Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Oktoba 2021 alizindua safari ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: 2021-2023 inayoongozwa na kauli mbiu: Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Oktoba 2021 alizindua safari ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: 2021-2023 inayoongozwa na kauli mbiu: Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume! 

Sinodi ya Maaskofu 2021-2023: Papa Francisko Hotuba Elekezi

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023. Papa Francisko alikazia ushirika au umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa unaotekelezwa na kila mbatizwa, kama kielelezo cha imani tendaji! Ni wakati wa kuondokana na nadharia, mtazamo mgando, ili kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja, daima likiwa karibu zaidi na watu! Kanisa linapaswa kutenda kadiri ya ukaribu wa Mungu!

Na Timu ya Wafasiri kutoka Jimbo kuu la Tabora, Tabora, Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa kwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2023, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Alikazia ushirika au umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa unaotekelezwa na kila mbatizwa, kama kielelezo cha imani tendaji! Ni wakati wa kuondokana na nadharia, mtazamo mgando, ili kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja, daima likiwa karibu zaidi na watu! Kanisa linapaswa kutenda kadiri ya ukaribu wa Mungu, upole na huruma! Ndugu wapendwa, Asanteni kufika hapa kwa ajili ya ufunguzi wa Sinodi. Mmefika kutoka sehemu mbalimbali na makanisa mbalimbali, kila mtu akibeba katika moyo wake maswali na matumaini. Natumaini kabisa kwamba Roho Mtakatifu atatuongoza na kutupatia neema ya kusonga mbele pamoja, kusikilizana na kuanzisha upya mwendo wa kung’amua ishara za nyakati zetu tukiwa imara pamoja na changamoto na matamanio ya mwanadamu wa leo. Lazima tuelewe kwamba Sinodi siyo bunge. Sinodi siyo utafiti wa maoni ya watu. Sinodi ni wasaa wa Kanisa na anayetenda kazi katika Sinodi ni Roho Mtakatifu. Kama hakuna Roho Mtakatifu, hakutakuwa na Sinodi.

Tuiishi sinodi hii kwa moyo wa sala ambayo kwa dhati yote Kristo Yesu alimwelekea Baba kwa ajili ya walio wake “ili wote wawe na umoja” (Yn 17:21). Katika hilo tumeitwa kuwa na ; umoja, mshikamano, na udugu unaotokana na kujisikia kukumbatiwa na upendo wa Mungu. Sote pasipo ubaguzi, na kwetu wachungaji kwa namna ya pekee, kama alivyowahi kuandika Mt. Cypriano “tunapaswa kuzingatia na kukuza kwa bidii huu umoja, hasa sisi maaskofu ambao ni viongozikatika Kanisa, ili kutoa ushuhuda kwamba hata uaskofu wenyewe ni mmoja na usiogawanyika”. Hivyo katika taifa moja la Mungu tunatembea pamoja, ili kuonja pamoja ukweli kwamba Kanisa linapokea na kuishi zawadi ya umoja na kuifungukia sauti ya Roho Mtakatifu. Maneno msingi matatu katika Sinodi ni: Ushirika/umoja (communion), Ushiriki (participation) na Utume (mission). Umoja na Utume kitaalimungu hueleza fumbo la Kanisa ambalo yafaa kulikumbuka daima. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican umefafanua kwamba Ushirika unapambanua asili yenyewe ya Kanisa na wakati huo huo unatamka kwamba Kanisa limepokea “utume wa kuutangaza ufalme wa Kristo na wa Mungu na kuusimika kati ya mataifa. (Lumen Gentium , 5).

Maneno mawili ambayo kwayo Kanisa linatafakari na kuiga maisha ya Utatu Mtakatifu, fumbo la  uwazi na ushirika wa ndani na hata nje chemchemi ya utume. Baada ya muda wa tafakuri ya mafundisho bayana, kitaalimungu na kiuchungaji ambayo ni sifa ya jumla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Paulo wa VI Papa alitaka kuyafupisha kwa maneno haya mawili;Ushirika na Utume-“kaulimbiu ya Mtaguso”. Alisema kwamba mlolongo wa jumla ulikuwa ni “Ushirika; yaani, msukumo na utimilifu wa ndani katika neema, katika ukweli, katika ushirikiano wa utume, yaani juhudi za kitume kuelekea ulimwengu wa leo”.  Na namna hii si uhamashaji wa kibabe wa masuala ya dini. Katika hitimisho la Sinodi ya Maaskofu ya mwaka 1985, miaka ishirini baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kusisitiza kwamba asili ya Kanisa ni Ushirika wa Kiroho: katika hilo huchipuka utume wake wa kuwa ishara ya muunganiko wa ndani wa familia ya wanadamu na Mungu. Alikazia kusema “inafaa kwamba katika Kanisa ziadhimishwe Sinodi za kawaida na kadiri inavyofaa hata zisizo za kawaida” na ili kuzaa matunda zinapaswa kuandaliwa vizuri; “Yafaa katika makanisa mahalia watu wafanye kazi ya kutosha ya maandalizi pamoja na ushiriki wa wote”.

