Tafuta

Mkutano wa 35 wa Kuombea Amani: Wito wa Amani Duniani Oktoba 2021. Mkutano wa 35 wa Kuombea Amani: Wito wa Amani Duniani Oktoba 2021. 

Mkutano wa 35 wa Kuombea Amani Duniani: Wito wa Amani: 2021

Mkutano wa 35 wa Kuombea Amani Duniani 2021: Amani inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa amani duniani. Amani inakwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uharibifu wa mazingira ni matokeo ya kiburi cha binadamu anayejisikia kuwa ni mmiliki wa kazi ya uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuanzia tarehe 6 hadi 7 Septemba 2021 imeendesha Mkutano wa 35 wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani duniani, kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu umenogeshwa na kauli mbiu “Watu ndugu, Ardhi ya baadaye.” Wajumbe walitoa wito wa amani kwa Jumuiya ya Kimataifa uliosomwa na Sabera Ahmadi kutoka Afghanstan na kukipatia kikundi cha watoto ili kuwagawia wajumbe, tayari kwenda kuhamasisha utamaduni wa amani katika nchi zao asilia. Wajumbe wanasikitika kusema kwamba, hata leo hii kuna vita vinaendelea kurindima sehemu mbalimbali za dunia, kuna vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha amani, ustawi na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa inaonekana kana kwamba imeamua kujikita katika matumizi ya silaha kama suluhu ya migogoro mbalimbali inayoendelea kuibuka kila kukicha! Kwa bahati mbaya kizazi kilichoshuhudia madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kinaendelea kutoweka pole pole, kiasi cha kupoteza kumbukumbu ya majanga ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Kumekuwepo na mjadala mintarafu ujenzi wa utamaduni wa amani duniani unaoendelea kushika kasi ili kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupata mwono wa pamoja kuhusu familia kubwa ya binadamu. Watu wanakufa na kuteseka. Kuna kundi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Kuna watu wameathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na waathirika wakubwa ni wanawake wanaoteswa na kudhalilishwa utu na heshima yao! Kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kiasi cha kuwapokonya watoto hawa ile fursa ya kufurahia utoto wao na hatimaye wazee wanajikuta wakiwa “wametelekezwa kama magari mabovu.” Kuna maskini wasionekana, lakini wameshiriki katika mkutano huu, wakiomba kwanza kabisa amani duniani na kusikilizwa ili kuweza kufahamu madhara ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Dini zina uwezo wa kukuza na kudumisha msingi wa amani na kusaidia kuelimisha juu ya umuhimu wa amani. Ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema, ikiwa kama dini zinatumika kwa ajili ya kuchochea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Amani ni chemchemi ya utakatifu na wala hakuna Vita Takatifu na watu wasitumie jina takatifu la Mwenyezi Mungu kwa kufanya vitendo vya kigaidi au kuchochea, ghasia na vita. Watu wa Mungu wana kiu ya amani.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya majadiliano ya kidini na kiekumene katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zinazojitokeza. Wajumbe wanawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kunogesha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni sehemu mbalimbali za dunia. Kamwe wasikate tamaa kwani huu ni msingi wa utambulisho wa udugu wa kibinadamu. Huu ndio mwelekeo unaopaswa kuendelezwa. Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita ni kinyume cha maadili na utu wema. Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW unalenga kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu bila ya kuwa na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Amani ya kweli inajengwa kwa njia ya majadiliano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa amani duniani.

Amani inakwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uharibifu wa mazingira ni matokeo ya kiburi cha binadamu anayejisikia kuwa ni mmiliki wa kazi ya uumbaji. Msimamizi wa mazingira aliyegeuka kuwa ni mmlimiki wa mazingira, tayari kutawala na kutumbukia katika vita. Udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira ni chanda na pete, ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limedhihirisha udhaifu wa binadamu na kwamba, watu wote wako kwenye mtumbwi mmoja; kumbe, washibane na kushikamana! Matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kamwe hayawategemei watu wanaotumia vibaya kazi ya uumbaji kwa kuinyonya na ubinafsi, unaowafanya baadhi ya watua kuishi kwa ajili yao binafsi, bila kuwafirikia jirani zao. Leo na kesho iliyo bora zaidi inawategemea zaidi wanawake, watu wanaomwilisha mshikamano na udugu wa kibinadamu. Wajumbe wanamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie waamini kujenga familia ya kibinadamu inayo heshimu mazingira nyumba ya wote. Wito wa amani umesomwa mbele ya Magofu ya Colosseo mjini Roma, alama ya ukuu lakini pia inafumbata mateso na mahangaiko ya binadamu. Kwa msisitizo mkubwa wajumbe wanasema nguvu ya imani kwa Mwenyezi Mungu ni kwake ambaye jina lake amani!

Wito wa Amani 2021

 

12 October 2021, 14:58