Tafuta

Papa: Kanisa Ni Sakramenti ya Upendo na Umoja Kwa Wote!

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Septemba 2021, amegusia kishawishi cha Mitume kutaka kujifungia wao wenyewe na baadaye anawapatia wosia wa kutekeleza katika maisha na utume wao dhidi ya majaribu ya dhambi. Mtume Yohane kwa niaba ya wengine anasema: Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza! Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo Mtume anasema, “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Flp 2:9-11. Ni katika jina la Kristo Yesu nguvu ya Mungu inayoganga, kuponya na kuokoa imejidhihirisha katika Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele katika historia ya wokovu! Kumbe, Jina Yesu maana yake Mungu anaokoa. Kwa njia ya Jina la Yesu mwanadamu anakirimiwa maisha mapya. Kanisa la Mwanzo lilitenda miujiza mingi kwa njia ya Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umoja wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Rej. LG 48. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 26 Septemba 2021 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya 26 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amegusia kishawishi cha kutaka kujifungia wao wenyewe na baadaye anawapatia wosia wa kutekeleza katika maisha na utume wao dhidi ya majaribu ya dhambi.

Mtume Yohane kwa niaba ya Mitume wengine anasema: “Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake.” Mk 9: 38-41. Kristo Yesu anachukua fursa hii, kuwataka wafuasi wake waondokane na tabia ya kuwagawa watu katika makundi ya wema na wabaya, kwa sababu jambo kubwa zaidi ni ushiriki mkamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini wote wanaalikwa kuwa macho ili wasiingie katika majaribu ya dhambi na hivyo kuwa ni sababu ya makwazo kwa wengine. Maneno ya Kristo Yesu yanaonesha kishawishi cha kutaka kumbinafsisha Kristo Yesu katika maisha yao na kwamba, wao ndio waliokuwa wadau wakuu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, hali ambayo ingewafanya kujisikia kuwa kama wateule na hatimaye, kugeuka kuwa ni adui wa watu wengine.

Tabia ya kutaka kujifungia katika ubinafsi inapelekea watu wengine kutengwa na hasa ikiwa kama “hawawezi kupikika chungu kimoja.” Uchoyo na ubinafsi ni chanzo cha maafa makubwa katika historia ya mwanadamu. Huu ni mwanzo wa kuwa na watu wanaotawala kimabavu na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anatoa angalisho hata kwa upande wa Kanisa kuwa makini zaidi kwa sababu Shetani, Ibilisi ni chanzo cha migawanyiko na mipasuko ya kijamii, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, waliotaka kumwengua hata yule aliyethubutu “kumshikisha adabu Shetani, Ibilisi”. Waamini wajenge Jumuiya ya Kikristo inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, upendo, ukarimu na uwazi na kamwe wasiwepo baadhi ya waamini wanaodhani kwamba, “wao ni matawi ya juu” na wengine wanabaki kuwa ni “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Jumuiya ya waamini ijitahidi kutembea na kuwaambata watu wote bila ya kuwahukumu wala kuwatenga. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema, ili waweze kukishinda kishawishi cha kuwahukumu na kuwapanga watu wengine katika makundi maalum. Hatimaye, Mwenyezi Mungu awaepushe na mawazo ya kutaka kujifungia katika undani wao, kwa “kujikinai kuwa ni watu wema zaidi.”

Hii ndiyo tabia ya baadhi ya Mapadre wanaoambatana na watu wachache wanaodhani kwamba, ni waaminifu kwao; wafanyakazi katika shughuli za kichungaji wanaojifungia kwenye “ngome” zao ili kutokutoa mwanya kwa watu wengine kuingia ndani mwake. Huu ndio mwelekeo pia kwa baadhi ya vyama na mashirika ya kitume yenye karama maalum. Kuna hatari ya kuzigeuza Jumuiya za Kikristo kuwa ni “viota” vya ubaguzi na wala si mahali pa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Roho Mtakatifu anatenda shughuli zake katika ukweli, uwazi na ukarimu ambapo kila mtu anajisikia kuwa amefika nyumbani! Kristo Yesu mwishoni mwa mazungumzo yake na Mitume anawapatia wosia na onyo kali kuhusu majaribu ya dhambi akisema, “Na mkono na mguu wako ukikukosesha ukate; na jicho lako likikukosesha ling’oe” Rej. Mt 9: 42-50. Hapa Kristo Yesu anaonesha ukali, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wafuasi wake! Anafikiri na kutenda kama daktari bingwa, ili waweze kukua na hatimaye, kuzaa matunda ya upendo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ni wapi ambapo maisha yao yanasigana na kwenda kinyume cha tunu msingi za Kiinjili? Ni yepi yale ambayo Kristo Yesu anataka kila mmoja wao kuyakata katika maisha? Bikira Maria, Mwenye Moyo Safi awasaidie waamini kuwa wakarimu kwa jirani zao na makini katika maisha yao ya kiroho!

Papa Tafakari
26 September 2021, 15:02

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >