Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwa: Watangazaji wa Injili, Mashuhuda wa Udugu na Wajenzi wa Injili ya Matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwa: Watangazaji wa Injili, Mashuhuda wa Udugu na Wajenzi wa Injili ya Matumaini. 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Ujumbe kwa Maaskofu!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake iliyokuwa inabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, amegusia kuhusu ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanapaswa kuwa ni watangazaji wa Injili. Wawe ni mashuhuda wa udugu na wajenzi wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo! Ujumbe mzito kwa Maaskofu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Budapest, Hungaria, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 na kupokelewa kwa heshima zote za kitaifa alikutana na kuzungumza kwa faragha na Rais pamoja na Waziri mkuu wa Hungaria na baadaye akakutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria. Katika hotuba yake iliyokuwa inabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, amegusia kuhusu ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanapaswa kuwa ni watangazaji wa Injili. Wawe ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu na wajenzi wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo! Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa nchini Hungaria limejengeka juu ya ushuhuda wa waungama na wafiadini. Hawa ndio wale waliosagwa kama “ngano”, ili kuwashirikisha jirani zao upendo wa Mungu. Ni watu waliopondwa na kugeuka kuwa ni “divai” chemchemi ya maisha mapya, tayari kujenga historia ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Injili ya upendo ni kielelezo muhimu sana cha ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kwa kutunza mizizi ya historia ya Kanisa, Maaskofu wawe na ujasiri kwa kuangalia mbele kwa matumaini, kwa kuibua mbinu mpya za kutangaza na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu anasema, anayo kumbukumbu endelevu ya Watawa wa Shirika la Yesu, waliolazimika kuikimbia nchi yao kutokana na madhulumu.

Lakini kutokana na uaminifu kwa wito wao, wakaanzisha makao mapya nchini Argentina. Baba Mtakatifu anasema amejifunza mengi kutoka kwa watawa hawa! Na kwa njia yao, Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wote ambao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na madhulumu na nyanyaso mbalimbali. Mapokeo ya Kanisa ni mto wa maisha mapya unaobubujika kutoka katika asili, yaani Kristo Yesu hadi kulifikia Kanisa kwa wakati huu, na hivyo kushirikishwa historia ya Mungu katika maisha yao. Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yananogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kanisa linapata asili yake kutoka kwenye Kisima ambacho ni Kristo Yesu na hivyo kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili, changamoto na mwaliko kwa Maaskofu kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mungu na ulimwengu katika ujumla wake.

Maaskofu wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya wokovu, baada ya kukutana na kufanya uzoefu na mang’amuzi kutoka kwa Kristo Yesu. Watambue kwamba, Hungaria ni nchi muhimu sana katika kukabiliana na changamoto mambaleo kama vile: Ukani Mungu pamoja na watu kupenda kumezwa na malimwengu zaidi. Uwepo wa Kanisa uwe ni alama ya maji yanayozima kiu ya mwanadamu. Maaskofu wawe ni mashuhuda wa upendo wa Injili. Wawe pia watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu; furaha ya watu wa Mungu na majirani mwema kwa mapadre na watawa. Waoneshe na kushuhudia moyo wa kibaba, huku wakiwashirikisha zaidi waamini walei. Kisima cha maji ya ushuhuda wa imani kiwabubujikie watu wa Mungu nchini Hungaria. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki Hungaria kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, unaobubujika kutoka kwa watu wenye tamaduni, makabila, itikadi na dini mbalimbali, kielelezo cha Injili ya upendo!

Kamwe tofauti za watu kisiwe ni sababu ya chuki na uhasama, na badala yake nyenzo msingi ya majadiliano katika ukweli na uwazi. Maisha ya wananchi yajengwe kwenye udugu wa kibinadamu, mshikamano, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Katika mwelekeo huu, Kanisa liwe ni daraja jipya na mragibishaji wa majadiliano na kwa njia hii, Injili itaweza kung’ara katika maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Maaskofu wawe ni wajenzi wa matumaini yanayobubujika kutoka katika ushuhuda wa upendo wa udugu wa kibinadamu, kwa kutangaza Injili ya huruma ya Mungu, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza kanuni maadili na utu wema. Leo hii Hungaria inakabiliwa na changamoto za maisha ya vijana, tunu msingi za kimaadili na utu wema sanjari na udumishaji wa misingi ya kidemokrasia. Katika hali na mazingira kama haya, Kanisa linapaswa kuwa ni faraja kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kuonesha ujirani mwema na kuwakirimia watu waliokata tamaa, matumaini mapya. Utangazaji na ushuhuda wa Injili usaidie kupyaisha maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Matumaini ya Hungaria kwa siku za usoni yako mikononi mwa vijana wa kizazi kipya. Katika changamoto na kinzani za kijamii au kikanisa, Maaskofu wawe ni chemchemi ya matumaini.

Papa Maaskofu
12 September 2021, 12:03