Na hivyo, Neno la tatu ni Ushiriki. Ushirika na utume vina hatari ya kubaki katika nadharia kama hakuna juhudi thabiti za kuweka utaratibu halisi ya kisinodi katika kutembea pamoja na kufanya mambo pamoja kila mmoja akivaa uhusika. Nipende kusema, kuadhimisha Sinodi ni jambo jema la kupendeza na la muhimu. Lakini Sinodi itakuwa na manufaa ya kweli kama itakuwa kielelezo cha uwepo wa Kanisa na utendaji wake unaofumbatwa na ushiriki wa kweli wa watu wote. Hayo yote hayafanyiki kwa ajili ya mahitaji ya kimuundo, bali imani. Ushiriki ni tamanio la imani tuliyopokea katika Ubatizo. Mtume Paulo anasema, “sisi sote tumebatizwa ubatizo mmoja katika mwili mmoja” (1Kor12:13). Sehemu ya kuanzia katika Kanisa ni ubatizo na si kitu kingine. Hapo ipo chemchemi ya maisha yetu na usawa wa hadhi ya watoto wa Mungu licha ya tofauti za karama na huduma. Kwa hiyo, sote tunaitwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Kama hakuna ushiriki halisi wa watu wote wa Mungu, hotuba juu ya ushirika zina hatari ya kubaki katika nia tu. Katika kipengele hiki tumepiga hatua, lakini bado miongoni mwetu wapo watendaji wa shughuli za kichungaji, mifumo na makundi ambayo wanapata taabu na mateso katika kushirikisha Jimbo, Parokia na hasa wanawake ambao mara nyingi huachwa pembeni. Ushiriki wa watu wote ni suala la juhudi ambalo halikwepeki. Wabatizwa wote kitambulisho chetu ni ubatizo.

Wakati Sinodi ikitupatia wasaa mzuri wa wongofu wa kichungaji katika mtazamo wa kimisionari na kiekumene, hatari pia haziko mbali. Nitazitaja hatari tatu. 1.Urasimu. Inawezekana watu wakaifanya Sinodi kuwa tukio lisilo la kawaida, kama tu ukuta fulani wa Kanisa bila kuugusa kamwe. Lakini Sinodi ni mwendo wa pamoja wa mang’amuzi ya kiroho ambayo si kwamba tunafanya ili kujionesha wenyewe kwa watu bali kwa ajili ya kukuza ushirikiano wetu na kazi ya Mungu katika historia. Kumbe tunapoongelea Kanisa la Kisinodi hatupendi kujiridhisha kwa  mitindo pekee bali kwa majukumu halisi, vitendea kazi na mazingira yanayochochea majadiliano na mchangamano wa watu wa Mungu, hususan, baina ya mapadre na waamini. Kwa nini nasisitiza hili? Ni kwa sababu mara nyingi kuna hali fulani ya werevu miongoni mwa Mapadre ambao huwafanya wajitenge mbali na waamini. Mwishowe padre anakuwa bwana mkubwa na siyo tena mchungaji wa Kanisa linalosonga mbele. Hili huhitaji mabadiliko katika mtazamo mbovu juu ya Kanisa, utume wa kipadre, nafasi ya walei, wajibu wa kikanisa, nafasi za uongozi na kadhalika.

