Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Kuelekea Sisi Kubwa Zaidi". Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Kuelekea Sisi Kubwa Zaidi".  

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 107 Ya Wakimbizi Duniani 2021

Maadhimisho ya Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Kuelekea Sisi Kubwa Zaidi”. Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 107 ya Wakimbizi anakazia kuhusu: Mwelekeo mpana wa historia “yetu”, Kanisa linapaswa kuwa ni Katoliki zaidi, Kujenga ulimwengu fungamanishi na ndoto ndiyo kwanza inaanza kucharuka! Upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Tangu wakati huo, Siku hii imekuwa ikiadhimishwa Jumapili baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Lakini kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza maoni na kuridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Jumapili ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 26 Septemba 2021. Maadhimisho ya Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Kuelekea Sisi Kubwa Zaidi”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2021 anakazia kuhusu: Mwelekeo mpana wa historia “yetu”, Kanisa linapaswa kuwa ni Katoliki zaidi, Kujenga ulimwengu fungamanishi na ndoto ndiyo kwanza inaanza kucharuka!

Baba Mtakatifu anasema, changamoto ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 imesababisha watu kuanza pole pole kutoka katika ubinafsi na tabia ya kujifirikia wenyewe na kuanza kujielekeza katika mawazo fungamani yanayoonesha dira na mwelekeo mpana zaidi wa ulimwengu mamboleo. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha umoja katika utofauti! Mwanadamu alipopotoka na kukengeuka, Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake wa daima akaanzisha mchakato wa upatanisho na familia nzima ya binadamu na akataka kufanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao! Rej. Ufu 21:3. Historia ya wokovu ni fungamanishi, changamoto kwa waamini kuwa mwelekeo mpana zaidi badala ya kujikita katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko sanjari na ubinafsi wa kupindukia. Waathirika wakubwa ni wale wanaotazamwa kuwa ni wengine kwa maana: wageni, wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Ukweli wa mambo ni kwamba, watu wote ni wamoja na wamepanda boti moja, mwaliko ni kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama familia kubwa ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa Kanisa Katoliki kuwa kweli wakatoliki kwa kutambua kwamba wao ni “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” Efe 4:4-6. Ukatoliki unapaswa kuwafumbata na kuwaambata watu wote hadi miisho ya dunia. Roho Mtakatifu anawawezesha kujenga umoja katika tofauti zao msingi, ili kunogesha utamaduni wa watu kukutana ili hatimaye, kukuza majadiliano ya kitamaduni, fursa kwa Kanisa kuweza kukua na waamini kutajirishana. Waamini wajitambue kwamba, wao ni sehemu ya Kanisa na familia moja ya binadamu. Waamini wanaalikwa kushirikiana na kushikamana katika kutangaza na kushuhudia imani yao inayosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Rej. Mt 10: 7-8. Kanisa linatumwa kwenda kukutana na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii!

Huko ndiko wanaweza kukutana na wakimbizi, watu wasiokuwa na makazi maalum; wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; wote hawa Kristo Yesu analitaka Kanisa kuwaonesha upendo na wokovu unaotangazwa. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni fursa ya kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa matendo. Ni nafasi ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuuangana pamoja katika safari hii, ili kuweza kupyaisha familia ya binadamu, ili hatimaye, kujenga leo na kesho inayosimikwa katika haki na amani bila mtu awaye yote kuachwa nyuma. Yote haya yawe ni sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kubadilishana mawazo kama ilivyokuwa wakati ule wa Sherehe ya Pentekoste, watu wakazungumza na kusikilizana katika lugha ya upendo, matendo makuu ya Mungu. Rej. Mdo 2: 9-11. Hapa mjini Yerusalemu watu wote walikuwa wameungana katika umoja na amani, ili kusherehekea matendo makuu ya Mungu. Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja ya kuvunjilia mbali kuta zinazowatenga watu na hivyo kujielekeza katika utamaduni wa watu kukutana, kwa kuondokana na woga, ili kutajirishana kutokana na tofauti zilizopo. Mipaka ya nchi inaweza kuwa ni mahali pa watu kujenga umoja na mshikamano wa dhati!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili kuitengeneza dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Huu ni mwaliko wa kujizatiti katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuwajibika kwa pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi kijacho! Watu wa Mungu waoneshe upendo na mshikamano wa dhati kwa wale wote wanaoteseka kutoka na sababu mbalimbali, ili kujenga ulimwengu unaokita msingi wake katika maendeleo fungamani ya binadamu, haki, usawa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuota ndoto ya pamoja, bila woga kama familia moja ya binadamu na wandani wa safari, kama ndugu wamoja wanaoishi katika dunia hii. Baba Mtakatifu Francisko anakamilisha ujumbe wake kwa Siku ya 107 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2021 kwa sala, inayoonesha ile furaha ya kuwapata wale waliopotea, waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Anamwomba Mwenyezi Mungu awajalie waamini neema ya kutekeleza mapenzi yake hapa duniani na awabariki wale wote wanaoonesha upendo na ukarimu kwa wageni, wakimbizi na wahamiaji, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja!

Papa Wakimbizi 2021
23 September 2021, 15:19