Tafuta

Mateso ni makali ya kuishi huko Haiti wanahitaji msaada. Mateso ni makali ya kuishi huko Haiti wanahitaji msaada. 

Papa Francisko anaombea watu wa Vietnam na Haiti kwa mateso yao

Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana,Papa Francisko ametoa wito wa kusali na kuwa na mshikamano wa dhati kwa watu wa mataifa yenye matatizo kama wale wa Vietnam na Haiti, wote walikumbwa na mafuriko lakini pia kukumbuka hata kusini mwa Italia ambapo kumenyesha mvua kali na kusababisha mafuriko.Amekumbusha uzinduzi wa mkutano wa UN wa COP26 huko Glasgow .

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 31 Oktoba 2021 kwa waamini na mahujaji waliofika kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Papa Francisko amewakumbuka watu ambao wanazidi kuteseka kutokana na hali mbali mbali za matatizo ya maisha, kama vile Vietnam na Haiti nchi ambazo ziko mbali kati yao lakini wakiwa na hali ngumu zinazofanana. Papa amesema: “katika sehemu tofauti za Vietnam mvua za nguvu za muda mrefu katika wiki za mwisho zimesababisha mafuriko makubwa kwa kupelekea kuwahamisha maelfu ya watu. Sala zangu na mawazo yangu yanawaendea familia ambazo zinateseka, pamoja na kuwatia moyo wale ambao wanajikita kujibu dharura hiyo kama vile Mamlaka ya nchi na Kanisa mahalia".

Ukaribu wa kisiwa cha Sicilia na Haiti

Papa anaonesha ukaribu wake hata kwa watu wa Kisiwa cha Sicilia, talia ambao wamekumbwa na mvua kali sana na kusababisha mafuriko. Amefikiria ha watu wa Haiti ambao wanaishi hali ngumu sana. Anawaomba wahusika wa Mataifa waweze kusaidia nchi hiyo ili wasiache peke yake. Na kwa wote waliokuwa wamekusanyika hapo amewaomba wakirudi nyumbani watafute habari za Haiti na kusali sana. Papa Francisko amethibitisha jinsi alivyokuwa anatazama kipindi cha “A Sua Immagine”, (kinachotolewa na televisheni ya Baraza la Maaskofu Italia TV2000) ushuhuda wa Mmisionari mkamiliano wa Haiti, Padre Massimo Miraglio, na kwamba mambo aliyokuwa anasema yanaonesha wazi  jinsi gani mateso na uchungu mwingi uliopo katika ardhi hiyo na jinsi gani ilivyoachwa. Kwa maana hiyo ameomba watu hao wasiachwe.

Wenyeheri wapya

Papa Francisko amekumbusha ambavyo siku ya Jumamosi tarehe 30 Oktoba 2021, walitangazwa huko Tortosa Wenye heri wapya Francesco Sojo López, Millán Garde Serrano, Manuel Galcerá Videllet na Aquilino Pastor Cambero, ambao walikuwa ni mapadre wa Jumuiya ya Shirika la Mapadre Wafanyakazi wa Jimbo la Moyo wa Yesu, na ambao waliuawa kwa chuki kutokana na kutetea imani yao. Walikuwa ni makuhani adilifu na wakarimu wakati wa mateso ya kidini kwenye miaka ya therathini na wakabaki waaminifu katika huduma hata ya kuhatarisha maisha yao. Kwa njia ya ushuhuda wao, Papa ameomba uwe mfano hasa kwa makuhani na kwa maana hiyo ameongeza akiomba kuwapigia makofi wenyeheri wapya!...

Mkutano wa umoja wa mataifa UN, Glasgow

Papa Francisko akiendelea zaidi amegusia juu ya mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN)ambao tarehe 31 Oktoba umefunguliwa rasmi huko Glasgow, nchini Scotland wa COP26, unaohusu mabadiliko ya tabianchi. Papa ameomba kusali ili kilio cha ardhi na kilio cha maskini kiweze kusikilizwa; na katika mkutano huo uweze kutoa majibu muafaka wa kuweza kutoa matumaini ya dhati kwa kizazi kijacho. Katika muktadha huo hata hivyo amekumbusha jinsi ambavyo tarehe hiyo katika uwanja wa Mtakatifu Petro, wanazindua maonesho ya Picha Laudato si’, ambayo ni kazi ya kijana mmoja mpiga picha wa asili ya Bangladesh. Na kwa kuhitimisha amewasalimia waamini wa Roma na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu na amewatakia Dominika njema na wasisahau kusali kwa ajili yake.

31 October 2021, 13:11