2.Usomi-nadharia. Uhalisia huenda upande mmoja na sisi na tafakari zetu tunakwenda upande kinzani. Hali hii huweza kuifanya Sinodi kuwa aina fulani ya kundi la msomo, pamoja na mada za kisomi ambazo ninadharia tu juu ya matatizo ya Kanisa na ulimwengu. Aina fulani ya hotuba na semina za kidunia. Mwishowe, humalizia kwa kukuza umbali baina ya wanadamu na Mungu. 3. Mtazamo Mgando. Neno “tumelizoea kufanya kwa namna hii.” (Evangelii Gaudium, 33) ni sumu dhidi ya maisha ya Kanisa. Tumezoea kufanya hivi-afadhali tusifanye mabadiliko! Anayeangukia katika mtazamo huo hata pasipo kujitambua anafanya kosa kubwa la kutotilia maanani ishara za nyakati zetu. Hatari yake ni kwamba watu hutumia suluhu za kizamani kutatua matatizo mapya. Mahusiano ya viraka vya zamani katika kitambaa kipya (Mt. 9:16). Kwa hivyo , inafaa kwamba sinodi iwe mchakato wa kufanyika upya, kuhusisha wengine hasa kutoka ngazi ya chini ya Kanisa mahalia ili kukuza namna ya ushirika na ushiriki wa maisha na utume wa Kanisa. Tuuishi wakati huu wa Sinodi kama wasaa na mwema wa neema kwa kusikilizana na kutafakari pamoja. Wakati wa neema ambao unaturuhusu kuchota huchota walau nafasi hizi tatu muhimu:

a) Kutembea pamoja sio mara kadhaa tu bali kimfumo kabisa  tukielekea kuwa Kanisa la Kisinodi. Mahali wazi ambapo kila mmoja atajisikia nyumbani na ana nafasi ya kushiriki. b) Sinodi inatufanya pia tuwe Kanisa linalosikiliza. Kutufanya kuchukua muda kutathimini wasiwasi wetu wa kichungaji na kuwa tayari kusikiliza. Kumsikiliza Roho katika maabudu na sala. Leo hii tuna changamoto kubwa sana kusali na kufanya maabudu! Wengi wameshapoteza siyo tu tabia ya kuabudu bali pia hawaelewi maana yake. Kuwasikiliza ndugu zetu katika misukosuko na matumaini yao ya imani, upyaisho wa uchungaji na ishara nyinginezo katika mazingira yetu. c) Sinodi ni nafasi ya kuwa Kanisa lililo karibu na watu. Tukirudi daima katika namna ya utendaji wa Mungu. Namna ya ukaribu, upole, huruma na mapendo. Daima Mungu ametutendea namna hii. Kama kweli hatutaifikia namna hii ya kuwa Kanisa la huruma, upole na ukaribu hatutakuwa Kanisa la Bwana. Na hayo si kwa maneno tu bali kwa uwepo, unaoanzisha mfungamano ya kirafiki na jamii na ulimwengu mzima. Kanisa ambalo halijitengi na maisha, bali linabeba mizigo ya unyonge na ufukara wa nyakati zetu, likiponya vidonda na kuhuisha mioyo ya walioumizwa. Tusisahau namna ya Mungu ya ukaribu, upole na huruma.

Wapendwa, Sinodi iwe wakati uliojaa Roho Mtakatifu. Tunamwitaji Roho Mtakatifu, hewa mpya ya Mungu ambayo huweka huru kila kilichofungwa, huhuisha kila kilichokufa, hufungua mafundo, husambaza furaha. Roho Mtakatifu ndiyeanayetuongoza kule anakotaka Mungu na siyo kule zinakotupeleka fikra, mawazo na vionjo vyetu. Padre Congar alitukumbusha “Hakuna haja ya kutengeneza Kanisa lingine, inatakiwa kutengeneza Kanisa lililo tofauti.” Na hii ni changamoto Kwa ajili ya kanisa lililo tofauti, lililo wazi kwa ajili ya mabadiliko anayotunulia Mungu, tumwite kwa nguvu zaidi Roho Mtakatifu na kwa unyenyekevu tumsikilize, tukitembea pamoja naye, mwumbaji wa ushirika na utume. tunahitaji ujasiri. Njoo Roho Mtakatifu, wewe unayewasha ndimi mpyauweke midomoni mwetu maneno mapya ya uzima, tulinde dhidi kuwa Kanisa-Makumbusho, zuri lakini bubu, lenye historia ndefu na mustakabali mfupi. Njoo kati yetu ili katika Sinodi tusiachane nyuma, kusipuuze unabii na kubaki katika mabishano yasiyo na tija. Njoo Roho Mtakatifu wa Upendo, fungua mioyo yetu kusikiliza. Njoo Roho wa Utakatifu, pyaisha taifa takatifu la Mungu. Njoo Roho Muumbaji, uufanye upya uso wa nchi. AMINA

18 October 2021, 09:55