Tafuta

Mwenyeheri Mamerto Esquiú alikuwa kweli ni mmisionari na mchungaji aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo katika huduma. Mwenyeheri Mamerto Esquiú alikuwa kweli ni mmisionari na mchungaji aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo katika huduma. 

Mwenyeheri Mamerto Esquiù: Mmisionari Na Baba wa Maskini

Mwenyeheri Mamerto Esquiú, Mtawa na Askofu wa Jimbo Katoliki Cordobola alikuwa ni shuhuda na mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Jumuiya ya waamini na watu wa Mungu katika ujumla wake. Alikuwa ni mtu aliyejisadaka kwa maisha ya: Sala, Utume, Huduma sanjari na kupandikiza mbegu ya amani na udugu wa kibinadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 5 Septemba 2021amewakumbusha waamini kwamba, Jumamosi tarehe 4 Septemba, Mtumishi wa Mungu Mamerto de La Ascensiò Esquiú ametangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Baba Mtakatifu anasema Mwenyeheri Mamerto Esquiú wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko na Askofu wa Jimbo Katoliki Cordobola, Argentina alikuwa ni shuhuda na mtangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Jumuiya ya waamini na watu wa Mungu katika ujumla wake. Alikuwa ni mtu aliyejisadaka kwa maisha ya: Sala, Utume, Huduma sanjari na kupandikiza mbegu ya amani na udugu wa kibinadamu!

Mwenyeheri Mamerto de La Ascensiò Esquiú alizaliwa tarehe 11 Mei 1826 huko San Josè de Piedra Blanca nchini Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, tarehe 14 Julai 1842 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 18 Oktoba 1848 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baadaye, kuanzia mwaka 1850 aliteuliwa kufundisha Seminarini na kama Padre mwongozi wa maisha ya kiroho. Kutokana na uchaji, uadilifu na busara akachaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Serikali ya Catamarca. Kunako mwaka 1862 alihamishiwa nchini Bolivia kama mmisionari na kupangiwa kufundisha Seminarini. Papa Leo XIII akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Còrdoba, Argentina na kuwekwa wakfu tarehe 12 Desemba 1880. Katika utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, akajipambanua kuwa ni mtu wa sala, na mwenza makini katika safari ya maisha ya kiroho. Alijitahidi kuishi ufukara kwa ajili ya huduma kwa maskini.

Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumiziwa pembezoni mwa jamii. Alijitahidi kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inajikita zaidi katika Injili ya upendo na huduma kwa maskini. Alibahatika kuwa na kipaji kizuri sana cha kuhubiri. Aliposimama kuhubiri, watu walidemka kwa furaha na shangwe. Mwenyeheri Mamerto Esquiú alifariki dunia tarehe 10 Januari 1883 huko La Posta Del El Suncho. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 16 Desemba 2006 akaridhia karama zake za kishujaa na hatimaye, tarehe 4 Septemba 2021 akatangazwa na Kardinali Luis Héctor Villalba kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri. Huu ni wito na mwaliko wa kutembea katika utakatifu wa maisha, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Mwenyeheri Mamerto de La Ascensiò Esquiú alikuwa ni mzalendo kwa nchi yake ya Argentina, kiasi cha kutumia mali na utajiri wa Argentina kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Alisimama kidete kulinda, kutetea: amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mwenyeheri

 

 

07 September 2021, 14:31