Tafuta

Mwenyeheri Sandra Sabattini alisimika maisha yake katika Injili ya upendo, maisha ya sala na huduma kwa maskini! Mwenyeheri Sandra Sabattini alisimika maisha yake katika Injili ya upendo, maisha ya sala na huduma kwa maskini! 

Mwenyeheri Alessandra Sabattini: Injili ya Upendo, Sala na Huduma!

Mwenyeheri Alessandra Sabattini, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 22. Katika ujana wake, asimika maisha yake katika Injili ya upendo na maisha ya sala! Akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Tarehe 24 Oktoba 2021 ametangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Mwenyeheri! Changamoto kwa vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika, tarehe 24 Oktoba 2021 amemkumbuka Mwenyeheri Sr Lucia wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri Jumamosi tarehe 23 Oktoba 2021. Ni Mtawa wa Shirika Watumishi wa Upendo “Ancelle della Carita”. Ni mtawa ambaye alisadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa jirani, lakini mwishoni, akashambuliwa na magonjwa, lakini bado alibaki imara na thabiti moyoni mwake! Mwingine ni Mwenyeheri Alessandra Sabattini, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 22. Katika ujana wake, asimika maisha yake katika Injili ya upendo na maisha ya sala! Akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kardinali Marcello Semeraro Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Alessandra Sabattini kwa ni Mwenyeheri. Ibada ya Misa takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Columba, Jimbo Katoliki la Rimini, Italia.

Mwenyeheri Sandra alikuwa na upendo wa ajabu kwa Mwenyezi Mungu asili ya wema wote na kwa maskini. Alitamani kushirikiana nao ili kuweza kubeba mgizo wa mateso na mahangaiko yao ya ndani. Alipenda kumwilisha Utenzi wa Upendo katika maisha na utume wake. Muhtasari wa upendo unadadavuliwa kwa kina na mapana na Mtume Paulo katika utenzi wa upendo kwenye Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho Sura ya 13: 1-13. Kardinali Marcello Semeraro katika mahubiri yake, amefafanua utenzi wa upendo mintarafu maisha ya Mwenyeheri Alessandra Sabattini. Ari na mwamko wa huduma ya upendo, ilikuwa ni chemchemi ya maisha yake ya kiroho iliyokuwa inapata asili na chanzo chake kutoka kwenye upendo wa Mungu. Alitamani kuwashirikisha wengine, karama na mapaji aliyokuwa amejaliwa na Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha yake ya kila siku pasi na makuu. Lengo lake msingi lilikuwa ni kuwashirikisha wengine Injili ya upendo wa Mungu. Huduma kwa maskini, ilikuwa ni ngazi ya kupandia utakatifu wa maisha.

Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha maskini upendo wao huko huko waliko na wala wasisubiri maskini kuwafuata majumbani mwao ili kuomba msaada wa hali na mali. Msaada na huduma kwa maskini uoneshwe kwenye hospitali, nyumba za watoto yatima, kambi za wakimbizi na wahamiaji na kwa maskini wanaotamani kuonja faraja na upendo kutoka kwa jirani zao. Kupenda maana yake ni kuhisi mahitaji msingi ya jirani yako, tayari kumsaidia kubeba mateso na mahangaiko yake kwa unyenyekevu mkuu. Mwenyeheri Alessandra Sabattini alipenda kuhakikisha kwamba, anatumia vyema rasilimali muda kwa ajili ya huduma kwa maskini na vijana waliokuwa wanahitaji zaidi huduma yake. Alitamani kuwa ni shuhuda na chombo cha huduma ya upendo. Ili kufahamu lugha ya upendo, mwamini hana budi kupenda kwa dhati

Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Alessandra Sabattini alizaliwa tarehe 19 Agosti 1961 huko Riccione nchini Italia. Ni mwamini mlei na mfuasi wa maisha ya kiroho wa Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi, Muasisi wa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII iliyoanzishwa kunako mwaka 1968. Jumuiya hii imeenea katika nchi 42, Tanzania ikiwemo na imekuwa ni kama hospitali katika uwanja wa mapambano sehemu mbalimbali za dunia. Mwenyeheri Alessandra Sabattini anayejulikana na wengi kama Sandra, tangu mwaka 1974 alionesha ari na mwamko wa shughuli za kimisionari hususan kuwasaidia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini, ujinga na maradhi. Alipenda kuwasaidia vijana walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na walemavu!

Tarehe 29 Aprili 1984 aligonjwa na gari akiwa njiani kwenda kutoa huduma. Jitihada za kuokoa maisha yake, ziligonga mwamba na hatimaye, alifariki dunia tarehe 2 Mei 1984. Ni mwamini mlei, aliyependa kutangaza Injili ya upendo kwa maskini! Alirutubisha maisha yake ya kiroho kwa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, lakini zaidi kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, iliyompatia nguvu ya kugeuka kuwa ni Ekaristi kwa jirani na maskini waliohitaji zaidi huduma yake. Alitambua kwamba, ngazi ya kuweza kwenda mbinguni ilikuwa ni kwa njia ya sala. Tarehe 7 Machi 2018, Kanisa likatambua karama yake ya ushujaa, baada ya mtu mwenye umri wa miaka 40 aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa Saratani mbaya, alipopona ghafla kwa maombezi ya Mwenyeheri Alessandra Sabattini kunako tarehe 3 Septemba 2007. Muujiza huu ni matokeo ya sala ya pamoja ya Jumuiya ya Papa Yohane XXIII. Mgonjwa huyo akafanyiwa uchunguzi wa kina kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2014 wala hakuwa tena na chembe za Ugonjwa wa Saratani mwili wake. Tarehe 2 Oktoba 2019 Baba Mtakatifu Francisko akaridhia kwamba, jina lake liandikwe kwenye Orodha ya Wenyeheri wa Kanisa.

Mwenyeheri Sandra
25 October 2021, 15:13