Tafuta

Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaua, CCEE. Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaua, CCEE. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, CCEE

Jubilei ya Miaka 50 ya CCEE ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu hali halisi kama ilivyo Barani Ulaya; kutambua mambo msingi yanayoathiri maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, pamoja na kuibua sera na mikakati ya wongofu wa kichungaji. Utu na heshima ya binadamu; majadiliano; maendeleo sanjari na kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, linayoyaunganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi 33, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Lilianzishwa tarehe 25 Machi 1971 na Mtakatifu Paulo VI na kupewa mkazo wa pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1995 kama kielelezo cha urika wa Maaskofu Katoliki Barani Ulaya chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, “Cum et sub Romano Pontefice.” Pamoja na mambo mengine, Shirikisho hili linapania kukoleza mchakato wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ni Shirikisho linalotaka kuwa ni kielelezo cha umoja wa Kanisa katika Jumuiya ya Ulaya ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika ulimwengu wa sayansi na maendeleo makubwa ya teknolojia. Maaskofu wanatambua kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka Maaskofu Barani Ulaya kuwa “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:14), na “chumvi ya dunia” (Mt 5:13). Bara la Ulaya kwa watu wengi limekuwa ni mahali pa matumaini, lakini Mtakatifu Yohane Paulo II anakumbusha kwamba, Injili ya matumaini ya kweli inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Kumbe, Maaskofu wanapaswa kuendeleza majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Ni katika muktadha huu, kauli mbiu inayoongoza Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE ni “CCEE, Miaka 50 Ya Huduma Barani Ulaya, Kumbukumbu na Matarajio Mintarafu Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Jubilei ya Miaka 50 ya CCEE ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu hali halisi kama ilivyo Barani Ulaya; kutambua mambo msingi yanayoathiri maisha ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, pamoja na kuibua sera na mikakati ya wongofu wa kichungaji kwa ajili ya Bara la Ulaya kwa siku za usoni: Utu na heshima ya binadamu; mchakato wa majadiliano; maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya, ni muhimu sana ili Bara la Ulaya liweze kukua na kukomaa kama familia ya binadamu, mahali pa haki, amani, maridhiano na matumaini.

Maaskofu kutoka nchi mbalimbali Barani Ulaya kuanzia tarehe 23 hadi 26 Septemba 2021 wanakutanika mjini Roma ili kusherehekea Jubilei ya Miaka 50 ya CCEE. Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa ya Ufunguzi wa Jubilei hii amewataka Maaskofu kuzingatia mambo makuu matatu: Kutafakari, Kujenga na Kuona! Huu ni wakati wa ujenzi mpya wa Bara la Ulaya ambalo limechoka na kuchakaa! Ni wakati wa kusikiliza kwa makini, ili kuwasha tena moto wa njaa na kiu ya Mungu; kwa kuwashirikisha watu wa Mungu, ile furaha ya kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti na matendo ya huruma! Hiki ni kipindi cha kupyaisha Injili ya Huruma na Upendo! Ni wakati muafaka wa kulijenga na kulikarabati Kanisa la Kristo, ili liweze kung’aa kwa uzuri, upendo, huruma na ukarimu unaofumbatwa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni wakati wa kujenga ujirani mwema na ushuhuda wa imani, kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo. Watakatifu, mashuhuda na waungama imani Barani Ulaya wamejitahidi kumwilisha upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika tunu msingi za Kiinjili.

Ni wakati wa kujenga na kukarabati Kanisa la Mungu kwa kujikita katika ujenzi wa umoja katika Injili, ili hatimaye, watu wa Mungu waweze kumwona Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Watu wanataka kumwona Kristo Yesu mchungaji mwema kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Ni fursa ya kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia fadhila ya ufukara wa Kiinjili, kipaji cha ubunifu, sadaka na majitoleo thabiti ili kujenga upya Bara la Ulaya, ili hatimaye, kulipyaisha kwa sura ya ujana wa Kristo na Kanisa lake! Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican anasema, Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unagusia: Magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. 

Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa.” Waraka huu ni chombo cha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Ni chombo cha ujenzi wa umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Maaskofu wawe  mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifolaini. Maaskofu wawe mstari wa mbele kumwilisha kanuni maadili na utu wema mambo yanayopaswa kumwilishwa katika mchakato wa elimu makini. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Umoja wa Ulaya utaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama utaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya. Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, inayoendelea kushuhudiwa hata leo hii. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; sanjari na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Yote haya yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, bila Bara la Ulaya kusahau mizizi na asili yake!

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia, Ijumaa tarehe 24 Septemba 2021 alikutana na kuzungumza na Wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE. Katika hotuba yake amewapongeza Maaskofu kwa kusaidia kujenga Umoja wa Ulaya unaojikita katika kanuni na tunu msingi za Kiinjili. Amani, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu, upendo na mshikamano wa kidugu. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya haki, mshikamano, maisha, utu na heshima ya binadamu; daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha pekee. Mchakato wa haki, amani na upatanisho umepewa uzito wa pekee na Rais Sergio Mattarella.

CCEE Miaka 50
25 September 2021, 16:02