Tafuta

Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa 5-12 Septemba 2021: Kauli mbiu: "Visima vyangu vyote vimo kwako." Zab 87: 7 Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa 5-12 Septemba 2021: Kauli mbiu: "Visima vyangu vyote vimo kwako." Zab 87: 7 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa Ni Kiini Cha Matumaini!

Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Kongamano hili linapania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni ili kunogesha na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu ndani na nje ya Hungaria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kwa mara ya kwanza, Hungaria ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa kunako mwaka 1938. Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi nchini Hungaria, zaidi ya miaka 70 iliyopita yaliacha alama ya kudumu kwa familia ya Mungu nchini humo. Hapa mwaliko kwa waamini ilikuwa ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwani maadhimisho haya yalifanyika mara tu baada ya Vita ya Pili ya Dunia. Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika ngazi mbalimbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji.  Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) limeanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7.

Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Kongamano hili linapania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni ili kunogesha na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anatarajiwa kushiriki katika Sherehe ya kufunga Kongamano hili. Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest anasema, Kongamano hili ni alama ya matumaini; umoja na mshikamano wa Kanisa. Kongamano hili linaadhimishwa baada ya kuhailishwa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kutokana na maambukizi makubwa ya Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kongamano hili linaendelea kunogeshwa na Katekesi kuhusu Ekaristi Takatifu kama chemchemi ya maisha ya Kikristo pamoja na maadhimisho ya Ekaristi Takatifu Barani Afrika.

Kongamano Budapest

 

04 September 2021, 16:09