Tafuta

Katekesi Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Uhuru wa Kikristo!

Uhuru wa Kikristo ni chachu ya ukombozi ulimwenguni na unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka. Utamadunisho na Fumbo la Umwilisho ni vielelezo vya uhuru wa kweli ambao umeletwa na Yesu! Kiini cha Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni uhuru wa kweli unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia amekwisha kugusia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anakazia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Baba Mtakatifu Francisko amechambua pia kuhusu hatari zinazoweza kuibuka kutokana na utekelezaji wa Torati katika misingi ya uhuru kamili, hali inayoweza kupelekea baadhi ya waamini kuwa wanafiki kwa kuogopa ukweli.

Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, limechapisha Tamko la Pamoja Kuhusu Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki. Hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Tarehe 3 Januari 2021, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kwa pamoja yamefanya kumbukumbu ya miaka 500 tangu Martin Luther alipotengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Kwa pamoja, Makanisa haya yanapenda kutangaza nia ya kufanya hija ya upendo na mshikamano kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja kamili wa Wakristo. Tamko la Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki la tarehe 31 Oktoba 1999 lilikuwa na: Utangulizi, Ujumbe wa Biblia juu ya Kuhesabiwa Haki, Mafundisho ya Kuhesabiwa haki kama suala la kiekumene; Ufahamu na maelezo ya pamoja juu ya kuhesabiwa haki. Tamko lilifafanua kuhusu udhaifu wa binadamu, msamaha wa dhambi na kufanyika wenye haki; kuhesabiwa haki kwa njia ya imani na neema. Lilimwangalia aliyehesabiwa haki kama mtu mkosefu; Sheria na Injili; Uhakikisho wa wokovu; Matendo mema ya mtu aliye hesabiwa haki sanjari na umuhimu na lengo la maafikiano yaliyofikiwa. Baba Mtakatifu katika Katekesi yake, mwishoni, ametafakari kuhusu uhuru wa kweli ambao Kristo Yesu amewakirimia waja wake kama zawadi inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, binadamu amekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti, mwaliko wa kutambua na kutembea katika ukweli na imani!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Oktoba 2021 wakati wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia ametafakari kuhusu: Uhuru wa Kikristo ni chachu ya ukombozi ulimwenguni na unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Utamadunisho wa Injili na Fumbo la Umwilisho ni vielelezo vya uhuru wa kweli ambao umeletwa na Kristo Yesu! Kiini cha Katekesi kuhusu Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni uhuru wa kweli unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa njia hii, watu wamekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Wamekombolewa kwa neema na kwa njia ya upendo inakuwa ni muhtasari wa sheria na maisha mapya ya Kikristo! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, uhuru wa Kikristo unawakumbatia na kuwaambata watu wote kutoka tamaduni mbalimbali na hivyo kuingia katika uhuru wa wana wa Mungu. “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.” Gal 5:6. Upya huu wa mawazo, haukuweza kukubalika kwa urahisi sana, ndiyo maana Mtakatifu Paulo Mtume, alishambuliwa sana. Walimtuhumu kwamba alipendelea kutumia fursa hii ya kichungaji kwa ajili ya kuwafurahisha “watu wote” na hivyo kubeza mambo msingi yaliyokuwa yanabubuhika kutoka katika mapokeo ya dini yake. Mashambulizi dhidi ya upya wa Kiinjili yana historia ndefu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Mtakatifu Paulo Mtume, anajibu shutuma hizi kwa kusema “Maana, sasa Je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.” Gal 1:10. Katika mahubiri yake, kamwe hakutafuta utukufu wa kibinadamu. Mtakatifu Paulo Mtume anaonesha jinsi ambavyo Ufunuo wa Neno la Mungu ulivyogusa undani wa maisha yake kiasi hata cha kuweka kando tamaduni na mapokeo yake ya zamani, ili kupokea upya na usafi wa Injili. Uhuru wa Wakristo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka unapyaisha tamaduni na mapokeo ya kidini mintarafu mwanga wa Injili. Uhuru wa wana wa Mungu walioupata kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo unawawezesha kupata hadhi ya kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu na wakati huo huo, kuiwezesha imani kupenya katika tamaduni mbalimbali na kutambua mbegu ya ukweli na hatimaye, kuiwezesha kufikia utimilifu wake! Kwa njia ya wito wa uhuru, waamini wanagundua maana halisi ya utamadunisho wa Injili: Uwezo wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuheshimu na kuthamini kile kilicho kizuri na cha kweli katika tamaduni. Jambo hili si rahisi kwani kuna kishawishi cha “Kila mwamba ngoma, ngozi huivutia kwake.” Katika mchakato wa uinjilishaji, kumekuwepo na makosa yaliyotendeka, kiasi cha kulinyima Kanisa amana na utajiri kutoka katika tamaduni mahalia, kielelezo cha jamii ya watu husika. Huu ni mwelekeo ambao umekwenda kinyume kabisa na uhuru wa Kikristo!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Fumbo la Umwilisho limetangazwa na kufunuliwa na Kristo Yesu, chemchemi na kilele cha ufunuo wote. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho amewarejeshea wanadamu hadhi yao kuu, amejiunga kwa namna fulani na kila mwanadamu, akafanya kazi, akafikiri na kutenda kwa utashi na moyo wa kibinadamu, akazaliwa, na kufanana na binadamu katika yote isipokuwa katika dhambi! Rej. GS 22. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kuheshimu tamaduni za watu na kwamba, Kanisa Katoliki maana yake ni Kanisa ambalo liko wazi kwa ajili ya watu, tamaduni na nyakati zote, kwani Kristo Yesu ameteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya watu wote. Tamaduni katika asili yake ni mchakato unaoendelea kubadilika, changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa nyakati hizi zenye mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia. Wakristo watambue kwamba, wamepokea zawadi ya uhuru ambayo wanapaswa kuilinda na kuendelea kujielekeza zaidi katika kuimwilisha, ili hatimaye, iweze kufikia utimilifu wake. Baada ya kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti, waamini wanapaswa kuendelea kusafiri kuelekeza utimilifu wa uhuru wa kweli!

Uhuru wa Kikristo
13 October 2021, 16:31

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >