Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, tarehe 12 Septemba amekutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Makanisa Slovakia. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, tarehe 12 Septemba amekutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Makanisa Slovakia. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Ushuhuda wa Kiekumene

Papa amegusia: Umoja na udugu wa kibinadamu, changamoto ya utumwa wa maisha ya kiroho; amani na utulivu wa ndani; uinjilishaji na umuhimu wa Neno la Mungu linalopaswa kutafakariwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Baba Mtakatifu amewaambia viongozi wa Baraza la Makanisa Slovakia kwamba, imani ya Kikristo ni chachu ya umoja na udugu wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7 aliondoka na kuelekea nchini Slovakia. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Slovakia, alimtumia ujumbe wa matashi mema Rais János Áder wa Hungaria. Anawashukuru watu wa Mungu nchini Hungaria kwa wema na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake nchini Hungaria. Anawaombea heri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuwasili nchini Slovakia, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 alilakiwa na wenyeji wake na moja kwa moja akaelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Slovakia na huko akakutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Makanisa Nchini Slovakia. Katika hotuba yake, amegusia kuhusu: umoja na udugu wa kibinadamu, changamoto ya utumwa wa maisha ya kiroho; amani na utulivu wa ndani; uinjilishaji na umuhimu wa Neno la Mungu linalopaswa kutafakariwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Baba Mtakatifu amewaambia viongozi wa Baraza la Makanisa Slovakia kwamba, imani ya Kikristo ni chachu ya umoja na udugu wa kibinadamu, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujizatiti zaidi katika ujenzi wa umoja kwa kuondokana na kinzani zilizopelekea majanga makubwa katika maisha ya watu.Slovakia imepitia historia na vipindi vigumu vya dhuluma na nyanyaso za kidini pamoja na ukosefu wa uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kweli ni tunu msingi katika maisha ya binadamu. Kwa watu wengi wanataka kupigania uhuru, lakini wanapopewa uhuru huo na kujaliwa kuwa na amani na utulivu, wanaweza kujikuta wakitumbukia katika utumwa wa maisha ya kiroho. Uhuru wa Kiinjili uwawajibishe kutafuta na kuambata umoja wa Wakristo unaofumbatwa katika: maamuzi thabiti, udumifu na sadaka kama kielelezo cha imani. Uhuru wa kweli unawafumbata na kuwaambata watu wote bila ubaguzi.

Watakatifu Cyril na Method, wasimamizi wa Bara la Ulaya, wanaheshimiwa sana na familia ya Mungu huko Czech na Slovakia, kutokana na mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho, amana na utajiri mkubwa ulioachwa na ndugu hawa pacha katika maisha na utume wa Kanisa! Ni ndugu ambao wameacha urithi mkubwa wa tunu msingi za maadili, kiasi kwamba, Ukristo umekuwa ni chemchemi ya matumaini hasa wakati wa giza na mahangaiko ya watu! Walichangia kutafsiri Biblia ambayo ni msingi wa maisha ya kiroho na maendeleo ya kitamaduni; na rejea ya sheria katika nchi mbalimbali. Umoja wa Wakristo ndiyo changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Watakatifu hawa pacha wawasaidie Wakristo kujibidiisha katika mchakato wa upatanisho na umoja wa Kitaifa katika utofauti ndani ya Roho Mtakatifu. Watakatifu hawa wawasaidie Wakristo kupata umoja katika utofauti wao kama kielelezo cha uhuru ndani ya Kristo Yesu, anayelegeza minyororo ya historia iliyopita, kuganga na kuponya hofu na mashaka ya waja wake.

Watakatifu Cyril na Method walifanikiwa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ili kueneza uhuru wa Kiinjili na Umoja, kuna haja ya kujikita katika tafakari makini inayomwilishwa katika matendo. Watu wa Mungu nchini Slovakia wamebahatika kuwa na karama ya kutafakari, lakini kwa sasa wanahamasishwa kuhifadhi imani inayovyuka mang’amuzi ya falsafa na taalimungu, ili kuambata fumbo lenyewe. Viongozi wa Makanisa wasaidiane kukuza moyo na ari hii inayohitajika sana Barani Ulaya. Watu wa Mungu wasaidiwe kugundua tena ndani mwao uzuri wa Ibada ya kumwabudu Mwenyezi Mungu sanjari na kutambua umuhimu wa Jumuiya za Imani si katika utekelezaji wa programu na ufanisi wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya Neno la Mungu inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani Kristo Yesu amejitambulisha zaidi na watu kama hawa!

Ni vyema pia viongozi wa Makanisa wakakazia ubora wa huduma inayotolewa kwa wageni kama kielelezo makini cha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, hata kama bado hakuna umoja kamili unaofumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo una nguvu na mashiko. Upendeleo na huduma vinaweza kuwasaidia hata maskini kuvuka kipindi chenye changamoto kubwa za kiafya. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa ushuhuda wa safari ya umoja wa Wakristo na ukarimu wao; amani na utulivu kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji. Kwa upande wao, viongozi wa Baraza la Makanisa Slovakia wamegusia Kumbukizi la Miaka 490 ya Ungamo la Augusta pamoja na Mwongozo wa Liturujia uliotolea na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri pamoja na Kanisa Katoliki unaojulikana kama “Sala ya Pamoja” inayobubujika kutoka katika Hati ya pamoja kati ya Wakatoliki na Waluteri ijulikanayo kama “Kutoka kwenye kinzani, kuelekea kwenye Umoja”. Huu ni Waraka unaoweza kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Imegota miaka 20 tangu Sakramenti ya Ubatizo ilipotambuliwa na Makanisa ya Kikristo. Huduma makini kwa maskini ni changamoto ya kumwilisha Injili katika matendo!

Baraza la Makanisa

 

 

 

13 September 2021, 15:03