Tafuta

Papa Francisko akitafakari. Papa Francisko akitafakari. 

Moyo wangu huko vipande. Katika mikono ya Papa kuna barua ya mwathirika wa manyanyaso

Hivi karibuni Papa Francisko alishirikishwa ushuhuda wa kijasiri wa mwathiriwa wa nyanyaso na kapenda Kardinali O’Malley,Rais wa Tume kwa ajili ya Ulinzi wa Watoto aishirikishe kwa mapadre wote na waseminari.Katika kurasa ya barua hiyo kuna uchungu wa kutoweza kuhisi usalama Kanisani, na wito kwa mapadre:“Mmepokea zawadi kubwa mno,muwe wema".

Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.

“Jina langu ni ... (jina limehifadhiwa)na kwa miaka nilinyanyaswa na padre ambaye ningepaswa kumwita 'kaka mdogo’ na mimi nilikuwa “dada yake mdogo”. Katika barua hiyo inaonesha jinsi alivyuumizwa sana, na jeraha kubwa la nyanyaso kutoka kwa padre na ambazo zimewaka muhuri katika  roho ya mwanamke huyo ambaye, hata baada ya miaka mingi bado  anajitahidi kuanza mchakato wa njia ya uponyaji. Hii inajionesha wazi kiasi ambacho kwamba bado anaogopa kuona padre yeyote na hata hawezi kwenda katika Misa.

Onyo kwa makuhani

Katika barua barua iliyoandikwa kwa lugha ya kiitaliano mwathiriwa na kuishirikisha na Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto ni ya kusikitisha lakini wakati huo huo ni ya ujasiri. Papa Francisko baada ya kupokea na kuzisoma kurasa hizi zilizozama kwa uchungu na mateso na macho yake mwenyewe ametaka mapadre wote waweze kuisoma pia, kama kuwa onyo la kitisho ambacho Kanisa linajitahidi kukabiliana nacho kwa sasa. Halafu alimruhusu Rais wa Tume ya Kipapa ya ulinzi wa Watoto ,Kardinali Sean O'Malley, kuweka ushuhuda  huo kwa umma.

O'Malley: sauti ya watu wote waliojeruhiwa

Kwa mujibu wa maandishi ya Askofu  mkuu wa Boston, katika utangulizi mfupi wa barua hiyo  anaandika kuwa: “Katika wakati huu wa upyaishwaji na uongofu wa kichungaji ambao  Kanisa linakabiliwa na kashfa na majeraha ya unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa kwa watoto wengi wa Mungu kila mahali, Baba yetu Mtakatifu amepokea ushuhuda wa kijasiri uliotolewa kwa ajili ya makuhani wote na aliyenusurika. Kwa kushiriki ushuhuda huu, uliotolewa kwetu na mwathiriwa ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu ya kutokujulikana, Baba Mtakatifu Francisko anataka kupokea sauti ya watu wote waliojeruhiwa na kuwaoneesha makuhani wote wanaotangaza Injili, njia inayoongoza huduma halisi ya Mungu kwa ajili ya faida ya wanyonge wote”.

Kwa niaba ya watoto

Manusura huyo anaomba ushindi wa ukweli wa kupendeza na anasema kusimulia kile alichofanua uzoefu pia “kwa niaba ya  Watoto waathiriwa  wengine ... kwa watoto ambao walijeruhiwa sana, ambao utoto wao, usafi na heshima zao zimeibiwa. ..”. Watoto “ambao walisalitiwa na walitumia fursa ya imani yao isiyo na mipaka ... watoto ambao mioyo yao hudunda, wanapumua wanaishi ... lakini waliwaua mara moja (mara mbili, mara zaidi)”. “Mioyo yao imetengenezwa vipande vidogo vya damu. Kanisa ni Mama yangu na inaniuma sana linapojeruhiwa, na wakati linakuwa chafu. Watu wazima ambao walipata uzoefu huu wa unafiki wakiwa watoto hawataweza kuufuta kutoka katika maisha yao. Wanaweza kusahau juu yake kwa muda, kujaribu kusamehe, kujaribu kuishi maisha kamili, lakini makovu yatabaki kwenye roho zao, hayatapotea”. anaandika mwanamke huyo,

