Tafuta

Papa Francisko: Maadhimisho ya Sinodi Ngazi ya Kijimbjo ni muda muafaka wa kupyaisha hija ya maisha ya kiroho, alama ya umoja na uwajibikaji wa watu wa Mungu. Papa Francisko: Maadhimisho ya Sinodi Ngazi ya Kijimbjo ni muda muafaka wa kupyaisha hija ya maisha ya kiroho, alama ya umoja na uwajibikaji wa watu wa Mungu. 

Maadhimisho ya Sinodi Kijimbo: Upyaisho, Umoja na Uwajibikaji!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo Katoliki la Cuneo na Fosano nchini Italia yatasaidia kupyaisha safari ya maisha ya kiroho ya watu wa Mungu kwa kujikita katika msingi wa umoja na uwajibikaji. Amewataka watawa na waamini katika ujumla wao kuendelea kumfuasa Kristo Yesu huku wakiwa na furaha tele! Uwajibikaji wa waamini wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa la Kristo Yesu kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Anawataka waamini kukuza ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu muhimu sana ya kuyatakatifuza malimwengu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha wa “Dhana ya Sinodi Katika Maisha na Utume wa Kanisa” Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 01 Septemba 2021 amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Cuneo na Fossano, waliokuwa wameambatana na Askofu wao Piero Delbosco. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo yatasaidia kupyaisha safari ya maisha ya kiroho ya watu wa Mungu kwa kujikita katika msingi wa umoja na uwajibikaji. Amewataka watawa na waamini katika ujumla wao kuendelea kumfuasa Kristo Yesu huku wakiwa na furaha tele!

Neema na nguvu ya Roho Mtakatifu iwashukie na kuwafariji wazee, wagonjwa na wanandoa wapya. Upendo kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha maisha ya Kikristo na chemchemi ya wokovu. Licha ya udhaifu na dhambi, lakini upendo wa huruma ya Mungu utaendelea kumwandamana mwamini katika hija ya maisha yake hapa duniani. Ni katika Kristo Yesu, mwamini anaweza kuonja na kupata neema na utimilifu wa furaha ya kweli katika maisha na nguvu ya kutekeleza matendo mema! Roho Mtakatifu awakirimie imani, matumaini na mapendo, ili waweze kuwa ni mashuhuda wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Ili kuweza kufanikisha azma hii, Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kukita maisha yao katika: Sala, Sakramenti za Kanisa sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Mwezi Septemba, shule na taasisi nyingi za elimu zinafunguliwa. Huu ni wakati wa wanafunzi na waalimu kujiandaa kurejea tena kwenye majukumu yao ya kawaida. Baba Mtakatifu anawaombea wanafunzi na walimu wote, waweze kupata Roho wa hekima, ili aweze kuwafariji katika shida na mahangaiko yao ya kila siku.

Papa Sinodi Jimbo

 

 

 

01 September 2021, 12:20