Tafuta

Balozi Liberata Mulamula Rutageruka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anahimiza ujenzi wa utamaduni wa amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anahimiza ujenzi wa utamaduni wa amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Balozi Mulamula: Dumisheni Amani Kwa Maendeleo na Ustawi wa Jamii

Balozi Liberata Mulamula Rutageruka anasema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa watu wanaochezea amani duniani, watambue kwamba, wanachezea uhai, ustawi wa jamii na maendeleo ya watu wa Mungu. Kumbe, hakuna maendeleo bila amani na wala hakuna amani bila maendeleo ya kweli yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu! Msichezee Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa aliwakutanisha viongozi wa kidini huko mjini Assisi, nchini Italia, kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuanzia tarehe 6 hadi 7 Septemba 2021 imeendesha Mkutano wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani duniani, kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za dunia akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu ulinogeshwa na kauli mbiu “Watu ndugu, Ardhi ya baadaye.”

Mkutano umeandaliwa wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana na athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki hitimisho la Mkutano huu uliofanyika pembeni mwa Magofu ya Colloseo alikazia umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; kwa kuguswa na shida, mahangaiko na matarajio ya wengine, kwa kujivika ujasiri wa huruma na upendo. Ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii dalili za kushindwa kwa siasa na binadamu katika ujumla wake. Ni aibu ya kushinda kwa nguvu za giza na ubaya wa moyo! Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu.

Dialogue
Dialogue

Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa ni vyombo na sauti ya wale wasiokuwa na sauti; watetezi wa wanyonge, tayari kujenga utamaduni wa amani duniani. Ni wakati wa kung’oa dhana ya vita, chuki na uhasama kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu. Ni wakati wa kupunguza matumizi makubwa ya silaha za kijeshi na kuanza kuwekeza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kudumisha Injili ya uhai. Ni wakati wa kupunguza silaha na kuwekeza kwenye usalama na uhakika wa chakula! Ni muda muafaka na kuacha unafiki na kujikita katika ukweli na uwazi; kwa kuongeza mgawo wa chanjo dhidi ya silaha! Lengo ni kujenga utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika akili na nyoyo za watu! Ni wakati wa kuwa ni mashuhuda na watumishi wa ukweli! Ni wakati wa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu.

Ni wajibu wa watu wote kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini. Uchafuzi wa mazingira ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kuondokana na magonjwa ya kusahau uwepo wa Mungu na jirani, kiasi cha baadhi ya watu kujiamini kupita kiasi, matokeo yake ni uchafuzi wa maisha ya kiroho. Sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni tiba muafaka na chachu ya mabadiliko ya kweli katika maisha ya binadamu. Udugu wa kibinadamu ujengwe na kusimika katika imani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Ni katika muktadha huu, Balozi Liberata Mulamula Rutageruka (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee katika mkutano huu. Anasema, kauli mbiu iliyochaguliwa kwa Mwaka 2021 ni hamasa kwa wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kauli mbiu inatambua umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Tofauti za kidini, kiimani na kitamaduni ni amana na utajiri mkubwa unaoweza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa haki, amani na mapatano kati ya watu na wala kamwe kisiwe ni kisingizio cha vita, ghasia, chuki na uhasama. Matatizo na changamoto nyingi zinazomwandama mwanadamu zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi na huo ni mwanzo wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Dini kamwe zisiwe ni sababu ya kuibuka kwa vita, chuki na uhasama. Amani ya kweli anasema Baba Mtakatifu lazima ipate chimbuko lake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu!

Balozi Liberata Mulamula Rutageruka alipata fursa ya kuchangia mada katika mkutano huo na mkazo wake ulikuwa ni katika ushiriki wa wanawake na vijana katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano, sanjari na udhibiti wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Watu wengi wameathirika sana kutokana na athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wajumbe wamekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwani hakuna nchi hata moja inayoweza kuishi kama Kisiwa. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu yamewagusa wengi. Kumbe, kuna haja ya kudumisha mshikamano wa kutembea pamoja kama ndugu wamoja! Mshikamano huu ni silaha madhubuti katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini duniani.

Amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Haya ni mambo yanayosimikwa katika kanuni maadili, uhuru wa kujieleza pamoja na mchakato mzima wa maamuzi yanayotolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haki na amani ni sawa na chanda na pete, vinakumbatiana na kukamilishana. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbukumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya wongofu wa kiikolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka anakaza kusema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa watu wanaochezea amani duniani, watambue kwamba, wanachezea uhai, ustawi wa jamii na maendeleo ya watu wa Mungu. Kumbe, hakuna maendeleo bila amani na wala hakuna amani bila maendeleo ya kweli yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu!

