kati ya watu. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 90 tangu kuzinduliwa kwa Sanamu ya Kristo Mfalme nchini Brazil ni fursa ya kupyaisha ukarimu na upendo miongoni mwa watu wa Mungu pamoja na kushikamana na Kristo Yesu ambaye anatembea kati pamoja nao. Ni wakati muafaka wa kujenga ujirani mwema. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Mwishoni amewapatia baraka zake za kitume kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Aparecida, Msimamizi wa Brazil.

Jubilei Brazil

 

14 October 2021, 16:40