Tafuta

Papa Francisko tarehe 17 Oktoba 2021 anawaweka wakfu Askofu mkuu Andrès Gabriel Ferrada Moreira na Askofu Guido Marini. Papa Francisko tarehe 17 Oktoba 2021 anawaweka wakfu Askofu mkuu Andrès Gabriel Ferrada Moreira na Askofu Guido Marini. 

Askofu mkuu Andrès Moreira na Askofu Marini Kuwekwa Wakfu 17 Okt. 2021

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwakweka wakfu Monsinyo Andrés Gabriel Ferrada Moreira Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuwa Askofu mkuu na Monsinyo Guido Marini (56) atawekwa wakfu ili kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki laTortona, nchini Italia. Maaskofu hawa wapya wanatumwa kuyangaza na kuyashuhudia mambo waliyoyaona na kuyasikia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 17 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa katika maadhimisho haya kuwakweka wakfu Monsinyo Andrés Gabriel Ferrada Moreira Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kuwa Askofu mkuu na Monsinyo Guido Marini (56) atawekwa wakfu ili kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tortona, nchini Italia. Maaskofu hawa wapya wanatumwa kuyangaza na kuyashuhudia mambo waliyoyaona na kuyasikia! Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa sala, kiongozi anayejipambanua kwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu. Ni kiongozi anayepaswa kuwa kweli ni mchungaji mwema, anayetambulikana pia kutokana na harufu ya kondoo wake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Kimsingi haya ndiyo mambo msingi ambayo yanapaswa kuoneshwa na Askofu au wale wanaotamani kufikia utimilifu wa Daraja Takatifu ambalo kimsingi limegawanyika katika madaraja makuu matatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi, kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Askofu anapaswa kuwa ni shuhuda aminifu wa Kristo Yesu na Kanisa lake; mtu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu; kiongozi ambaye ataonesha kwa maneno na maisha yake kwamba, uongozi kwake ni huduma na wala si cheo! Kwa wanajimbo wake anapaswa kuwa kweli ni mfano wa Baba na Kaka; mpole na mnyenyekevu wa moyo, mwingi wa huruma na mapendo; mvumilivu na mwenye hekima na busara! Awe ni baba mwema anayejitaabisha kuwachunga kondoo wake, kwa kuwaonesha dira na mwelekeo sahihi wa maisha; daima akikazia ushirika, upendo na mshikamano, ili kati ya kondoo wake, asiwepo anayepotea njia, Askofu awe kweli ni kiongozi anayekesha kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Kanisa la Kristo, pasi na kumezwa na malimwengu. Baba Mtakatifu Francisko angependa kuona Kanisa ambalo halina makuu, Kanisa linalojitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ni maskini wa kiroho, hali na kipato. Kanisa ambalo uwezo na nguvu yake haitokani na mali au utajiri wake, bali neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hili ni Kanisa linalopaswa kuiga na kufuata mfano wa Yesu aliyekuwa: fukara, mtii na mseja kamili. Kanisa halina budi kuendeleza utume wa Yesu kwa kuwatangazia watu Injili ya furaha.

Kanisa liwasaidie watu kukutana ili hatimaye, liweze kuambatana na Yesu katika maisha yao. Maaskofu wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni wajenzi wa haki na amani inayofumbatwa katika majadiliano na upatanisho wa kitaifa. Wawe ni vyombo na wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuondokana na wimbi la vita, machafuko na kinzani mbali mbali ili hatimaye, kupandikiza Injili ya upendo. Maaskofu wasaidie kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, kwa kuvuka tabia ya maamuzi mbele na mipasuko. Baba Mtakatifu anasema, amepata uzoefu mkubwa kwa kukutana, kusali na kutafakari kwa pamoja katika nyakati mbali mbali za maisha na utume wake kama Khalifa Mtakatifu Petro. Kwa hakika upendo unagangana na kuponya mipasuko ya kijamii. Utambulisho wa ni upendo kwa Mungu na jirani zao; dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa: furaha, upendo na matumaini kwa wale wote waliokata tamaa. Yote yatapita, lakini upendo kwa Mungu na jirani wadumu milele.

Itakumbukwa kwamba hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Monsinyo Andrés Gabriel Ferrada Moreira kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri na hivyo kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu, uteuzi ambao ulianza rasmi tarehe 1 Oktoba 2021. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Andrés Gabriel Ferrada Moreira alikuwa ni Afisa mwandamizi kwenye Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Andrés Gabriel Ferrada Moreira alizaliwa huko Santiago de Chile tarehe 10 Juni 1969. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 3 Julai 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Santiago de Chile. Baadaye alijiendeleza kwa masomo ya juu na hatimaye, mwaka 2006 akatunukiwa Sahada ya Uzamivu katika Taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian. Kabla ya kuitwa kutekeleza dhamana na utume wake mjini Vatican kunako mwaka 2018, aliwahi kushika nafasi mbalimbali za utume Jimbo kuu la Santiago de Chile. Aliwahi kuwa Mwadili mkuu wa wanafunzi na mkuu wa kitivo cha Taalimungu Seminari kuu ya Kipapa ya Malaika Walinzi, Jimbo kuu la Santiago de Chile: “Seminario Pontificio Mayor de los Santos Ángeles Custodios, Santiago de Chile.”

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Agosti 2021 alimteuwa Monsinyo Guido Marini (56) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tortona, nchini Italia. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Guido Marini alikuwa ni Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Guido Marini alizaliwa tarehe 31 Januari 1965 huko Genoa, Kaskazini mwa Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 4 Februari 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na Kardinali Giovanni Canestri. Baadaye alijiendeleza kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran na kujipatia Shahada ya Uzamivu Kuhusu Sheria za Kanisa na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani. Na mwaka 2007 alijipatia Shahada ya Uzamivu katika Saikolojia ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesianum.

Tangu mwaka 1988 hadi mwaka 2003 amekuwa ni Katibu muhtasi wa Maaskofu wakuu watatu wa Jimbo kuu la Genoa. Amewahi kuwa pia Jaalimu wa Sheria za Kanisa, Mkurugenzi wa Maisha ya Kiroho Seminari ya Jimbo kuu la Genoa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akamteuwa kuwa ni Mshereheshaji Mkuu wa Kipapa hadi mwaka 2013. Wakati wa mkutano wa Baraza la Makardinali kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, alisimamia maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa huku akishirikiana na Kardinali Tarcisio Betone, aliyekuwa Msimamizi mkuu wa mali za Kanisa yaani “Camerlengo” kama anavyojulikana kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Francisko alipoingia madarakani, akaridhia uteuzi wake kunako mwaka 2014 na hivyo kuendelea na utume huu hadi mwaka 2019 alipomwongezea majukumu ya kuwa Mratibu mkuu wa Kwaya ya Kipapa. Kati ya Mwaka 2018 hadi mwaka 2019 alikuwa anafundisha Liturujia katika Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselm, mjini Roma. Amekuwa pia mhubiri mzuri wa mafungo, semina na makongamano mbalimbali. Amewasindikiza vijana wengi katika maisha na utume wao, akiwasaidia kiroho!

Maaskofu wapya

 

15 October 2021, 15:11