Wasiwasi, hofu, shida za baada ya kiwewe

Mwandishi wa barua hiyo hata hivyo hafichi hali mbaya ya maisha ambayo anajikuta nayo kwa sasa, hata baada ya miaka: “Ninajaribu kuishi, kuhisi furaha, lakini kiukweli ni mapambano magumu sana ... Nina shida ya utambulisho wa kujitenga, shida ngumu baada ya kiwewe unyong’onyevu, wasiwasi, hofu ya watu, kuhisi makosa na wakati mwingine  siwezi kulala na ikiwa ninaweza kulala katika hali hiyo, huwa ninaota ndoto mbaya. Wakati mwingine huwa nabadilika, ninapokuwa 'nje', sioni 'hapa' na 'sasa'. Mwili wangu unakumbuka kila mguso wa hali hiyo yote mmoja …. Ninawaogopa makuhani, kuwa karibu nao”, anaendelea kuandika. “Hivi karibuni siwezi kwenda kwenye Misa Takatifu.  Hii inaniuma sana… “. Kanisani ni nafasi takatifu ambayo ilikuwa nyumba yangu ya pili, na, kuhani aliyeninyanyasa, aliniondolea nafasi hii  kwangu. Nina hamu kubwa ya kujisikia salama Kanisani, ili kuweza kutoogopa, lakini mwili wangu, na hisia zinaguswa kwa njia tofauti kabisa”, yanasomeka maandishi hayo, ambayo yanahitimishwa kwa kutoa wito kwa kila kuhani, wa kila rika na kila nchi.

Kulinda Kanisa

“Ninapenda kuwaomba mlinde Kanisa, mwili wa Kristo! Yule ambaye kila kitu kimejaa vidonda na makovu. Tafadhali MSIRUHUSU majeraha hayo yawe ya ndani zaidi na mapya yatokee! Ninyi ni vijana na hodari. MNAITWA! Watu walioitwa na Mungu, kumtumikia Mungu na kwa njia yake kwa watu… Mungu amewaita muwe chombo chake kati ya wanadamu. Mna WAJIBU MKUBWA! Wajibu ambao sio mzigo, bali ni Zawadi! Tafadhali mtende kulingana na mfano wa Yesu ... kwa UNYENYEKEVU na UPENDO! ".

Wito kwa makuhani: kuishi ukweli

Kwa hakika wito huo ni ombi la kusisimua lililosukumwa na silika ya upendo kwa Kanisa kwamba: “Tafadhali visifagiliwe vitu na kuachwa chini ya zulia, kwa sababu hapo vitaanza kunuka,  kuoza na  zulia lenyewe litaoza ... tatambue kwamba ikiwa tunaficha ukweli huu, tunapokaa kimya juu yake, tunaficha uchafu na kwa hivyo tunakuwa nasi washabiki. Ikiwa tunataka kuishi ukweli, hatuwezi kufunga macho yetu! Kuishi katika ukweli ni kuishi kwa mujibu wa Yesu, kuona vitu kupitia macho yake”, barua hiyo inaisisitiza. Kristo hakufumba macho yake mbele ya dhambi na mdhambi lakini aliishi UKWELI kwa UPENDO ... Kwa dhati ukweli wa kupendeza alionesha dhambi na mwenye dhambi. Mwathiriwa huyo amesisitiza kwa mapadre kuwa: “Tafadhali tambueni kwamba mmepokea zawadi kubwa. Zawadi ya kuwa altar Christus aliyefanyika kuwa mwili wa Kristo hapa ulimwenguni. Watu na hasa watoto, hawaoni mtu ndani yenu, lakini Kristo, Yesu, ambaye wanamtumaini bila mipaka. Ni kitu kikubwa na chenye nguvu” lakini pia mdhaifu sana na mwathiriwa. Tafadhali kuweni makuhani wema”, anahitimisha mwathiriwa barua yake ambayo ilimfikia Papa kupitia kwa Rais wa Tume ya Kipapa ya ulinzi wa Watoto, Kardinali Sean O'Malley.

BARUA KWA MAPADRE
18 October 2021, 17:09