Tafuta

Vatican News

Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia: Fumbo la Pasaka!

Upendo wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha maisha na chemchemi ya wokovu! Kamwe walisiridhike na matendo ya nje, tu ili kuridhisha dhamiri zao. Huu ni mwaliko wa kuzama na kukita maisha katika amana na utajiri wa imani; uzuri na upya unaobubujika kutoka kwa Yesu, bila kuyumbishwa na mambo ambayo yatawaachia utupu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia amekwisha kukazia kuhusu: Ushuhuda wa Mtume Paulo, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu, Wito wa Mtume Paulo kutoka kwa Mungu, jinsi alivyolitesa Kanisa na jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyomwezesha kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Maadui wa Mtume Paulo walijikita zaidi katika mapokeo na Torati na kusahau upya ulioletwa na Injili ya Kristo Yesu! Hakuna Injili mpya isipokuwa ile iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Yesu! Mtume Paulo anapozungumzia kuhusu Sheria anagusia: Sheria ya Musa pamoja na Amri Kumi za Mungu, msingi wa Agano kati ya Mwenyezi Mungu na Waisraeli. Sehemu ifuatayo ya Maandiko Matakatifu inaelezea kwa muhtasari kuhusu Torati! “Na BWANA, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng’ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa BWANA atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako; ukiwa utaifuata sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.” Kum 30. 9-10.

Baba Mtakatifu amechambua pia kuhusu hatari zinazoweza kuibuka kutokana na utekelezaji wa Torati katika misingi ya uhuru kamili, hali inayoweza kupelekea baadhi ya waamini kuwa wanafiki kwa kuogopa ukweli. Kwa bahati mbaya sana hata ndani ya Kanisa kuna unafiki mkubwa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alilaani zaidi unafiki! Chanzo cha karama za Roho Mtakatifu, Sheria na Imani vinakinzana: “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Gal 3:1-3. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI, Jumatano tarehe 01 Septemba 2021. Mtakatifu Paulo anakutana na ukinzani mkubwa mbele ya Wagalatia na maneno yake yakaingizwa katika Maandiko Matakatifu kwa sababu ni matukio ya kweli yanayoweza kuthibitishwa kihistoria.

Kimsingi, Waraka huu ni Katekesi endelevu kuhusu Maandiko Matakatifu. Wagalatia wanapaswa kuendelea kujikita katika mchakato wa kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha yao, kwa sababu kwa njia ya imani wamevikwa utu mpya. Hadi sasa Mtakatifu Paulo, Mtume anazungumzia kuhusu maisha na wito wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jinsi ambavyo neema ya Mungu ilivyoleta mabadiliko makubwa katika maisha yake, kiasi cha kumtenga kwa ajili ya huduma ya Injili. Mtume Paulo anazungumzia hali halisi kwa wakati huu, kwa kuchambua na kuwaonesha jinsi ambavyo wanaweza kuonja kipindi cha neema katika maisha yao. Mtume Paulo katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu anatumia maneno makali kidogo, kuliko kawaiada yake: “Ndugu zangu” au “wapendwa”. Anawaita akisema enyi Wagalatia na zaidi ya mara mbili anawaita “wajinga”. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wameshindwa kutumia vyema akili zao, kiasi cha kuhatarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wanataka kupoteza hazina yenye thamani yaani utu na upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kwa masikitiko makubwa anapenda kuwakumbusha Wakristo wa Galatia kwamba, wanapaswa kutambua mchakato wa uinjilishaji wa awali, uliowapatia nafasi ya kujaribu kupata uhuru wa kweli unaovuka hata uwezo wao wa kufikiri.

Mtume Paulo anawauliza Wagalatia maswali makuu mawili, ili kuamsha tena dhamiri zao "zinazosinzia". Kimsingi, Wagalatia wanatambua kwamba, imani yao ni matunda ya neema inayobubujika kutoka katika Injili waliyotangaziwa na kushuhudiwa. Hii ni Injili inayokita mizizi yake katika upendo uliofunuliwa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ukweli huu ulimpelekea Mtume Paulo kusema kwa uchungu kabisa kwamba: “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu. Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.” Gal 2:20-22. Mtakatifu Paulo katika maisha na utume wake anasema, “Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulubiwa” 1Kor 2:2. Wagalatia wanapaswa kutambua Fumbo la Pasaka kuwa ni kiini cha imani na maisha yao na kamwe “miluzi mingi isiwachanganye na hatimaye, kupoteza dira na mwelekeo wa imani sahihi.

Utekelezaji wa Sheria ni muhimu, lakini imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu inachukua uzito wa hali ya juu kabisa! Anatambua kwamba, Wagalatia walikwisha kuwa na uzoefu na mang’amuzi ya uwepo wa Roho Mtakatifu katika jumuiya na Makanisa ya jirani na kwao, Roho Mtakatifu aliwashuhudia upendo na kuwakirimia karama mbalimbali. Kumbe, maisha na utume wao ni matunda ya upya wa Roho Mtakatifu. Kimsingi imani yao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa nguvu zao wenyewe. Roho Mtakatifu akawaongoza na hatimaye, kuipokea imani. Kwa sasa wanataka kumbeza na kumweka kando, jambo ambalo Mtume Paulo anasema kamwe haliwezi kukubalika! Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko, waamini wanaalikwa kutafakari kwa makini jinsi ambavyo wanaiishi imani yao. Upendo wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha maisha ya Wakristo na chemchemi ya wokovu! Kamwe walisiridhike na matendo ya nje, tu ili kuridhisha dhamiri zao. Huu ni mwaliko wa kuzama na kukita maisha katika amana na utajiri wa imani; uzuri na upya unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, bila kuyumbishwa na mambo ambayo yatawaachia utupu katika maisha.

Na kwa njia hii, wanaweza kujikuta wakiwa wanaelea kwenye ombwe bila kuzama katika undani wa maisha ya imani. Waamini wakumbuke kwamba, hata pale wanapotopea na kutoweka mbele ya Uso wa huruma ya Mungu, lakini bado Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo ataendelea kuwatafuta na kuwakirimia karama na mapaji yake. Mwenyezi Mungu bado anaendelea kutenda kazi katika historia na maisha ya mwanadamu. Jambo la msingi ni kutambua na kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, mwaliko kwa waamini kutembea katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani! Mtume Paulo anawakumbusha Wagalatia kwamba, “Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, Je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Gal 3:5. Mtakatifu Paulo anazungumzia mambo ya wakati huu “awapaye” na “kufanya”, kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake, licha ya udhaifu na ugumu wa mioyo yao. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwa pamoja na waja wake katika upendo wenye huruma. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia hekima ya kupokea ukweli wa Fumbo la Pasaka!

Katekesi Waraka
01 September 2021, 15:21

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >