Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani 8 Septemba 2021: Papa Francisko anakazia umuhimu na maana ya elimu kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani 8 Septemba 2021: Papa Francisko anakazia umuhimu na maana ya elimu kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. 

Papa Francisko: Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani 2021

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2021 anasema kwamba, elimu ni nyenzo msingi katika ujenzi wa utu wa binadamu ulimwenguni pamoja na historia yake. Elimu kimsingi ni kielelezo cha upendo na uwajibikaji unaorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ujinga Duniani “International Literacy Day” yaliasisiwa kunako mwaka 1965 katika mkutano wa Mawaziri wa Elimu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliokuwa wamekutanika huko mjini Teheran nchini Iran. Mawaziri hao wakapendekeza kuanzishwa kwa Siku ya Kupamba na Ujinga Duniani kwa kuhimiza dhana ya usomaji endelevu. Wazo hili liliibuliwa kutokana na kiwango kikubwa cha watu wasiojua kusoma na kuandika duniani. Kunako mwaka 1966, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), lilitangaza kwamba, tarehe 8 Septemba ya kila mwaka ni Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani. Lengo ni kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kujizatiti katika mapambano dhidi ya baa la ujinga duniani. Hata leo hii, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado kuna umati mkubwa wa watu wasiojua kusoma na kuandika! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 773 ambao hawakubahatika kupata elimu ya msingi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho Siku ya Kupambana na Baa la Ujinga Duniani kwa mwaka 2021 anasema kwamba, elimu ni nyenzo msingi katika ujenzi wa utu wa binadamu ulimwenguni pamoja na historia yake. Elimu kimsingi ni kielelezo cha upendo na uwajibikaji unaorithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine! Kimsingi elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye, kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano wa udugu, mafungamano na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano.

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamewawezesha wanafunzi wengi kuendelea na masomo, lakini kuna umati mkubwa wa watoto na vijana umebaki nyuma kwa masomo kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo limetikisa mfumo mzima wa sekta ya elimu duniani. Inakadiriwa kwamba, kuna watoto zaidi ya milioni 10 wako hatarini kutoendelea na masomo kutokana na kuyumba kwa uchumi kitaifa na kimataifa. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa kwenda shuleni, hawakupata fursa hii. Changamoto zilizoibuliwa kwenye sekta ya afya zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kukazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika udugu wa kibinadamu.

Mabadiliko ya mfumo wa elimu duniani yanapaswa kuwahusisha wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuondokana na ukosefu wa haki jamii; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kuweza kupambana na umaskini pamoja na tabia ya watu kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato fungamanishi unaopania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kuondokana na upweke hasi, kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini. Hali hii itawasaidia vijana wengi kuondokana na ugonjwa wa sonona; utumwa mamboleo, chuki, uhasama, matusi, ukatili pamoja na uonevu mitandaoni.

Ujinga Duniani 2021

 

08 September 2021, 15:47