Tafuta

Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa limefunguliwa rasmi kwa kuongozwa na kauli mbiu "Visima vyangu vyote vimo kwako" Zab. 87:7 Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa limefunguliwa rasmi kwa kuongozwa na kauli mbiu "Visima vyangu vyote vimo kwako" Zab. 87:7 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Injili na Ekaristi Takakatifu

Kardinali Bagnassco amesema, Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika Injili na uwepo wake endelevu na angavu unafumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hata kama sauti ya waamini ni hafifu, lakini huu ni mwangwi wa sauti ya waungama imani na wafiadini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Imani kwa Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, (Council of Bishops’ Conferences of Europe (CCEE), Jumapili tarehe 5 Septemba 2021 amezindua Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), kwa Ibada ya Misa Takatifu huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria.  Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Hii ilikuwa ni siku maalum ambamo waamini waliizunguka Altare kuadhimisha Fumbo la Imani, Ekaristi Takatifu, chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Hili ni adhimisho la furaha ya watu wa Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi ili kuwaambata watu wote wa Mungu popote pale walipo! Katika mahubiri yake, Kardinali Angelo Bagnasco amekazia kuhusu uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake; ujumbe kwa vijana waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaojionesha katika Injili na uwepo wake endelevu na angavu unafumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hata kama sauti ya waamini ni hafifu, lakini huu ni mwangwi wa sauti ya waungama imani na wafiadini waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa anatangaza furaha kuu inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu mwanga angavu wa Mataifa, licha ya dhambi na udhaifu wa watoto wake. Kardinali Bagnasco amewakumbusha waamini kwamba, hawako peke yao ili kukabiliana na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo, fumbo la maisha pamoja na kutaka kuzima kiu ya uhuru na maisha ya uzima wa milele. Kila mtu anayo nafasi ya pekee mbele ya Uso wa Mungu anayemwangalia kila mmoja wao kwa upendo kwa sababu wamekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu. Huyu ndiye Mkombozi wa ulimwengu na Mkate wa maisha na uzima wa milele. Kanisa linayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapewa heshima na utu wake unaobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka!

Vijana waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wamekumbushwa kwamba, wao ni amana, utajiri na mapambazuko ya Kanisa. Kristo Yesu ameingia katika sakafu ya nyoyo zao ili kuweza kuishi pamoja nao milele yote. Shukrani za pekee, zimewaendea wazazi na walezi waliothubutu kuwarithisha Injili ya uhai na imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Jambo la msingi kwa vijana ni kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema kipindi hiki cha majiundo na malezi kujifunza elimu ya dini na Ukristo katika ujumla wake, bila kuwa na maamuzi mbele, daima wakitambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye siri ya mafanikio yao. Imani na uhuru wa kweli ni chemchemi ya furaha na upendo wa dhati. Katika ulimwengu mamboleo kuna udhaifu mkubwa sana katika kufikiri kwani kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba imani ni adui mkubwa wa sayansi pamoja na uwezo mkubwa wa mwanadamu kufikiri. Imani inatafuta kuelewa na sayansi inahitaji imani ili kujihifadhi.

Hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kujizatiti katika njia inayowapeleka katika ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watambue kwamba, katika maisha kuna kupanda na kushuka; kuna kuteleza na kuanguka, lakini changamoto kubwa ni kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Kanisa lina matumaini makubwa kwa uwepo wa vijana, kwa ari na moyo wao mkuu na kwamba, hata vijana wanahitaji uwepo angavu wa Kristo Yesu katika safari ya maisha yao. Yote yanapita na kuzeeka, lakini Mwenyezi Mungu ni kijana na Kanisa ni kielelezo cha ujana wa ulimwengu kwa sababu ndani mwake, linahifadhi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya waamini kila siku!

Kardinali Angelo Bagnasco amewashukuru na kuwapongeza wakleri, kielelezo cha Kanisa Mama na Mwalimu; “Mater et magistra” chemchemi ya mafundisho jamii ya Kanisa. Kanisa linakazia kuhusu: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mapadre ni kielelezo cha Kristo Yesu mchungaji mwema, mwanga angavu wa Injili, nguvu ya Ekaristi Takatifu na umoja wa Kanisa. Mama Kanisa anawapongeza Mapadre kwani wao ni kielelezo cha upendo wa Mungu, manabii wa Roho Mtakatifu; watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kanisa haliwezi kuwahakikishia usalama wa maisha yao, lakini linawaambia! Jipeni moyo msiogope! Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na uwepo wake angavu na endelevu unajikita katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha" (Mt 11:28). Ni mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu kwa wale wanaoelemewa na Msalaba wa maisha; wanaolia na kuomboleza; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa utu na heshima yao kwa kudai haki! Kwa wakimbizi na wahamiaji; wote hawa Kristo Yesu anawaita waende kwake naye atawatuliza na kuwanyanyua juu hadi kwenye utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa katika maisha na utume wake anamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho haya amesema, Kongamano hili ni alama ya matumaini; umoja na mshikamano wa Kanisa. Amewashukuru wote waliochangia katika kufanikisha Kongamano hili, kielelezo makini cha uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu ndani ya Kanisa na katika ulimwengu katika ujumla wake. Ekaristi Takatifu ni chakula na lishe ya maisha ya Kikristo na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni fursa ya kumwomba Mwenyezi aendelee kufanya hija na Kanisa lake, kwa kulijalia nguvu na mwanga wa kutekeleza dhamana na utume wake katika ulimwengu mamboleo. Awajalie walimwengu nguvu na ari ya kuishi pamoja kwa amani na upendo!

Budapest Ekaristi Takatifu

 

06 September 2021, 14:53