Tafuta

Jukwaa la Chakula Duniani 2021 "World Food Forum" Ujumbe wa Papa Francisko kwa Dk. Qu Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa FAO. Jukwaa la Chakula Duniani 2021 "World Food Forum" Ujumbe wa Papa Francisko kwa Dk. Qu Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa FAO. 

Jukwaa la Chakula Duniani: Vijana na Mapambano Dhidi ya Baa la Njaa Duniani

Papa anaipongeza FAO kwa kuwahusisha vijana katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Hiki ni kizazi cha vijana wenye kiu ya haki, wanaoweza kutumia kipaji cha ubunifu, nguvu na uwezo wao kukabiliana na baa la njaa duniani. Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni changamoto inayoitaka familia ya binadamu kushikamana kidugu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni dhamana ya kimaadili kwa Kanisa la Kiulimwengu. Chakula na maji safi na salama ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula na Maji, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao kama sehemu ya haki msingi za binadamu pasi na ubaguzi. Yesu mwenyewe anasema kwamba, Yeye ni mkate wa uzima wa milele na anapenda kuwaalika wote wenye njaa na kiu kujongea mbele yake ili aweze kuwalisha na kuwanywesha. Matendo haya ya huruma kimwili, yanajenga uhusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma! Athari za mabadiliko ya tabianchi yaani: ukame wa kutisha, mafuriko, majanga asilia, vita, ghasia, kinzani na machafuko mbalimbali, ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kusababisha ongezeko kubwa la baa la njaa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na umaskini duniani.

Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kuweza kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Ili kufanikisha malengo haya, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo, kwa kuwawezesha pia wakulima wadogo wadogo wanaochangia uhakika wa usalama wa chakula kwa familia zao pamoja na kujipatia kipato cha kuweza kuboresha hali ya maisha. Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO linabainisha kwamba, hata kabla ya kuzuka na hatimaye kupamba moto kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kumesababisha ongezeko la watu wanaosiginwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Takwimu zinaonesha kwamba,  kuna zaidi ya watu milioni 700 wanaoshambuliwa na baa la njaa duniani. Changamoto mamboleo ni uhakika na usalama wa chakula duniani, hali ambayo inapaswa kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maboresho ya maisha ya watu duniani.

FAO inapenda kuwekeza zaidi katika teknolojia rafiki, utunzaji bora wa takwimu, utawala bora pamoja na maboresho ya taasisi mbalimbali zitakazosaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Kuanzia tarehe 1-5 Oktoba 2021 FAO inaendesha Jukwaa la Chakula Duniani, linalowajumuisha vijana wa kizazi kipya, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na baa la njaa duniani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia  Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO ujumbe maalum. Anampongeza kwa namna ya pekee kabisa kwa kuwahusisha vijana wa kizazi kipya katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Hiki ni kizazi cha vijana wenye kiu ya haki, wanaoweza kutumia kipaji cha ubunifu, nguvu na uwezo wao kukabiliana na baa la njaa duniani. Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni changamoto inayoitaka familia ya binadamu kushikamana ili kukabiliana na majanga yanayomwandama mwanadamu. Vijana wanapaswa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa duniani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwezi Septemba 2021 huko New York, nchini Marekani, Umoja wa Mataifa umefanya mkutano kuhusu: Mifumo Endelevu ya Chakula mintarafu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameendelea kusababisha uharibifu kwa mazingira na ukame kwa maisha ya kiroho. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu, lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu unaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua binadamu. Hii ni kashfa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Baba Mtakatifu anasema hii ni ahadi kwa familia ya binadamu na kwamba, vijana wa kizazi kipya wanaoshiriki katika Jukwaa la Chakula Duniani wasiogope na wawe na maamuzi thabiti katika kutekeleza ndoto zao kwa ajili ya maisha bora zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni.

Vijana waondokane na ndoto za mchana zilizoibuliwa kutokana na madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, tayari kujikita katika mshikamano, ubunifu na ushupavu wa moyo. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliofanya maamuzi hivi karibuni, kamwe wasiwaangushe vijana wa kizazi kipya, wawe tayari kuwasikiliza na kutekeleza matamanio halali ya nyoyo zao, kwani wao ndio walengwa wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawataka washiriki kamwe wasikate tamaa, bali wasimame imara huku wakiwa wameunganika ili kuhakikisha kwamba, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha vinapewa kisogo!

Papa Vijana na Chakula
01 October 2021, 15:55