st. Egidio
st. Egidio

Mabadiliko ya tabianchi ni janga linalotukumba na kuongezeka kwa kasi kila siku. Athari za mabadiliko ya tabianchi yanaonekana katika dunia yote katika uhalisia wake na kwa namna inayohatarisha maisha. Ongezeko la joto linasababisha limesababisha mafuriko makubwa, ukame wa kutisha na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kutokuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani! Fedha za miradi ya tabianchi ni fedha zinazotolewa na watu binafsi, taifa au mataifa ambazo zinakusanywa kutoka vyanzo vya umma, binafsi na vyombo mbadala kwa lengo la kusaidia hatua za kupunguza na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris vimetaka kuwepo kwa msaada wa kifedha kutoka vyanzo vilivyo na rasilimali nyingi kifedha kwenda kwa wale wenye uwezo mdogo na walioko hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Itifaki hii inatambua kwamba mchango unaotolewa na nchi moja na nyingine kwenye mabadiliko ya hali ya hewa na uwezo wao wa kuzuia na kukabiliana na athari zake hutofautiana sana. Fedha hizo zinahitajika ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwasababu uwekezaji mkubwa unahitajika katika kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa. Si kuzuia tuu, fedha za mabadiliko ya tabianchi zinahitajika kwa usawa huo huo wa kuzuia kwenye kukabiliana na athari mbaya na kupunguza athari zitokanazo na maadiliko ya tabianchi.

Kanuni ya "uwajibikaji wa kawaida lakini uliotofautishwa na uwezo husika" uliowekwa katika Mkataba wa Paris ni kwamba, nchi zilizoendelea zinapaswa kutoa rasilimali fedha ili kusaidia nchi zinazoendelea katika kutekeleza malengo ya mkataba wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC. Mkataba wa Paris umeeleza wajibu wa nchi zilizoendelea, na kuhimiza michango ya hiari kwa wadau wengine. Nchi hizo zilizoendelea pia zimepewa jukumu la kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kwenye mabadiliko ya hali ya hewa. Nchi hizo pia zimepewa jukumu la kuunga mkono mikakati inayoendeshwa na zinazoendelea pamoja na kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya nchi hizo. Ni muhimu kwa serikali na wadau wote kuelewa na kutathmini mahitaji ya kifedha ya nchi zinazoendelea, na pia kuelewa jinsi rasilimali hizi za kifedha zinaweza kuhamasishwa. Utoaji wa rasilimali pia unapaswa kulenga kufikia usawa kati ya kuzuia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa ujumla, juhudi zilizo chini ya Mkataba wa Paris zinaongozwa na lengo lake kuu la kufanya kuwepo na mtiririko wa kifedha unaoendana na uzalishaji mdogo wa hewa chafuzi kwa tabaka la ozoni pamoja na kufanya maendeleo yanayo stahimili hali ya hewa. Mkataba wa Paris pia unasisitiza juu ya uwepo wa uwazi na utabiri unaoaminika wa msaada wa kifedha. Utaratibu wa kifedha: Ili kuwezesha utoaji wa fedha za miradi ya kudhibiti tabianchi, Mkataba ulianzisha utaratibu wa kifedha wa kutoa rasilimali fedha kwa upande wa nchi zilizoendelea kwenda nchi zinazoendelea. Utaratibu huu wa kifedha pia unatumikia kwenye Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Paris. Mkataba unasema shughuli za uendeshaji wa wa taratibu za kifedha zinaweza kukabidhiwa kwa taasisi moja au zaidi za kimataifa zilizopo.  Kituo cha Mazingira Duniani (GEF) kimekuwa kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha tangu kuanza kutumika kwa Mkataba huo mwaka 1994. Katika Mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa UNFCCC, COP16, nchi zilianzisha Mfuko wa tabianchi (GCF) na mwaka 2011 kuuteua kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha. Utaratibu wa kifedha unawajibika kwa COP, ambao ndio unafanya maamuzi ya sera zake, programu zitakazopewa kipaumbele na vigezo vya wakataokuwa wanastahili kupata ufadhili.

Pamoja na kutoa muongozo GEF na GCF zimeanzisha mifumo miwili maalum ya fedha. Mfuko Maalum wa Mabadiliko ya Tabianchi (SCCF)na Mfuko wa Nchi masikini zaidi (LDCF) Mifuko yote hiyo inasimamiwa na GEF na Mfuko wa Kukabiliana (AF) ulioanzishwa chini ya Itifaki ya Kyoto mnamo 2001. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka anasema, licha ya ahadi zote hizi, lakini fedha taslimu iliyokwisha kuchangwa na Nchi tajiri zaidi ulimwenguni ni kidogo sana, ikilinganishwa na ahadi zilizotolewa. Katika mkutano kati ya Italia na Nchi za Afrika, imeamua kuongeza dau katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kufunga mkutano Mkutano wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani dunia. Alipata nafasi ya kusalimiana naye na kwamba, ana matumaini makubwa kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan wa siku moja atapata nafasi ya kutembelea Vatican na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Atahakikisha kwamba anasambaza ujumbe wa amani ulitolewa kwenye mkutano huo!

Balozi Mulamula amani

 

12 October 2021, 15:40